Wanafunzi wa Stashada wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika wakiwa wameshikilia bendera
za nchi wanachama wanaoshikiana na nchi ya Tanzania kuendesha chuo hicho wakati
wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Duniani yaliyofanyika leo katika Chuo hicho
kilichopo jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni "Takwimu
Bora, Maisha Bora.
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Dkt. Albina Chuwa (hayupo
pichani) wakati akihutubia kwenye
maadhimisho ya Siku ya Takwimu Duniani yaliyofanyika leo katika Chuo cha
Takwimu Mashariki mwa Afrika jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya maadhimisho
hayo ni "Takwimu Bora, Maisha Bora".
Na Veronica Kazimoto
WATAKWIMU vijana wameaswa
kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kusaidia katika ukusanyaji na
upatikanaji wa takwimu bora zitakazosaidia katika kupanga mipango ya maendeleo.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Takwimu Duniani yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema vijana wenye taaluma ya takwimu wana nafasi kubwa katika kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji wa takwimu bora nchini.
"Ninyi watakwimu ambao bado ni vijana mna jukumu la kuhakikisha kuwa mnatumia taaluma yenu ya takwimu katika kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi ili zitumike katika kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo,” amesema Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa amesema maadhimisho haya ya Siku ya Takwimu Duniani yana nafasi kubwa katika kutambua umuhimu wa takwimu katika kufanikisha utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, amesema kuwa
kutokana na dunia kuzindua Mpango Mpya wa Maendeleo Endelevu (SDGs), ofisi yake
imejipanga vyema katika kuhakikisha takwimu bora zinapatikana kwa wakati ili
zisaidie Taifa katika kutekeleza malengo ya mpango huo.
“Kutokana na umuhimu
wa takwimu katika utekelezaji wa malengo 17 na viashiria 169 vya Mpango wa
Maendeleo Endelevu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imejipanga vyema katika
kuhakikisha takwimu zote muhimu zinapatikana na kusaidia katika utekelezaji wa
malengo ya mpango huu,” amesisitiza Dkt. Chuwa.
Siku ya Takwimu
Duniani huadhimishwa kila baada ya miaka mitano tarehe 20 Oktoba ambapo kwa
mwaka huu maadhimisho haya yameongozwa na Kauli mbiu isemayo “Takwimu Bora,
Maisha Bora”.
No comments:
Post a Comment