Kutoka Jeshini :Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha India chaipongeza TMAA - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


25 May 2016

Kutoka Jeshini :Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha India chaipongeza TMAA

Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi na Udhibiti wa Uzalishaji na Biashara ya Madini, Mhandisi Godfrey Kasekenya Kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA),( aliyesimama), akifafanua jambo katika Kikao kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (wa kwanza kushoto) na Ujumbe kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India (NDC) ulioongozwa na Admiral DM Sudan (hayupo pichani). Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi John Shija.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kulia) akikabidhiwa Ngao ya Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India ambayo alikabidhiwa na Admiral DM Sudan (kushoto). Ujumbe kutoka Chuo hicho ulifika katika Wizara ya Nishati na Madini ili kujifunza masuala ya ukaguzi wa madini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (katikati) akiwa katika kikao na Ujumbe Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India (NDC)ulioongozwa na Admiral DM Sudan (Kulia kwa Katibu Mkuu). Ujumbe huo ulifika katika Wizara ya Nishati na Madini ili kujifunza masuala ya ukaguzi wa madini. Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi John Shija.
Meneja wa Mipango na Utafiti Kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Julius Moshi, (aliyesimama), akielezea shughuli za Wakala huo mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (katikati) na Ujumbe kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India (NDC) ulioongozwa na Admiral DM Sudan (hayupo pichani). Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi John Shija.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mazingira na Ukaguzi wa Mazingira Migodini, Emanuel Sumay Kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA),(aliyesimama), akifafanua jambo katika Kikao kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (wa kwanza kushoto) na Ujumbe kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India (NDC) ulioongozwa na Admiral DM Sudan (hayupo pichani). Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi John Shija.

Na Teresia Mhagama

Watendaji kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini India (NDC) wameupongeza Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kwa umakini wake katika Usimamizi na Ukaguzi wa Shughuli za uzalishaji na Biashara ya Madini nchini, ambazo zimeifanya Serikali kupata mapato stahiki kutokana na rasilimali hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Chuo hicho Admiral D. M Sudan, katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam ambapo Ujumbe huo ulikutana na watendaji wa Wizara na TMAA wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.

Ujumbe huo kutoka nchini India uliofika Wizara ya Nishati na Madini ili kujifunza namna Wakala huo unavyosimamia shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini, ulieleza kuwa TMAA inafanya kazi nzuri kwani imekuwa ni mwangalizi wa madini nchini hasa katika juhudi zake za udhibiti wa utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi.

Awali, Meneja wa Mipango na Utafiti wa TMAA, Julius Moshi aliueleza Ujumbe huo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wakala huo ikiwemo ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na mauzo ya dhahabu kutoka kwa wazalishaji wanaotumia teknolojia ya “vat leaching” katika kuchenjua marudio ya dhahabu katika mikoa ya Mbeya, Mwanza na Geita.

Alisema kuwa katika kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016, jumla ya kilo 1,114.49 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 73.5 zilizalishwa na Mrabaha wa Shilingi Bilioni 2.9 kulipwa serikalini kutokana na shughuli hizo za uchenjuaji madini.

“Siyo hivyo tu, TMAA pia tumejikita katika kudhibiti Utoroshaji na Biashara Haramu ya Madini ambapo kazi hii tunatekeleza kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Idara ya Madini na Usalama wa Taifa kwa kufanya ukaguzi kupitia madawati maalum yaliyopo katika viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (Dar es Salaam), Kilimanjaro, Mwanza, Songwe (Mbeya) na Arusha,”,” alisema Moshi.

Alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2015 hadi Januari 2016, ukaguzi uliofanyika kupitia madawati yaliyopo katika viwanja hivyo vya ndege, umewezesha kukamatwa kwa watoroshaji wa madini katika matukio 16 yaliyoripotiwa ambayo yalihusisha madini yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.2.

Aidha Moshi alisema kuwa Wakala huo pia umeweka Wakaguzi katika migodi yote mikubwa nchini ambapo juhudi hizo zimezaa matunda kwani Ukaguzi uliofanywa na TMAA kwa kushirikiana na TRA umewezesha baadhi ya kampuni za uchimbaji madini kuanza kulipa kodi ya mapato ambapo katika kipindi cha mwaka 2009 hadi Machi 2016, kampuni mbalimbali zimelipa jumla ya Shilingi bilioni 680.5 kama kodi ya mapato.

Vilevile, alisema kuwa Wakala huo umekuwa ukifanya ukaguzi wa mara kwa mara wa shughuli za ukarabati na utunzaji wa mazingira katika maeneo ya migodi mikubwa, ya kati na midogo ambapo Wahusika wamekuwa wakipewa maelekezo yenye lengo la kuboresha hali ya mazingira kwenye maeneo yao, suala lililopelekea kuimarika kwa shughuli za utunzaji wa mazingira nchini katika maeneo ya migodi mikubwa, na baadhi ya migodi ya kati na midogo nchini.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa aliukaribisha Ujumbe huo kutoka nchini India na kukishukuru Chuo hicho kwa kuamua kujifunza masuala ya ukaguzi wa madini nchini kwani suala hilo limepelekea pande zote mbili kujadiliana na kutoa maoni yatakayoboresha Sekta ya Madini katika nchi za India na Tanzania.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali kutoka nchini India kuwekeza katika uzalishaji umeme nchini kwa kutumia vyanzo mbalimbali kama gesi asilia na Nishati jadidifu ili kuweza kuwa na umeme wa kiasi cha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad