Najua mimi na wewe tunafamiana toka tukiwa wadogo lakini kwa faida ya wasomaji naomba ujitambulishe majina yako halisi: Asante, mimi ninaitwa Mahmoud Ramadhan Zubeiry, mtaani walizoea kuniita Mudi
Unaweza ukatuelezea kidogo kuhusu elimu yako? Shule
ya msingi nilisoma pale Mgulani, baadaye nikaenada Rutabio sekondari
kabla ya kufanya kozi mbili za awali za Uandishi wa Habari MAMET
(Maarifa Media Trust), chuo ambacho kilikuwa kinamilikiwa na akina
Jenerali Ulimwengu. Baada ya hapo, mwaka 2008 nilipata Stashahada ya
Uandishi wa Habari ya LSJ (London School of Journalism) ambayo nilifanya
online
Ilikuwaje mpaka ukaanzisha blog yako na kwanini uliiita binzubeiry?
Baada ya kufanya kazi za kuajiriwa kwa muda mrefu tangu
mwaka 1999, katika magazeti ya Dimba, Mtanzania, Rai, Bingwa, The
African na baadaye Tanzania Daima na Sayari hapa nyumbani nikaona sasa
inatosha. Lazima nisimame kama mimi kutafuta mafanikio binafsi. Ndipo
nikaamua kuanzisha blog, ambayo sasa imekuwa tovuti kamili ya michezo, www.binzubeiry.co.tz
Yalikuwa maamuzi magumu, ambayo mpinzani wa kwanza
alikuwa mke wangu, pale nilipomuambia ghafla ninaacha kazi mwaka Mei
mwaka 2012. Kama unavyojua mishahara ya kwenye vyombo vya habari hapa
nyumbani haitoshelezi kukidhi mahitaji- hivyo niliacha kazi sina
chochote. Sikuwa hata na kiwanja. Nilianza blog katika mazingira magumu
sana, sina vifaa, nahangaika kusaka habari mitaani. Nilijituma hivyo
hivyo hadi blog ikaanza kuvuma hatimaye nikaanza kupata watangazaji,
taratibu nikaanza kununua vifaa vya kazi. Alhamdulillah sasa nina vifaa
ambavyo ninafurahia kufanyia kazi, kuanzia kamera, MacBook na zagazaga
zote. Nipo full, ila tu ofisi bado popote.
Hali ikoje leo? Alhamdulillah
ninamshukuru Mungu, watoto wangu wane kati ya watano wote wanasoma
shule za kulipia, wawili kati wao sekondari kidato cha kwanza (Nurat na
Precious). Wawili wapo shule ya msingi darasa la kwanza (Prince Akbar)
darasa la pili (Princess Asia). Mungu akijaalia mwakani Sheikh Yussuf
(miaka miwili) ataanza chekechekea. Nina
shamba la embe ekari mbili eneo la Kigamboni. Nina nyumba Kigamboni huko
huko na kiwanja ambacho hakijajengwa bado cha ukubwa wa 40-40.
Unamagari mangapi? Yapo matatu tu, Passo anayotumia mke wangu, Range Rover na BMW ambazo natumia mwenyewe
Unamagari mangapi? Yapo matatu tu, Passo anayotumia mke wangu, Range Rover na BMW ambazo natumia mwenyewe
Inaelekea unapenda sana michezo, je ulisomea uwandishi wa habari upande wa michezo au ni kipaji tuu ulizaliwa nacho?
Kama utakumbuka napenda
michezo tangu nipo mdogo, nimecheza mpira mwenyewe pale KJ, lakini
sikubahatika kufika mbali. Wakati nipo shule ya msingi Mgulani
nilichaguliwa na Mwalimu Chale kama unamkumbuka katika kikundi cha
Chipukizi, ambao ndiyo tulikuwa Ball Boys wa Uwanja wa Taifa enzi hizo
mpira wa Tanzania uko juu sana. Kwa hivyo tangu hapo nikawa mpenzi sana
wa michezo. Kwa kupenda kusoma magazeti, nikapenda sana na mimi siku
moja niandike. Nilikuwa navutiwa wana na uandikaji wa watu kama Johnson
Mbwambo na Francis Chirwa. Nilitamani siku moja niwe kama wao. Nashukuru
walikuwa mabosi wangu, walinifundisha kazi katika gazeti la Dimba kwa
upendo kabisa. Kama ninasifiwa leo ni Mwandishi mzuri wa michezo, basi
kwa sababu nilipitia kwa walimu wazuri hao na wengine wengi kweli. Eric
Anthony alikuwa Mhariri wangu wa kwanza pale Dimba. Huyu jamaa alinipiga
msasa sana.
Ulipata
wapi ujasiri wa kuanzisha blog yako mwenyewe?haswa ukitazama hapo nyuma
watanzania walio wengi walikuwa wanafikiri kuanzisha blog ni lazima uwe
mtu maharufu au mtu ambaye umetoka kwa familia yenye pesa? Kama
nilivyokuambia, niliamua tu kujilipua kwa kuacha kazi na kwenda
kujiajiri mwenyewe. Nilijikabidhi kwa Mungu na leo ninamhsukuru sana
Mungu kwa kweli. Amenisamamia na anaendelea kunisimamia. BIN ZUBEIRY
ndiyo habari mjini
Hii blog unaitumia kama sehemu tuu ya vitu unavyo vipenda au pia ni sehemu ya kujiingizia kipato? Mama
hii ofisi, inafanya niishi kupitia malipo ninayopata kutokana na
vijitangazo hivyo. Ukiondoa hii tovuti, mimi mkulima na nina mpango
kuanza mradi wa ufugaji nitakapohamia kwenye nyuma yangu Januari Mungu
akipenda.
Najua watu wengi hawajui historia ya
ulipo tokea ila kwa sisi tulio kufahamu tunaona ni kama miujiza ya ukuu
wa Mungu. Je wewe ulisha wahi kuwaza wakati wa utoto wako kuwa ipo siku
moja utaishi maisha haya unayo ishi sasa hivi? Labda udokeze kidogo
maisha ulio kulia: Kuna wakati huwa nalia mwenyewe
ninapokumbuka nilipotoka, misukosuko na shida za maisha nilizopitia.
Lakini mwisho wa siku ninamshukuru Mungu tu, kwani yeye ndiye mpangaji
wa yote. Niseme nini Alpha, mimi nimetokea
familia ya kimasikini pale Keko wewe mwenyewe unajua. Tulikuwa na maisha
duni kupita duni zote. Kuna wakati nilikuwa nakwenda kwenye jalala la
soko dogo pale Keko kuokota vilivyotupwa na kutafuta vyenye nafuu ili
twende nyumbani kupika kupata chakula. Nilianza
kufanya deiwaka hata kabla sijaanza darasa la kwanza, napimisha watu
uzito kwa mzani si unakumbuka? Na ni ule mzani ulinosomesha mimi,
ilikuwa kila nikitoka shule naenda kusanya, Napata fedha za mahitaji ya
shule. Nilikuwa nakwenda kubeba mizigo
Kitumbini. Nimepiga debe, nimeuza mitumba minadani. Manyanyaso, chuki na
masimango hivyo ni vya kawaida.
Wewe
ni mtu au mwandishi wa habari pekee ulie bahatika kuona gari la
kifahari (ambalo ni custom made) la kijana wa Bhakresa; ulijisikiaje
ulipo pata fursa hiyo? Kwanza mlifahamiana wapi au ulimjuaje?
Yussuf ni rafiki yangu. Tumejuana kutokana na kazi, wao wanamiliki timu ile ya Azam FC. Alipenda ninavyoandika habari za timu yao, akawa rafiki yangu, tumeshibana hadi tumeaminiana kiasi hicho.
Na Yussuf pamoja na Zacharia Hans Poppe ni watu wenye mchango mkubwa katika maisha yangu. Hawa ni wafadhili wakuu wawww.binzubeiry.co.tz
Ni nini umejifunza zaidi au faida kubwa umepata kutokana na mitandao? Je unafikiri watanzania wanatumia vizuri mitandao?
Nimejifunza mengi sana,
nilisahau kukuambia, nilisoma kozi moja fupi pia ya namna ya kuendesha
blog mwaka 2012 ilidhaminiwa na SBL (Serengeti Breweries). Kuhusu
matumizi, si Watanzania, watu dunia nzima wapo wanaotumia vibaya
mitandao ya kijamii. Na vigumu kuwabadilisha. Hizo ni hulka. Mtu
anayejishimu hawezi kuposti picha za ngono. Hawezi kutumia mtandao
kumtukana mtu.
Nini ujumbe wako kwa Watanzania wenzako? Ujumbe
wangu kwa Watanzania na vijana wenzangu. Wamtegemee Mungu, waache
ushirikina. Mafanikio yanakuja baada ya kujituma. Lazima tufanye kazi,
tuache majungu. Tanzania itaendelea zaidi, iwapo vijana watafanya kazi
kwa bidii.
Asante sana Zubeiry! Nami ninakushukuru Alpha,
nimefanya mahojiano haya kwa heshima yako dada yangu. Huwa ninawakatalia
hata watu wa televisheni huku, kwa sababu sipendi. Naomba utoe angalizo
kuzuia watu wengine wasitumie article hii.
ANGALIZO: Si
ruhusa kwa mtu au blogger yoyote yule kutumia (publish) haya mahojiano
kwenye media yoyote au mahali popote. Hii article itaoneka hapa
alphaigogo.com , Wazalendo 25 Blog na vijimambo blog peke yake na hairusiwi kusambazwa
mahali pengine. Asante.
Credit: Mahojiano haya yameandaliwa na Alpha Igogo
No comments:
Post a Comment