Mwakilishi
wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi
akizungumza katika siku ya tatu ya Mkutano Maalum wa Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa kuhusu mafanikio na changamoto za kukabiliana na tatizo la
dawa za kulevya duniani.
Sehemu ya Washiriki wa Mkutano Maaluma wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu dawa za kulevya.
Balozi
Tuvako Manongi ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu
akiwa na Bw. Rogers William Siyanga na Bw. Khamis Abdalla muda mfupi
kabla ya kulihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokutana
kujadili changamoto za dawa za kulevya. Mkutano huo umemalizika siku ya
Alhamis.
Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema, waathirika wa dawa haramu za kulevya wanatakiwa kusaidiwa badala ya kuwafunga jela.
Hayo
yameelezwa jana ( Alhamis) na Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa
Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, katika Mkutano Maalum wa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliokuwa ukijadili mafanikio, juhudi na
changamaoto za kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya duniani.
Balozi
Manongi ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu wa siku tatu na
ambao umewashirikisha Viongozi Wakuu wa Nchi, Serikali na Mawaziri
kutoka mataifa mbalimbali.
“Tunapoangalia
mbele, mkazo wetu uwe katika kuhakikisha tunapunguza idadi ya watu
wanaojihusisha na matumizi ya dawa haramu za kulevya na tunapunguza
idadi ya watu wanaofariki kutokana na matumizi ya dawa hizo” akasema
Balozi
Na
kusisitiza “ Lazima tuhakikishe wale wenye makosa madogo hawaishii jela
ambako matatizo yao yatokanayo na dawa za kulevya yatazidi kuwa makubwa
zaidi. Lakini pia tunao wajibu wa kuhakikisha huduma wanazopewa
zinazingatia afya na haki za binadamu.”
Mwakilishi
huyo wa Tanzania, amewaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa Tanzania,
kama ilivyo kwa mataifa mengine Tanzania haijapona na balaa hilo la dawa
za kulevya.
“Tanzania
hatujasalimika na balaa hili, nchi yetu, imekuwa sehemu ya kupitisha
dawa za kulevya kuelekea nchi nyingine. Lakini kiasi fulani cha dawa
hizo kina baki nchini na hivyo kuathiri wananchi wetu ambao wengine wao
tayari wameshaathirika kwa umaskini na matatizo mengine”.akaeleza Balozi
Akasema,
ni kweli kwamba, tatizo la dawa za kulevya, ni kubwa na lenye
changamoto nyingi, na ni tatizo ambalo halina ufumbuzi wa mara moja,
lakini pia ni tatizo ambalo lisiifanye jumuiya ya kimataifa kukata
tamaa.
Akasema
Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kupitia mkutano huo kuhakiksha kwamba
inakuja na mikakati mipya ikiwa ni pamoja na kutekeleza yale
yaliyopendekezwa kwenye tamko lililopitishwa kwenye mkutano huo. Balozi
Manongi ameongeza kuwa hapana shaka sera na sheria zilizopo hivi sasa
zimeshindwa kudhibiti wimbi la athari za dawa za kulevya. Na kwa
kutambua ukubwa na changamoto za tatizo hilo na athari zake kwa wananchi
wa Tanzania , Serikali imejiwekea mipango na mikakati mbalimbali ya
kulikabili.
Baadhi
ya mikakati hiyo ni pamoja na kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya
na ambao wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa na kuambukiza magonjwa
mbalimbali yakiwamo ya virusi vya ukimwi na Hepatitis B na C,
Akaelezea
pia juhudi zinazofanywa na serikali katika utungaji na uboreshaji wa
sheria zinazolenga kuwabana wasafirishaji, wauzaji na wasambazaji wa
dawa hizo, ikiwamo mikakati ya kufuatilia kwa makini mwenendo mzima wa
biashara ya dawa za kulevya , matumizi na matumizi ya madawa mengine ya
aina hiyo.
Balozi
Manongi amesema pia kwamba tatizo la dawa za kulevya linarudisha nyuma
juhudi za pamoja na kuwapatia watanzania maisha yenye hadhi na inaathiri
nguvu kazi ambayo inahitajika kufikia malengo ya kiuchumi na maendeleo
ya jamii.
“ Kama
hiyo haitoshi dawa za kulevya zinachochea uhalifu na vitendo vya jinai
vikiwamo vinavyohusisha ujagili wa wanyamapori na misitu, na kuongeza
kazi ya ziada kwa vyombo vya sheria na mfumo wa kitaifa wa utoaji huduma
za afya”. Amesisitiza Balozi
Katika
vita hivyo dhidi ya dawa za kulevya na umuhimu wa kuwasaidia
waathirika, Balozi Manongi amesisitiza kwamba ushirikiano wa pamoja
baina ya mataifa, taasisi za kimataifa na asasi zisizo za kiserikali
unahitajika sana kwa kile alichosema hakuna nchi inayoweza kukabiliana
na tatizo hilo peke yake.
Akaongeza
pia kwamba utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kimataifa, utasaidia
sana katika kuyakabili makundi na mitandao ya kihalifu na rushwa.
Hoja
zilizopewa msisitizo na wazungumzaji wengi ni pamoja na hiyo ya
kuwapatia waathirika matibabu na kutowafunga kwa kile walichosema hakuna
mzazi anayependa kuona mtoto wake akifungwa na badala yake angefurahi
kuona anasaidiwa.
Pamoja
na kuzungumzia adhabu ya kuwafunga waathirika wa dawa za kulevya,
wazungumzaji wengi pia wamepinga au kukemea adhabu ya kuwanyonga
wanaokamatwa kuhusika na masuala ya mihadarati.
Aidha
viongozi wengine walieleza kwamba wameanza mikakati ya kuwapatia
wananchi wao hasa maskini utalaamu wa kulima mazao mbadala badala ya
kutegemea kulima mazao yanayotumika kutengeneza dawa za kulevya kama
sehemu ya kuendesha maisha yao.
Wengine
wameeleza juhudi ambazo serikali zao zinafanya katika kukabiliana na
mitandao na magenge wafanyabiashara wa dawa za kulevya , juhudi
zinazohusisha pia kukamata na kutaifa mali zao.
Wako
waliokwenda mbali Zaidi kwa kutaka nchi ambazo kwa namna moja ama
nyingine zimelegeza sheria zao na kuruhusu matumizi ya dawa za kulevya
kama vile bangi basi nazo ziwajibike kwa kutoa ushirikiano na kuonyesha
utashi wa kisiasa.
Marais
wanaotoka katika nchi ambazo zimeathirika zaidi na biashara za dawa za
kulevya na mitandao ya kihalifu inayojihusisha na biashara hiyo,
walikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa, ikiwa nchi zilizoendelea na
ambazo ni wadau wakubwa hazitaonyesha ushirikiano ni wazi kwamba vita
dhidi ya dawa za kulevya itashindikana.
No comments:
Post a Comment