Na Mwandishi Maalum – Maelezo
Vyombo
vya habari nchini vimepongezwa kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutoa
taarifa kwa wananchi wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa
mwezi wa 10 mwaka huu.
Pongezi
hizo zimetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akiongea na
viongozi wa menejimenti ya wizara na taasisi zake kwenye kikao cha kazi
kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Prof.
Gabriel alisema kipindi cha uchaguzi vyombo vya habari vilifaya kazi
kubwa ya kuwahabarisha wananchi habari za uchaguzi kwa kuzingatia weledi
wa taaluma yao na hivyo kuwawezesha wananchi kujua mambo mbalimbali
yaliyokuwa yakiendelea hapa nchini.
Katibu
Mkuu huyo ambaye hicho kilikuwa ni kikao chake cha kwanza tangu
ateuliwe kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo mwishoni mwa mwezi wa kumi
aliahidi kuwatumikia na kuwaheshimu wafanyakazi wa wizara yake huku
akisimamia majukumu ya kazi kwa kufauata kanuni, taratibu na sheria za
utumishi wa Umma.
“Hiki
ni kikao chetu cha kujipanga kwa ajili ya kazi, ni vyema tukajipanga
huku tukijuwa matarajio ya Mhe. Rais kwetu ni yapi, wananchi
tunaowatumikia wanategemea kupata nini kutoka kwetu na mimi kama Katibu
Mkuu natarajia kupata nini kutoka kwenu”, Prof. Gabriel alisema.
Akimkaribisha
Katibu Mkuu huyo kuongea na viongozi hao Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na
Rasilimali watu Titus Mkapa alisema kikao hicho ni maalum kwa ajili ya
wizara kujadili utekelezaji wa mipango ya wizara kwa kasi.
Wakitoa
maoni yao kwa nyakati tofauti viongozi hao waliiomba Serikali iangalie
upya bajeti ya wizara hiyo ambayo ni ndogo ili iweze kuongezwa na
kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufaisi zaidi.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni
Bagamoyo (TasuBa) Michael Kadinde alisema chuo hicho kimekuwa
kikizalisha ajira kwa wanafunzi wanaosoma hapo mara baada ya kumaliza
masomo yao lakini wanafunzi wengi wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa
na ada.
“Kuna
baadhi ya wanafunzi wanajiunga na chuo hiki wakiwa na elimu ya darasa la
saba, na hivi sasa Serikali itaanza kutoa elimu bure kwa wanafunzi kwa
darasa la kwanza hadi kidato cha nne”.
“Ninaiomba
Serikali iweze kuwaangalia wanafunzi hawa wa darasa la saba ambao
wanasoma chuoni kwetu ili nao waweze kupata elimu bure sawa na wanafunzi
wa Sekondari”, alisisitiza Kadinde.
Kikao
hicho kimeitishwa kufuatia kikao cha Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
na Makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu na watendaji wakuu wa Serikali
kilichofayika mwishoni mwa wiki ambapo alieleza matarajio yake na
matarajio ya wananchi katika uongozi wake. Hivyo aliagiza kila sekta
ikae na kujipanga kufanya kazi ili kukidhi matarajio ya wananchi.
No comments:
Post a Comment