Mbio za kusaka urais kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimezidi
kushika kasi baada ya mtoto wa tano wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Nyerere, Charles Makongoro Nyerere kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wakati Makongoro akichukua uamuzi huo kwa mara ya kwanza katika historia
ya familia ya Mwalimu Nyerere, mkoani Mbeya Waziri wa Nchi,Ofisi ya
Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye ameingia kwenye mbio
hizo.
Akitangaza nia yake katika eneo la Mwitongo kijijini Butiama jana,
Makongoro aliwashambulia makada wenzake ndani ya CCM ambao wanaongoza
makundi ya kuwania urais kwa kuwaita ni ‘vibaka’ wanaokivuruga chama
hicho kwa maslahi yao binafsi.
Akitoa mfano kwa baadhi ya makada wanaoongoza makundi ndani ya chama
hicho, Makongoro aliwataja kwa majina kuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa
Fedha,Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven
Wasira.
Alisema makada hao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia fedha nyingi
kuendesha makundi ya urais na akahoji sababu za kutafuta cheo hicho cha
juu kwa fedha.
CCM irudishwe kwa wazalendo kwa sababu vibaka wamekuwa na mlengo mbaya wa kukiendeleza chama hicho, alisema.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuwa maradhi ya rushwa ambayo yameiambukiza nchi nzima.
Makongoro alisema yeye ni mzalendo wa kweli na anataka kuirudisha nchi
katika misingi ya uadilifu endapo CCM itampa ridhaa ya kupeperusha
bendera katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuibuka genge la watu wachache ambao utajiri wao ni wa shaka na umejijenga kwa fedha chafu.
“Ndani ya chama tawala wamekuwapo ‘vibaka’ wachache… unajua kibaka ni
kibaka tu hata kama kapewa gari la Serikali lina bendera ya taifa mbele
atabaki kuwa kibaka tu.
“Wananijua vizuri huwa siwaonei haya kuwaambia ukweli, hawa ndiyo
wanaotuvurugia chama na hawamheshimu Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya
Kikwete,” Makongoro.
Katika hotuba yake ambayo alitumia saa mbili, Makongoro alijikita
kuzungumzia madhara yanayotokana na rushwa ndani ya CCM na alisema
baadhi ya makada wanaotumia rushwa wamezalisha makundi na mipasuko isiyo
ya lazima huku akisisitiza kuwa anachukia kuwapo makundi ndani ya chama
hicho.
Kwa mujibu wa Makongoro, hali hiyo imechochea badhi ya viongozi wa CCM
katika ngazi mbalimbali wakiwamo wenyeviti wa mikoa na wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya chama hicho kuishi kama mifugo.
Alisema hali hiyo imesababisha baadhi ya viongozi hao kuishi maisha ya
kusukumwa kwa upepo wa makundi yanayomilikiwa na watoa fedha.
Aliwaasa Watanzania wawaogope watu wanaoonekana kuwa na haraka ya kukimbilia kutawala nchi.
“Ukiona watu kazi inatangazwa ifanywe kwa utaratibu wake na mtu
aliyeiomba kazi hiyo anakiuka taratibu, muogopeni sana huyo hafai
kukukuongoza maana hata akikuongoza ataendelea kukiuka taratibu ili
ajinufaishe,” Makongoro.
MTANZANIA NA MILLARDAYO.COM
No comments:
Post a Comment