Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akisalimiana
na wananchi wa kijiji cha Seka na wafanyakazi wa mgodi wa dhahabu wa MMG
Gold Mine Ltd mara baada ya kuwasili mgodini hapo
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kushoto)
akimsikiliza Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya dhahabu ya MMG
Gold Mine Ltd, Harrison Abraham (kulia).
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akikagua mgodi
wa dhahabu wa MMG Gold Mine Ltd. Kushoto ni Mwenyekiti na Mkurugenzi
Mkuu wa kampuni hiyo, Harrison Abraham (kulia).
Baadhi
ya mitambo ya kuchenjulia dhahabu iliyopo katika mgodi huo wa MMG Gold
Mine Ltd uliopo katika kijiji cha Seka, wilaya ya Musoma.
Serikali
imetoa miezi minne kwa mgodi wa dhahabu wa MMG Gold Ltd uliopo katika
kijiji cha Seka wilaya ya Musoma kuanza uzalishaji vinginevyo itafutiwa
leseni.
Agizo
hilo limetolewa hivi karibuni na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo alipofanya ziara mgodini hapo kwa lengo la kujionea
shughuli zinazoendelea katika mgodi huo.
Awali
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Mashariki, Mhandisi
Juma Sementa alisema leseni ya mwanzo kutolewa kwa mgodi huo ilikua
mwaka 2002 ambapo Kampuni ya awali ilikuwa JMG Exploration Co. Limited
ambayo ilifanya utafutaji wa madini kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.
Mhandisi
Sementa aliongeza kuwa baada ya hapo eneo hilo lilibaki chini ya maombi
ya makampuni na watu binafsi mbalimbali bila kutolewa Leseni ya
utafutaji wa madini hadi mwaka 2011 ambapo kampuni ya MMG ilipata leseni
ya utafutaji wa madini na mwaka huo huo tarehe 8 Desemba ilipatiwa
leseni ya uchimbaji wa madini namba ML.449/2011.
Akizungumzia
muda huo tangu kutolewa kwa leseni husika, Profesa Muhongo alisema ni
mrefu na ilipasa kampuni hiyo iwe imeanza uzalishaji. "Haiwezekani muda
wote huo tangu leseni imetolewa mgodi upo tu na hakuna kinachozalishwa."
Aliagiza
hadi kufikia tarehe 15 Julai mwaka huu mgodi huo uwe umeanza uzalishaji
vinginevyo kampuni hiyo itapewa notisi ya kusimamisha shughuli zake na
kuondoka mgodini hapo.
Mbali
na hilo, waziri Muhongo aliiagiza kampuni hiyo kuhakikisha inalipa kodi
na tozo mbalimbali za Serikali kama sheria inavyoagiza.
Akitetea
hali hiyo, Mkurugenzi Mkuu na Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Harison
Abraham alisema uchelewaji huo umetokana na sababu mbalimbali mojawapo
ikiwa ni wajiolojia wa kampuni hiyo ambao alisema walikuja na kampuni
yake kutoka nchini Urusi na Armenia kushindwa kumaliza shughuli za
utafutaji kwa wakati.
Aidha,
katika ziara hiyo mgodini hapo, Profesa Muhongo alizungumza na baadhi
ya wananchi wa kijiji cha Seka ambao walifika mgodini hapo kwa lengo la
kuzungumza nae; walimueleza tofauti zilizopo baina yao na kampuni hiyo.
Ilielezwa
kwamba awali kampuni hiyo iliingia mkataba na Serikali ya Kijiji cha
Seka ambao unailazimu kampuni hiyo kutekeleza masuala mbalimbali ya
kijamii na kiuchumi kijijini hapo jambo ambalo wanakijiji hao walisema
halijafanyika.
Hata
hivyo wanakijiji hao walitofautiana miongoni mwao kwani baadhi yao
walisema kampuni hiyo imefanya mambo mazuri ambayo ni pamoja na
ukarabati wa shule na barabara.
Akijibu
tuhuma hizo, Abraham aliwasihi wananchi hao wawe wa kweli na waeleze
mazuri pia yaliyofanywa na kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na ajira
zilizotolewa mgodini hapo.
"Wananchi
wa Seka ni familia yangu, mbali na kwamba hatujaanza uzalishaji nimekua
nikisaidiana nao mambo mbalimbali ya kijamii," alisema.
Akizungumzia
mkataba huo, Profesa Muhongo alimuagiza Kamishna Msaidizi wa Madini,
Mhandisi Sementa kukutana na viongozi wa kijiji pamoja na wawakilishi wa
kampuni husika ili kuujadili.
Aliongeza
kwamba huenda mkataba huo ukawa ni batili na hivyo kuna umuhimu wa
kuutazama upya ili kuepusha migogoro. "Ikigundulika kama mkataba huo ni
batili tutausimamisha."
Vilevile
Profesa Muhongo aliwaasa wanakijiji hao kuepukana na tabia za kibaguzi
na badala yake kutanguliza mbele haki. Vilevile aliwaagiza viongozi wa
Serikali ya Kijiji kufanya maamuzi kwa kushirikiana na wanakijiji na
siyo kujiamulia bila ya kuwa na makubaliano ya pamoja.
No comments:
Post a Comment