Teknolojia : Tanzania yapiga hatua kubwa katika matumizi ya huduma za mitandao - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Wednesday, 25 May 2016

Teknolojia : Tanzania yapiga hatua kubwa katika matumizi ya huduma za mitandao


 
 
 Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO

Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika sekta ya mawasiliano  hadi kufikia kuwa kwenye kundi la  nchi zilizoendelea kimawasiliano Duniani.

Takwimu zinaonyesha kuwa watanzania takribani milioni 39 wana laini za simu za kiganjani pamoja na watumiaji wa intaneti takribani milioni 20 ambapo miaka ya nyuma idadi ya laini za simu za kiganjani zilikuwa 2,963,737. 

Haya ni maendeleo makubwa yanayoifanya Tanzania kuwa nchi bora kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi James Kilaba alisikika akisema kwamba,"Ukuaji wa kasi wa sekta ya mawasiliano nchini umechangia sio tu katika kuboresha maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi bali unachangia sana katika kuinua pato la Taifa".

Ukuaji huu umetokana na kuwepo kwa sera, sheria, kanuni na mfumo mzuri wa utoaji leseni za huduma za mawasiliano.

Kama wasemavyo wahenga kuwa ya Kaisari tumpe Kaisari basi sifa zote ziwaendee Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa kazi nzuri wanazozifanya. 

TCRA wana jukumu la kusimamia shughuli  hizo zote wakishirikiana na wadau wa mawasiliano nchini katika kusimamia na kuzitekeleza kwa makini sera,sheria na kanuni hizo ili kuwezesha kupatikana kwa huduma za mawasiliano nchini kote kwa kushawishi uwekezaji ,kusimamia vizuri ushindani pamoja na kutoa fursa sawa kwa watoa huduma.

TCRA inaendelea kuhakikisha kuwa rasilimali adimu zikiwemo za masafa na namba za simu zinatumika kwa makini ili kukidhi mahitaji ya Taifa na maendeleo ikiwa ni kutekeleza lengo la Serikali la kuwawezesha wananchi wote kupata habari na kuhakikisha hawaachwi nyuma katika maendeleo ndani ya karne hii ya utandawazi. 

Huduma hizi za mitandao pia zimegawanyika kutokana na kutofautiana kwa mahitaji ya wananchi. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,  huduma za mitandao ni kama ifuatavyo; Intaneti, Benki Mtandao, Elimu Mtandao, Matibabu Mtandao,Biashara Mtandao, Malipo Mtandao pamoja na Mawasiliano Mtandao.

Huduma hizi zimekuwa zikirahisisha mambo mengi hasa ya kikazi na ya kijamii,ukiangalia kwa sasa ofisi zote za umma na za binafsi wanatumia huduma za mitandao katika kufanya shughuli zao zote za kiofisi kama njia salama ya kuhifadhi data zao.

Kwa ofisi za  Serikalini wameipa huduma hii jina la Serikali Mtandao (E-Government) ambapo watumishi wa umma wanashauriwa kutumia mtandao huu ili kuhakikisha kazi zote za ofisi zinafanyika katika hali ya usalama na usiri mkubwa.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Nuru Mllao anasisitiza umuhimu wa watumishi wa Umma kupata mafunzo ya huduma za mitandao ili kuepuka matatizo yanayotokana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii wakati wakuteleza majukumu yao.

“Tumegundua kwamba watumishi wanahitaji muongozo juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, hivyo tunashkuru sana uongozi wa TCRA kukubali kutoa mafunzo kwa watumishi wetu,”alisema Bi.Nuru wakati wa mafunzo ya watumishi kuhusu masuala ya mawasiliano.

Kwa upande mwingine, jamii inatumia huduma za mitandao kwa ajili ya mawasiliano kupitia intanenti ambapo kama tulivyosema hapo awali jumla ya wananchi milioni 20 wanatumia huduma za intanenti ambazo zinahusisha matumizi ya mitandao ya kijamii kama ya facebook, instagramu,WhatsApp, Forums, Linkedin pamoja na barua pepe katika kuwasiliana kati ya mtu mmoja na mwingine.

Matumizi hayo ya mitandao ya kijamii pia ni muhimu kwa wananchi kwa kuwa inatumika kama njia rahisi katika kupashana habari kwa haraka na kufanya dunia kuonekana kama kijiji kwani watu hupata habari za masafa ya mbali kwa haraka.

Kama tunavyojua "Kizuri hakikosi kasoro", japokua matumizi ya huduma za mitandao yana faida nyingi lakini kuna baadhi ya madhara hutokea kama mitandao hiyo ikitumiwa vibaya.

Meneja Mawasiliano wa TCRA Innocent Mungy anasema kuwa ongezeko la watumiaji wa huduma za mawasiliano linaenda sambamba na ongezeko la vifaa mbalimbali vinavyowezesha mawasiliano hayo kufanyika.

"Miongoni mwa vifaa hivyo ni pamoja na simu za kiganjani,vifaa vya mawasiliano ya kiganjani (tablets), kompyuta pamoja na modemu, kadri idadi ya watu na vifaa vya mawasiliano vinavyoongezeka ndivyo matumizi mabaya ya mitandao yanazidi kuibuka,"anasema Mungy.

Kuna baadhi ya wananchi ambao tunaweza kusema hawana maadili ya kutosha ambao wanatumia vibaya huduma hizi za mitandao kwa ajili ya kujinufaisha kwa njia zisizo za halali pamoja na kuupotosha umma kwa kutuma vitu ambavyo viko  kinyume na maadili ya mtanzania.

Matumizi mabaya ya mitandao yanapelekea kuwepo kwa madhara kama ya mauaji, wizi, ukiukwaji wa maadili, ugomvi na kutokuelewana katika jamii zetu.

Ili kuzuia madhara haya ni lazima kila mmoja azingatie matumizi sahihi ya huduma za mitandao. Mamlaka inayosimamia Huduma za Mawasiliano nchini imeelezea baadhi ya mambo muhimu ambayo yatasaidia kuimarisha usalama pindi utumiapo huduma hizo.

Unatakiwa kutotumia nywila (password) moja kujiunga kwenye mtandao zaidi ya mmoja wala kuweka nywila ambazo mambo yako binafsi ambayo yanajulikana kwa watu wengi ili kuzuia mtu mwingine asipate urahisi wa kubuni kuingia katika mtandao wa mtu mwingine.

Unashauriwa kubadilisha nywila mara kwa mara pamoja na kutengeneza nywila ambayo ina muunganiko wa namba na herufi ili isiwe rahisi mtu mwingine kuibuni pia nywila ni siri yako hushauriwi kumpa mtu mwingine yoyote.

Aidha, hutakiwi kuiandika sehemu yoyote kwa ajili ya kumbukumbu wala kukubali au kujibu barua pepe zinazotoka kwa watu usiowajua kwa kuwa wanaweza kutumia kama njia ya kufahamu  nywila yako. 

Mamlaka ya mawasiliano Tanzania inawasisitiza wananchi kujifunza njia bora za kutumia mawasiliano hususani matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii ili iweze kuwanufaisha na kuendelea kukuza uchumi wa nchi kuliko kuitumia vibaya hatimaye ikaleta madhara ambayo yatasababisha matatizo kwa mtu binafsi au Taifa kwa ujumla.

Watanzania tunatakiwa kubadilika kulingana na hali halisi ya maendeleo ya nchi yetu ambapo kwa sasa teknolojia ya huduma za mitandao inazidi kukua kwa kasi hivyo kurahisisha zaidi huduma muhimu.
Huduma hizi za mitandao ni kwa ajili ya wananchi wote, hatutakiwi kuziacha  zitupite kushoto.

No comments:

Post a Comment