Miundombinu : Kipaumbele chetu ni kuboresha reli ya TAZARA- Balozi Kijazi - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


10 May 2016

Miundombinu : Kipaumbele chetu ni kuboresha reli ya TAZARA- Balozi Kijazi


KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI, ENG. JOHN WILLIAM KIJAZI AFUNGUA MKUTANO  WA WATAALAM KUTOKA NCHI YA CHINA, TANZANIA NA ZAMBIA WA KUJADILI NAMNA YA KUBORESHA UTENDAJI WA SHIRIKA LA RELI LA TANZANIA NA ZAMBIA (TAZARA) KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA MWL. JULIUS NYERERE JIJINI DAR ES SALAAM.
  Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dkt. Leonard Chamuriho (kulia), akimkaribisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Eng. John William Kijazi kwenye Jengo la Ukumbi wa Mikutano la Mwl. Julius Nyerere, wakati alipofika kufungua Mkutano wa siku nne wa kujadili namna ya kuboresha utendaji wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA).
  Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Eng. John William Kijazi (kushoto), akisalimiana na ujumbe kutoka Nchini China ambao wanahudhuria  Mkutano wa siku nne wa kujadili namna ya kuboresha utendaji wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano la Mwl. Julius Nyerere. Kushoto kwake ni Balozi wa China Nchini Dkt. LU Youqing.
  Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Eng. John William Kijazi (kulia), akisalimiana na ujumbe kutoka Nchini Zambia ambao wanahudhuria  Mkutano wa siku nne wa kujadili namna ya kuboresha utendaji wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano la Mwl. Julius Nyerere.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dkt. Leornard Chamuriho (kulia), akitoa hotuba yake kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa siku nne wa kujadili namna ya kuboresha utendaji wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano la Mwl. Julius Nyerere.
 Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Eng. John William Kijazi, akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku nne unaozikutanisha Nchi Tatu China, Tanzania na Zambia kujadili namna ya kuboresha utendaji wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano la Mwl. Julius Nyerere.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Eng. John William Kijazi (wa nne kulia waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano wa siku nne wa kujadili namna ya kuboresha utendaji wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano la Mwl. Julius Nyerere.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano)

Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
SERIKALI  imesema iko tayari kuboresha reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia(TAZARA) ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi kwani ni jambo la msingi na itashirikiana na nchi za Zambia na China ili kufanikisha azma hiyo. 

Akizungumza  leo jijini Dar es salaam Katibu Mkuu Kiongozi,  Balozi  John Kijazi wakati akizindua kikao kazi kilicho shirikisha nchi tatu ambazo ni  Tanzania, Zambia na China kuhusu maboresho ya kiutendaji ya reli ya TAZARA.

“Kipaumbele chetu ni kuboresha reli ya TAZARA ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi, kikao hiki kitajadili kwa kina changamoto mbalimbali zinazoikabili reli hii, pamoja na fursa zilizopo na namna ya kutatua changamoto hizo ili kufufua uchumi wetu kupitia reli ya TAZARA” amesema Balozi Kijazi.

Balozi Kijazi amesema kwa muda sasa reli hii imekua ikifanya kazi bila ufanisi kutokana na sababu mbalimbali licha ya kuwa kiwango cha mizigo kutoka bandari ya Dar es salaam kimeongezeka kutoka tani milioni  6 mwaka 2006 hadi kufikia tani milioni 15 mwaka 2015, reli ya TAZARA imeshindwa kuwa na uwezo  wa kusaidia kusafirisha mizigo hiyo, ambapo mwaka kila mwaka uwezo wake unashuka kutoka kusafirisha mizigo tani 601,229 mwaka 2005/2006 hadi tani 87,860 kwa mawaka 2014/2015.

Vile vile, licha ya kuwa nchi za Zambia  na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeongeza uzalishaji wa shaba  bado TAZARA haikuwa na uwezo wa kuhudumia ama kusafirisha shaba hiyo, utendaji huu wa kiwango cha chini lazima ubadilike. 

Aidha, Serikali imesema ina ya dhati ya kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati, na yenye viwanda, kwa kujua kuwa uanzishwaji mzuri wa mtandao wa miundombinu hasa reli, barabara, usafiri wa anga, usafiri wa majini ni chanzo muhimu ya kutimiza azma hiyo.

Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Mawaziri la Zambia Dkt. Rowland Msiska amesema kuna haja kubwa ya kuboresha reli ya TAZARA kwa kuwa reli hiyo ina msaada mkubwa kiuchumi si tu kwa nchi za Tanzania, Zambia na China bali hata nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya  Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Aidha, amesema kuna faida nyingi za kuboresha reli ya TAZARA ikiwemo ya gharama nafuu. Usafirishaji mizigo kwa njia ya reli ni wa gharama nafuu kuliko barabara kwani inagharimu senti 5 kwa tani moja kwa umbali wa kilometa moja, huku gharama za usafirishaji kwa barabara ikiwa ni senti 12 kwa tani moja kwa umbali wa kilometa moja.

Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Biashara ya China, Bwana. Liu Junfeng amesema Serikali yake  itaendelea kushirikiana na nchi za Tanzania na Zambia ili kuboresha utendaji wa reli hiyo, huku akisisitiza uhusiano wa nchi hizi tatu umeendelea kuimarika  na unazalisha fursa nyingine za ushirikiano.

Reli ya TAZARA ilijengwa mwaka 1970 hadi 1976 kwa msaada wa Jamhuri ya watu wa China kama zawadi kwa mataifa ya Tanzania na Zambia, kwa lengo la kusaidiza kuongeza njia za usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

Post Top Ad