Katibu
wa Soko la Gezaulole lililopo Kiwalani Bomubomu Manispaa ya Ilala,
Salum Yusuf (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari
(hawapo pichani), Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu changamoto
wanazokabiliana nazo za kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia
sokoni hapo baada ya kuwezeshwa mafunzo ya kupinga ukatili huo na
Shirika la Equality for Growth. Kushoto Mwenyekiti wa Soko hilo, Muhidin
Waziri.
Ofisa
Ufuatiliaji na Tathmini wa Shirika hilo, Samora Julius akitoa ushauri
kwa Serikali hasa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) kushirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali katika masuala
mbalimbali yakiwemo ya ukatili wa jinsia. Kushoto ni mtaalamu wa
kujitolea wa masuala ya kijinsia kutoka nje ya nchi, Ashley.
Mwezeshaji
wa Sheria, Khadija Mohamed (kulia), akielezea mafanikio waliyoyafikia
ya kukabiliana na vitendo hivyo katika soko hilo baada ya kuwezeshwa na
EfG.
Mwezeshaji Asha Abbas akichangia katika mkutano huo.
Mfanyabiashara
wa samaki katika soko hilo, Asha Mohamed akihojiwa na wanahabari kuhusu
namna wanavyo pambana na ukatili katika soko lao hilo la Gezaulole.
Mfanyabiashara Amina Mussa akilishukuru Shirika la EfG kwa kusaidia kupunguza unyanyasaji wa kijinsia katika soko hilo.
Na Dotto Mwaibale
FAINI
zinazotolewa kwa watu wanaobainika na makosa ya unyanyasaji wa kijinsia
katika soko la Gezaulole lililopo Kiwalani Bomubomu Manispaa ya Ilala
jijini Dar es Salaam zimesaidia kupunguza vitendo hivyo kwenye soko
hilo.
Hayo
yamebainishwa Dar es Salaam leo asubuhi na Mwezeshaji wa Sheria katika
soko hilo, Khadija Mohamed wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari
waliotembea soko hilo kujua ni kwa kiwango gani vitendo hivyo
vimepungua katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth
(EfG) kutoa elimu ya kupinga unyanyasaji katika masoko ya Manispaa ya
Ilala.
"Faini
tunazo watoza wafanyabiashara wanaobainika na makosa ya kutumia lugha
chafu, kupigana na kuwadhalilisha wenzao kwa kuwakamata maunguni na
unyanyasaji mwingine zimesaidia kupunguza makosa hayo katika soko letu"
alisema Mohamed.
Alisema
mara zote matusi katika masoko yamekuwa yakichangia kuwakimbiza wateja
na ndio maana wana lishukuru shirika la EfG kwa kuwapa elimu
iliyowasaidia na kuwafanya waendelee na biashara zao kama kawaida.
Mwezeshaji
wa Sheria Amina Mussa alisema hapo awali wanaume walikuwa wamekubuhu
kwa kutukana tusi la mama jambo ambalo lilikuwa linawakera lakini hivi
sasa wanashukuru mungu baada ya wanaume hao kujitambua na kuacha matusi
hayo.
Mwenyekiti
wa soko hilo, Muhidin Waziri alilipongeza shirika hilo kwa kuwasaidia
wafanyabiashara katika masoko mbalimbali ya Manispaa ya Ilala na
kujitambua hivyo kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia masokoni.
Katibu
wa soko hilo, Salum Yusuf alisema changamoto kubwa waliyokuwa nayo hapo
awali kabla ya kufikiwa na EfG ilikuwa ni kutojua maana ya unyanyasaji
ambapo mtu aliyekuwa akishikwa mwilini au kutukanwa alikuwa hachukui
hatua yoyote.
Ofisa
Ufuatiliaji na Tathmini wa Shirika hilo, Samora Julius alitoa ushauri
kwa Serikali hasa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) kushirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali katika masuala
mbalimbali yakiwemo ya ukatili wa jinsia.
Julius
aliomba serikali kuyaunga mkono mashirika yanayofanya vizuri kwa kuyapa
ruzuku itakayosaidia kuwafikia wananchi kwa wingi na jamii kwa ujumla.
\(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com
No comments:
Post a Comment