Na Gasper Andrew, Singida
Mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Samwel Nyalandu, ameanza kwa kishindo awamu yake ya nne ya kuwatumikia wapiga kura na wananchi wa jimbo hilo, kwa kuahidi kutumia zaidi ya shilingi 1.3 bilioni kugharamia miradi ya maji katika vijiji 10.
Vijiji vitakavyonufaika na mradi huo,ni Munung’una,Ntoge,Ifombou,Itamka,Mitula,Merya,Maghojoa,Masauya,Mangida na Mkulo.
Amedai kuwa miradi hiyo ni sehemu ya kuunga mkono rais Dk.Magufuli  kauli mbiu yake ya ‘hapa kazi tu’.
Nyalandu ametangaza neema hiyo mbele ya mkutano maalumu wa baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Singida kilichopitisha bajeti ya zaidi ya shilingi 28.2 bilioni ya mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Alisema fedha hizo amepewa msaada na marafiki zake kutoka nchini Marekani na tayari wameishamkabidhi dola za kimarekani 45,000.
Akifafanua,alisema fedha hizo zitaghamia uchimbaji wa visima 10 virefu kila kimoja kikiwa na urefu wa meta 100,ununuzi wa pampu ya maji,tanki kubwa,mtambo wa umeme wa jua na kujenga kituo kimoja cha kuchotea maji kwa kila kijiji.
Nyalandu alisema kila kijiji  ili kiweze kunufaika na msaada huo,kinapaswa kufungua akaunti benki ya si chini ya shilingi laki mbili (sh.200,000).
“Hili sharti ambalo sio gumu,lengo lake ni kwamba kijiji kitatumia fedha zao hizo katika kughamia matengenezo ya miundo mbinu ya kisima cha maji pindi inapohitaji matengenezo.Kila kijiji kinapswa kuwa na kamati ya maji kwa ajili ya kusimamia mradi huo,” alisema.
Nyalandu alisema anayo imani kubwa kwamba serikali kupitia halmashauri,itaunga mkono mradi huu mkubwa wa maji,kwa kujenga vituo vya kuchotea maji na kusambaza maji hayo kwenye vijiji jirani na vijiji hivyo 10.
Katika hatua nyingine,Nyalandu amesema kuwa anayo wafadhili wengine ambao wameanza maandalizi ya kusaidia mchezo wa mpira wa miguu katika jimbo la Singida kaskazini.
Aliwataja wafadhili hao kuwa ni wachezaji wa mpira wa miguu NFL, (Waterboys), world serve, TWAF na Africa 6,000 wote kutoka nchini Marekani.