>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>><<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<
MGOMBEA anayeomba kuteuliwa na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Steven
Wasira, amesema hana majina ya washukiwa wa ufisadi, ingawa uovu huo umo ndani
ya vyama vya siasa ikiwamo CCM.
Wasira anayeongozwa na kauli mbiu ya
Uadilifu na Umoja wa Watanzania; Safari ya Uhakika, alisema hayo wakati
akizungumza na wana-CCM waliomdhamini katika mikoa ya Rukwa na Katavi jana.
Alisema CCM na serikali yake ni taasisi
zilizo na misingi ya uadilifu, ingawa ndani yake kuna uwezekano wa kuwapo watu
wanaotuhumiwa kwa uhalifu huo.
Alisema ufisadi na rushwa na miongoni
mwa matatizo makubwa yanayoiathiri jamii na kwamba taifa linamhitaji kiongozi
asiyekuwa na kashfa inayomfanya atiliwe shaka katika kukabiliana na kadhia
hiyo.
“Hapa sina majina ya mafisadi lakini
ninaamini kwamba si ndani ya CCM pekee, bali hata katika vyama vingine vya
siasa, rushwa na ufisadi ni miongoni ma matatizo makubwa yanayovikabili,”
alisema.
Wasira alisema kutokana na hali hiyo,
vita dhidi ya rushwa na ufisadi inapaswa kuwa katika misingi ya hoja na
uthubutu wa kuidhibiti badala ya kumlenga mtu binafsi.
Alisema Tanzania ina taasisi imara
ambazo zikitumika ipasavyo zitachochea kuwatambua washukiwa wa ufisadi,
vitendo vinavyoashiria uhalifu huo na kuchukua hatua kwa ukali na haraka.
Wasira alisema ikiwa CCM itamteua
kuwania na hatimaye kuwania Urais, imani yake ni katika kutoa uhuru na mamlaka
zaidi kwa vyombo husika vikiwamo vya sheria, kutekeleza majukumu bila kuoneana
aibu.
Alisema, “ninapozungumzia ufisadi
sizungumzii mtu au watu, tunauzungumza ufisadi kama hoja, lakini ukweli unabaki
pale pale kwamba hata ndani ya CCM kuna viashiria vya ufisadi, lakini
haimaanishi kwamba CCM ni chama cha kifisadi.”
Aliongeza, “hata kwa upinzani kuna
ufisadi pia, hivyo ufisadi ni tatizo kubwa katika jamii yetu, kama nitapata
fursa ya kuliongoza Taifa letu nitahakikisha tunaukabili kwa nguvu zote ili
kurejesha heshima na hadhi ya nchi yetu,” alisema.
Alisisitiza umuhimu wa kupiga hatua
katika kilimo na viwanda ikiwa ni moja ya njia kuu za kukuza uchumi na
kuboresha maisha na ustawi wa wananchi.
Kwa mujibu wa Wasira, kilimo pekee
ndicho kinaweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana kuliko sekta nyingine pamoja
na kuliingizia Taifa pato kubwa zikiwamo fedha za kigeni.
Wasira alizungumzia ajira kwa vijana na
kusema hivi sasa kuna kasi ya vijana wengi kukimbia kutoka vijijini kutokana na
umasikini unaowakabili, na kwenda kukutana na umasikini mwingine mijini.
Alisema uboreshaji wa kilimo,
uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya kuongeza thamani za mazao kutatoa
hamasa kwa vijana kushiriki kilimo na kutengeneza ajira.
Leo Wasira anatarajiwa kuwasili mkoani
Kigoma kutafuta wadhamini, ukiwa ni mkoa wa 30 tangu aanze safari ya kutafuta
wadhamini Juni 3, mwaka huu ambapo alianzia mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment