Matukio : Watu wenye ulemavu wajengewe miundombinu rafiki kupunguza changamoto za kimaisha. - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Monday, 16 May 2016

Matukio : Watu wenye ulemavu wajengewe miundombinu rafiki kupunguza changamoto za kimaisha.


 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge,Kazi,Ajira na Walemavu Mhe. Dkt Abdallah Possi akizungumza watu wenye ulemavu na wadau wa maendeleo nchini mara baada ya uzinduzi wa kanzidata kwa ajili ya watu wenye ulemavu nchini.
 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge,Kazi,Ajira na Walemavu Mhe. Dkt Abdallah Possi akifatilia uwasilishwaji wa kanzidata ya watu wenyes ulemavu nchini iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO. 

Na Raymond Mushumbusi - MAELEZO

Bwana Joachim Marege ni mtu mwenye ulemavu asiyeweza kutembea. Baba huyu anakofanyia kazi inabidi apande lifti hadi ghorofa ya kumi. Siku moja nikiwa nimeongozana naye kwenye lifti mara ghafla umeme ukakatika. Baada ya lift kufunguliwa nikamsaidia kutoka kwenye lift na kuendelea na safari yangu  lakini kwa ndugu huyu haikuwezekana kuendelea na safari yake kwa kupanda ngazi ilibidi asubiri kwa muda  hadi umeme utakaporudi ndo akapanda lift na kwenda ofisini kwake. Hii ni changamoto sana kwa watu wenye ulemavu katika kupata miundombinu rafiki ya kuwawezesha katika shughuli zao za kila siku na ambao idadi yao inaongezeka kila kukicha.

Mnamo Aprili 11 2016 Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu walizindua kanzi data maalum kwa ajili ya kupata takwimu za watu wenye ulemavu nchini.Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani, zaidi ya watu bilioni moja dunia sawa na asilimia 15 ya watu wote duniani wanakadiriwa kuwa na aina fulani ya ulemavu. Idadi ya watu wenye ulemavu inaongezeka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ajali, majanga ya asili na ya kusababishwa na binadamu, ongezeko la watu hasa wenye umri mkubwa, magonjwa ya kuambukiza, magonjwa ya akili na matatizo sugu ya kiafya.
 
Kuongezeka huku kwa idadi ya watu wenye ulemavu, kunasababisha mahitaji makubwa ya huduma muhimu za kijamii. Aidha, maisha ya watu wenye ulemavu yanakuwa magumu zaidi kutokana na unanyanyapaa kutoka kwa jamii kwa ujumla, hali ambayo inahitaji mabadiliko ya kimtazamo. Ni ukweli ulio wazi kwamba watu wenye ulemavu hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania wana matatizo ya upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile elimu na afya ikilinganishwa na watu ambao hawana ulemavu.
 
Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), karibu asilimia 80 ya watu wenye ulemavu wanaishi katika nchi zinazoendelea. Umaskini hupunguza uwezekano wa watu wenye ulemavu kupata huduma za kijamii na haki nyingine za kimsingi. Kwa bahati mbaya programu nyingi za maendeleo zimeshindwa kuzingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu kinyume na makubaliano ya kimataifa yanayosisitiza uzingatiaji huo kwa ajili ya maendeleo endelevu.
 
Tumeshuhudia majengo yaliyojengwa muda mrefu hata yanayojengwa sasa mengi hayazingatii mahitaji maalum kwa watu wenye ulemavu. Inabidi katika ujenzi miundombinu rafiki kwa wenye ulemevu iwekwe ili kuwapunguzia adha katika maisha watu wenye ulemavu.
 
Pamoja na umuhimu na uelewa uliopo bado upatikanaji wa takwimu sahihi ni tatizo hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania. Kwenye ngazi ya kimataifa, bado kuna tofauti kuhusu nini hasa maana ya ulemavu, suala ambalo husababisha ulinganifu wa takwimu kuwa mgumu. Katika ngazi ya kitaifa, taarifa za watu wenye ulemavu hazitoshelezi mahitaji ya kuweka misingi madhubuti ya kupanga na kutekeleza programu za maendeleo zinazolenga kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu.
 
 
Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita Serikali ya Tanzania kwa kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu, imefanya juhudi kubwa za kukusanya na kuchambua takwimu za watu wenye ulemavu kupitia tafiti mbalimbali na Sensa za Watu na Makazi za miaka ya 2002 na 2012. Pamoja na juhudi hizi bado ukusanyaji wa takwimu hizi mara zote hukabiliwa na changamoto kadhaa. Changamoto kubwa ni ile inayohusiana na mtazamo wa jamii kuhusu ulemavu na watu wenye ulemavu kwa ujumla. Tabia ya kuwaficha watu wenye ulemavu kwa visingizio mbalimbali hukwamisha upatikanaji sahihi wa idadi au taarifa ambazo zinahusiana na watu wenye ulemavu.
 
Changamoto nyingine ni watu kutojua maana halisi ya ulemavu. Watu wengi huchukulia ulemavu kuwa ni hali ya mtu kutoweza kabisa kufanya jambo fulani. Mfano kutosikia au kuona kabisa na kadhalika. Tafsiri ya ulemavu sio sahihi na huwaacha watu wengi wenye ulemavu katika tafiti na sensa zetu. Maana halisi ya ulemavu ni ile ambayo ilitolewa kwenye Tamko namba 61/106 la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wenye Ulemavu. Kulingana na Tamko hili, watu wenye ulemavu "ni watu wote wale ambao wana matatizo ya muda mrefu ya viungo , akili , uelewa , au hisia ambavyo kwa pamoja na vikwazo vingine vinaweza kusababisha ushiriki wa mtu kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za kijamii kama watu wengine”.
 
Utafiti kuhusu watu wenye Ulemavu nchini uliofanyika Mwaka 2008, ulionyesha kuwa asilimia 8 ya watu wote nchini wenye umri wa miaka 7 na kuendela walikuwa na ulemavu wa aina moja au nyingine. Taarifa za watu wenye ulemavu pia zilikusanywa kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 na kuonyesha kuwa asilimia 9 ya watu wote nchini walikuwa na ulemavu. Matokeo ya tafiti hizo na Sensa yanadhihirisha kwamba kiwango cha ulemavu ni kikubwa katika maeneo ya vijijiji kuliko mijini. Kulingana na matokeo ya Sensa ya Mwaka 2012, kiwango cha ulemavu vijijini kilikuwa ni asilimia 9.4 sawa na watu milioni 2.9 ikilinganisha na asilimia 7.3 sawa na watu 560,000 kwa maeneo ya mijini huku kiwango cha ulemavu ni kikubwa kwa Tanzania bara kwa asilimia 9 sawa na watu milioni 4.4 kuliko Tanzania Zanzibar asilimia 7 sawa na watu 55,355.17.  Pamoja na juhudi hizo Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekuwa ikikusanya pia taarifa za watu wenye ulemavu katika tafiti nyingine. Tafiti hizo ni pamoja Utafiti wa Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi na Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi.
 
Kulingana na Utafiti wa Watu Wenye Uwezo Kufanya Kazi wa Mwaka 2014, mikoa yenye watu wengi wenye ulemavu ni Tanga (asilimia 7.2), Mara (asilimia 6.3) na Dar es Salaam (asilimia 5.8).Pia inaonyesha mikoa yenye watu wengi wenye ulemavu wanaojua kusoma na kuandika ni Dar es Salaam (asilimia 89.5), Kilimanjaro (asilimia 84.7) na Mjini Magharibi (asilimia 83.7).Hali ya ajira kwa watu wenye ulemavu inaonyesha kuwa wengi wameajiriwa kwenye sekta ya kilimo. Hali ya kipato kwa watu wenye ulemavu walioajiriwa kwa mwezi ni kati ya Tshs. 65,000 na Tshs. 500,000, na kwa wale ambao wamejiajiri kipato chao ni kati ya Tshs. 65,000 na Tshs.300,000.
 
Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 yanaonesha kuwa kiwango cha kujua kusoma na kuandika ni asilimia 70.1 ya watu wote wenye ulemavu wanaojua kusoma na kuandika ikilinganishwa na asilimia 78.9 ya watu ambao hawana ulemavu. Vile vile matokeo hayo yanaonesha kuwa kiwango cha kuandikishwa shuleni kwa watoto wenye ulemavu ni kidogo pia ukilinganisha na watoto ambao hawana ulemavu kwani kulingana na matokeo hayo ni asilimia 75 ya watoto wenye ulemavu wenye umri wa miaka 7 - 13 waliokuwa wameandikishwa shule ukilinganisha na asilimia 77 ya watoto ambao hawana ulemavu.
 
Tofauti zote hizi ni matokeo ya mtazamo walio nao baadhi ya watu hapa nchini kwamba hakuna sababu ya kumpeleka mtoto mwenye ulemavu shule. Lakini, hata pale ambapo mzazi anakuwa tayari kumpeleka mtoto mwenye ulemavu shuleni miuondombinu isiyozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu inaweza kumzuia asifanye hivyo. Umbali wa kwenda shule ni chanzo cha watoto wa aina hii kutopelekwa shule.
 
Pamoja na kuwepo kwa taarifa hizi zinazotokana na Sensa na tafiti, lakini vile vile kuna takwimu ambazo hukusanywa na taasisi mbalimbali wakati wa utekelezaji wa shughuli zao za kikazi. Hata hivyo, takwimu hizi hazijawekwa pamoja na katika hali rafiki ili kumsaidia mtu au taasisi inayozihitaji. Aidha, inawezekana pia kuwa ukusanyaji wa takwimu hauzingatii vigezo vinavyokubalika na Serikali na taasisi za watu wenye ulemavu. 

kwa kutambua hali hiyo na Wizara inayoshughulikia watu wenye ulemavu kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Vyama vya Watu wenye ulemavu iliandaa kanzidata (database) ambayo ina takwimu muhimu kuhusu taarifa za watu wenye ulemavu nchini. Kwa kuanzia, kanzidata hii ina takwimu zinazotokana na Sensa na baadhi ya taifiti ambazo zimefanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
 
Kanzidata hii itakuwa ikiboreshwa mara kwa mara kwa kuingiza vyanzo vipya vya takwimu hasa vile vitokanavyo na taarifa za kiutawala kila zinapopatikana na inategemea kuwa msaada kwa watu wenye ulemavu kupata fursa mbalimbali za kujikwamua kichumi kwa sababu takwimu sasa zitakuwepo ambazo zitasaidia Serikali pamoja na asasi mbalimbali kuwawezesha watu wenye ulemavu nchini kujikwamua kiuchumi kwa kuwawezesha mikopo ya kufanya shughuliza za ujasiriamali, kuwawezesha kupata elimu na huduma bora za afya na huduma nyingine za kijamii.
 
Kanzidata hii itasaidia mambo kadhaa muhimu. Lakini kubwa zaidi ni upatikanaji wa taarifa hizi katika mfumo rafiki utakaosaidia watumiaji kufanya uchambuzi wa kina zaidi kulingana na mahitaji yao. Aidha, kanzidata hii itasaidia uelewa wa watu kuhusu ulemavu kwa ujumla na umuhimu wa kuhusisha mahitaji ya watu wenye ulemavu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
 
Mwaka huu wa 2016 dunia kwa ujumla itaanza kutekeleza Malengo Endelevu ya Maendeleo (Sustainable Development Goals).Utekelezaji huu ni wa miaka 15 ijayo baada ya kukamilika Malengo ya Millenia ya Mwaka 2015. Moja ya mapungufu yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa Malengo ya Milenia ni ukosefu wa takwimu za kutosha kwa ajili ya kufuatilia na kutathmini utekelezaji na kuachwa kwa baadhi ya sehemu ya jamii. Ndio maana, kauli mbiu kuu ya Malengo Endelevu ya Maendeleo ni "Hakuna atakayeachwa Nyuma" (Leaving no One Behind) na hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa kuna taarifa za kutosha kwa ajili ya kufuatilia na kutathmini Malengo mara utekelezaji utakapoanza baadaye mwaka huu.
 
Suala la watu wenye ulemavu ni mtambuka na hivyo linajitokeza katika Malengo yote yanayozungumzia maendeleo endelevu ya binadamu. Lengo Namba 1, kwa mfano, linazungumzia kumaliza umaskini wa aina zote kwa watu wote. Lengo Namba 4, linazungumzia kumaliza tofauti za aina yoyote kwenye suala elimu n.k. Kwa kutambua ukweli huo, Wizara husika kwa kushirikiana na wadau wengine inaandaa Andiko la Mradi ili kuweza kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi za watu wenye ulemavuni wakati muafaka kwa  wadau wote wa ndani na nje kuwa tayari kuunga mkono juhudi hizi za Serikali mtakapoombwa kufanya hivyo. Juhudi hizi ni pamoja na kujenga mfumo ambao utaiwezesha Serikali kupata takwimu za watu wenye ulemavu kwa haraka na usahihi zaidi.
 
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,kazi,Ajira na watu wenye Ulemavu Dkt Abdallah Possi ametoa wito kwa Wananchi na wadau wa maendeleo hasa asasi za kiraia kusoma taarifa hizi na kuzitumia vizuri taarifa zilizopo kwenye kanzadata hii kwa kuwa zimezingatia vigezo vyote vya takwimu bora na zimetolewa na taasisi zenye mamlaka ya Kisheria kufanya hivyo. 

Zitumieni kwa lengo moja kuu ambalo ni kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu nchini kwa kuondoa unyanyapaa katika jamii yetu na kushinikiza mabadiliko katika sera na programu za maendeleo. Wananchi mnaombwa kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wa tafiti zinazolenga kupata taarifa za watu wenye ulemavu. Toeni taarifa zao kamili ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi na hivyo kurekebisha sera na programu zake za maendeleo.

Mafaniko ya uazishwaji na utekelezaji wa matumizi ya kanzi data hii imetokana na  washirika wetu wa maendeleo ambao wamesaidia juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu na Watanzania kwa ujumla. Taarifa nyingi ambazo zipo kwenye kanzidata hii zimepatikana kwa ushirikiano na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

No comments:

Post a Comment