Rais John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri kwa kumteua aliyekuwa Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Wa Mambo Ya Ndani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, nafasi ya Mwigulu Nchemba inachukuliwa na Mheshiwa Dkt. Charles John Tizeba, Mbunge wa Buchosha ambaye Rais Magufuli amemteua kuchukua nafasi hiyo ya uwaziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi.
Nafasi ya Uwaziri wa Mambo ya Ndani ilibakia wazi baada ya aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Charles Kitwanga kufutwa kazi na Rais Magufuli kutokana na kile ambacho kiliarifiwa kuwa kosa la kuingia bungeni na kujibu maswali kuhusu wizara yake akiwa amelewa.
Waziri Nchemba anaenda kurithi wizara ambayo pamoja na mambo mengine bado inazungukwa na wingu la kashfa ya kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd ambayo inatuhumiwa kupewa mkataba wa Bilioni 37 wa mashine za kuchukulia alama za vidole Automated Fingerprint Information System (AFIS). Pamoja na kulipwa takribani hela zote za kufunga mashine 108, ni vituo 18 ambavyo vilikuwa vimeshafungwa mashine hizo ilipoibuka kashfa hiyo.
Pia Waziri Nchemba anakwenda kukabiliana na uhusiano unaozidi kutia shaka siku baada ya siku kati ya Jeshi La Polisi na vyama vya upinzani vikiongozwa na wabunge wa upinzani ambao wanalilalamikia jeshi hilo kutozingatia weledi hususani katika maamuzi yao ya kutoa au kutotoa vibali vya mikutano ya kisiasa ya vyama vya upinzani.
Jeshi la Polisi ambalo lipo chini ya Wizara ya Mambo ya ndani sambamba na idara nyeti kama uhamiaji na magereza, pia linakabiliwa na changamoto ya mauaji ya raia yanayozidi kushamiri mfano mauaji ya Tanga ya hivi karibuni ambapo watu wanane waliuawa.
Waziri Mwigulu Nchemba ambaye alizaliwa tarehe 7 Januari mwaka 1975 ni mchumi aliyesomea Chuo Kikuu Cha Dar-es-salaam na ni Mbunge wa Iramba Magharibi kwa tiketi ya chama tawala cha CCM.
Mengi zaidi ingia hapa www.bongocelebrity.com
No comments:
Post a Comment