Matukio : Waholanzi wawili wakamatwa na Tumbili 61 uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro. - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


25 Mar 2016

Matukio : Waholanzi wawili wakamatwa na Tumbili 61 uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro ,Kamishna Msaidizi wa Polisi,Wilbroad Mutafungwa akiwa ofisini kwake muda mfupi kabla ya kuzungumza na wanahabari.

 Na Dixon Busagaga wa Kanda ya Kaskazini .

VYOMBO vya ulinzi na usalama katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) vimefanikiwa kuwanasa wafanyabiashara wawili ndugu ,raia wa Uholanzi wakiwa katika harakati ya kusafirisha wanyama Hai 61,aina ya Tumbili kuelekea nchini  Armenia.

Wanyama hao wakiwa kwenye makasha sita tofauti ya kuhifadhia wanyama walikuwa wasafirishwe kwa ndege maalumu ya mizigo yenye namba EW/364G iliyosajiliwa nchini Belarus kupitia kampuni ya Arusha Freight Limited ya jijini Arusha.

Raia hao wa Uholanzi waliokamatwa juzi majira ya saa 1:30 jioni katika uwanja wa ndege wa KIA wametambulika majina yao kuwa ni Arten Vardanian (52) aliyekuwa na hati ya kusafiria yenye namba NWF8CKJR8  na Edward Vardanian (46) aliyekuwa na hati ya kusafiria namba NY969P96.

Meneja usalama uwanja wa ndege KIA,Kisusi Justine aliliambia Tanzania Daima mbali na kukamatwa kwa raia hao wa kigeni pia walifanikiwa kumshikilia Mtanzania ,Idd Misanya anayedaiwa kuwauzia wanyama hao.

“Wahusika hawa wawili walifika eneo la Cargo ambako walikuwa katika harakati za kusafirisha wanyama hao ndipo tulipowashikilia kwa sababu taratibu za kusafirisha wanyama Hai zilikiukwa”alisema Justine.

Kuhusu mazingira ya kukamtwa kwa watuhumiwa hao ,Justine alisema ndege hiyo inaonekana ilitua katika uwanja huo mahususi kwa ajili ya kubebeba wanyama hao na kwamba ili ruhusiwa kuondoka jioni ile baada ya kukamatwa kwao.

Kamnda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro Kamishna msaidizi wa Polisi ,Wilbroad Mutafungwa alithibitisha kukamatwa kwa raia hao na kwamba wamehifadhiwa katika kituo cha Polisi cha KIA huku uchunguzi zaidi ya tukio hilo ukiendelea.

“Mnamo Machi 23 mwaka huu majira ya saa 1:30 jioni huko uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA ) tulifanikiwa kuwakamata raia wawili wa Uholanzi wakiwa wanataka kusafirisha wanyama aina ya tumbili na tayari uchunguzi kwa kushirikiana na Wizara ya maliasili na Utalii unaendelea”alisema Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa alisema taarifa za awali zinasema wanyama hao waalisafirishwa hadi uwanjani hapo wakitokea mpakani mwa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambapo kampuni ya uwakala ya Arusha Fright Limited ilipewa kazi hiyo.

Alisema uchunguzi wa awali unaonesha ndege ya mizigo iliyokuwa isafirishe wanyama hao ni ya binafsi huku akikanusha kukamatwa kwa mtu mwingine anyetajwa kuhusika katika kuuza wanyama hao kwa raia hao wa Uholanzi.

“Mpaka sasa tumewakamata hao raia wawili ,lakini kama nilivyosema uchunguzi unaendelea tukishirikiana na wizara ya maliasili na utalii ili tuone kama kuna washiriki wengine wa tukio hilo ,so far tunao hao wawili tu”alisema Mutafungwa.

Alisema mbali na hati za  raia hao wa uholanzi kuonesha kuwa walikuwa wakiishi nchi kihalali bado vyomb vya ulinzi na usalama ikiwemo idara ya Uhamiaji vimeanza kuchunguza pia uhalali wa vibali vya raia hao vya kuishi nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad