Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria mkutano huo wakifuatilia taarifa toka kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage leo mjini Dodoma. |
(Habari na picha na Benedict Liwenga,
MAELEZO, Dodoma)
JUMLA ya dola Bilioni 3 za Kimarekani zinatarajiwa kutumika katika ujenzi
wa Mgodi wa Makaa ya Mawe na Chuma wa Liganga na Mchuchuma.
Kauli hiyo imetolewa Leo mini Dodoma na Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati akiongea na Waandishi wa habari mini Dodoma.
Amesema mradi huo unaojengwa kwa ubia kati ya Tanzania Kupitia Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya China ya Sichuan Hongda Group unatarajia
kuanza mwaka huu.
Mhe. Mwijage amesema kuwa fedha za kuwalipa fidia wananchi wanaozunguka
maeneo ya mradi huo ziko tayari ambapo zinatarajiwa kutumika zaidi ya bilioni
13 kwa ajili ya fidia na makazi.
Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasadia kuzalisha umeme Megawati
600 ambapo 250 zitatumika katika Kiwanda cha Chuma na nyingine 350 zitapelekwa
kwenye Gridi ya Taifa kwa ajili ya kuongeza nguvu katika nishati ya umeme.
‘’Pamoja na kuchimba chuma, Mradi wa Mchuchuma na Liganga utahusisha ujenzi
wa Kinu cha Umeme chenye uwezo wa Megawati 600”, alisema Mhe. Mwijage.
Ameongeza kuwa, Tanzania kwa sasa itakuwa na umeme wa gesi, maji na umeme
wa makaa ya mawe ambapo umeme wa makaa ya mawe utakuwa msaada mkubwa kwa nchi
kwani hautegemei tabianchi kama ilivyo vyanzo vingine vya umeme.
Mhe. Mwijage amesema kuwa katika mradi huo, Tanzania itakuwa na hisa asilimia
20 na Mwekezaji kutoka China atakuwa na asilimia 80, lakini hisa za Tanzania
zinaweza kuongezeka hadi kufikia 45.
Chini ya mradi huo, Mwekezaji huyo anatakiwa kutoa elimu kwa Vijana katika
ngazi zote za teknolojia zitakazohusika kutengeneza mgodi huo.
‘’Tutafundisha vijana wetu kwa ngazi tofauti kwani kampuni hii ni ya ubia
kati ya Tanzania na China, tuna mamlaka sawa, tuna Wakurugenzi wetu wa Tanzania
ndani ya hiyo kampuni, kwahiyo tutashiriki na hatutakuwa watazamaji”, alisema
Mhe. Mwijage.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia Viwanda,
Biashara na Uwekezaji ambaye pia ni Mtaalam katika masuala ya madini, Mhe. Dkt.
Dalaly Kafumu amesema kuwa, lengo la kuwajengea makazi wakazi wa maeneo ya
mradi huo ni kuwawezesha wakazi hao kuwa na uhusiano mzuri na mgodi
unaotarajiwa kujengwa.
‘’Serikali imeamua kuwajengea makazi wananchi ambao wanazunguka mradi Ili kuepusha
wakazi hao kutumia pesa watakayolipwa kama fidia kwa matumizi mengine na kukosa
makazi baadaye kuja kuilaumu Serikali kwamba imewadhulumu kwa kutowapa pesa za
kutosha za kujenga nyumba”, alisema Dkt. Kafumu.
No comments:
Post a Comment