











NA PETER FABIAN, MWANZA.
KATIBU
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Mwanza , Miraji Mtaturu, amewataka
wananchi wa Jimbo la Nyamagana kumuhoji Mbunge wao, Ezekiel Wenje, fedha
za mfuko wa Jimbo hilo zaidi ya milioni 156 kwa kipindi cha miaka
mitatu iliyopita zilifanya kazi gani?.
Maturu
alisema hayo juzi kwa nyakati tofauti wakati akihutubia wakazi wa
Bugarika Kata ya Pamba na wakati wa uzinduzi shina la vijana waendesha
Pikipiki wakareketwa wa CCM (Reli), mtaa wa Nyamagana Magharibi jijini
hapa.
Katibu
huyo alidai kuwa, fedha hizo hutolewa na serikali ya CCM kwa ajili ya
kuchochea maendeleo ya jimbo hilo lakini Mwenyekiti wa mfuko ambaye ni
Wenje, amekuwa akizitumia kwa kazi tofauti na malengo yake na kuzigawa
kwa ubaguzi akipendelea madiwani wa Chama chake cha CHADEMA.
“Umefika
wakati wananchi mumuhoji Wenje, na awape majibu ya kueleweka siyo
anakuja na kuwapa vijana viroba vya pombe halafu anatukana viongozi wa
serikali na CCM na kusepa baada ya mkutano.” Alisema Mtaturu na kudai
kuwa toka mwaka 2011 hadi 2013 fedha hizo hazieleweki zimefanya shughuli gani.
Alifafanua
kwamba, kazi ya mfuko huo ni kuchochea maendeleo kwenye jimbo hili
lakini kwa kipindi hicho hazijafanya kazi iliyokusudiwa tofauti na mwaka
2014/2015 mfuko huo uliopeleka mifuko 80 saruji kwenye shule kadhaa za
Msingi, baada ya Madiwani wa CCM kuingia kwenye Kamati hiyo.
Alisema,
Wenje amekuwa akijinadi kwenye mikutano ya hadhara kuwa amefanya kazi
na kuwaletea maendeleo wananchi wa Nyamagana lakini kazi hizo
haziuonekani machoni mwao, hivyo wananchi wakati ukifika wa kutafuta
mwakilishi mwingine, ni vyema wakamtosa na kuchagua mtu sahihi kutoka
CCM badala ya kupeleka Mbunge na mtalii kama yeye.
Akizindua
tawi la vijana hao, Mtaturu aliwataka vijana wengine waige mfano wa
waendesha bodaboda hao kwa kujiunga kwenye vikundi ili Chama na serikali
viwawezeshe, pia aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha
kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili wapate fursa ya kuchagua
viongozi bora ambao anaamini watatoka CCM.
Akiwa
Bugarika, Mtaturu alimuagiza Mtendaji wa Kata ya Pamba bw Charles Musso
aondoe dampo la taka lililorundikana katika makazi ya wananchi wa
Bugarika kwani linaweza kusababisha mripuko wa magonjwa kwa wananchi na
kumtaka Diwani wa Kata hiyo Samuel Range aanze kuaga kwani ameshindwa
kuwaletea maendeleo wana Bugarika badala yake amewarundikia rundo la
uchafu huo.
Alitoa
siku nnne taka hizo ziwe zimeisha ondolewa vinginevyo atamuagiza Meya
wa jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula (CCM), Mtendaji huyo aondolewe na
kupelekwa mwingine atakayeweza kuwatumikia wananchi ikiwemo kusimaia
shughuli za maendeleo na usafi wa mazingira kikamilifu.
Mbunge
Wenje alipotafutwa na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, alidai kwamba
CCM haiwezi kumsema vizuri bila kufafanua zaidi kwa madai kuwa ana
shughuli za chama chake ikiwa pamoja na kuwa kwenye Kikao cha Kamati Kuu
jijini Dar es salaam na hawezi kujibishana na wapinzani wake kwenye
majukwaa kwa sasa.
No comments:
Post a Comment