Baadhi
ya wanawake wa kituo cha “Mabinti” kilichopo Mikocheni jijini Dar es
Salaam, chini ya Hospitali ya CCBRT wakiwa darasani kujifunza elimu
ya ushanoaji wa aina mbalimbali za vitu baada ya kutibiwa na kupona
Fistula kupitia mradi wa matibabu unaofadhiliwa na Vodacom Foundation.
Kituo hicho kinawawezesha mabinti hao kupata elimu ya kazi za mikono
ili waweze kujikimu kimaisha pindi wanaporudi makwao.
Mmoja
wasichana wa kituo cha “Mabinti” aliyepata kutibiwa Fistula na kupona
katika Hospitali ya CCBRT Cherry David ( kulia) akiwaonesha maofisa wa
Vodacom Foundation moja ya mkoba alioushana wakati walipotembelea
katika kituo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam kuangalia
maendeleo ya wanawake hao baada ya matibabu. Kituo hicho kinawawezesha
mabinti hao kupata elimu ya kazi za mikono ili waweze kujikimu
kimaisha pindi wanaporudi makwao.
Tatu
Hussen wa kituo cha “Mabinti” aliyepata kutibiwa Fistula na kupona
katika Hospitali ya CCBRT akionesha umahiri wa kutengeneza urembo
kwenye kitambaa (screen printing) wakati maafisa wa Vodacom Foundation
ambao ndio wadhamini wa mradi wa matibabu ya Fistula kupitia CCBRT
walipotembelea kituo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam
kuangalia maendeleo ya wanawake hao baada ya matibabu. Kushoto ni
Mwalimu wa kituo hicho David Mkinga, Mkuu wa Kitengo cha Vodacom
Foundation, Renatus Rwehikiza na Afisa wa Mawasiliano Abigail Ambweni
(kulia). Kituo hicho kinawawezesha mabinti hao kupata elimu ya kazi za
mikono ili waweze kujikimu kimaisha pindi wanaporudi makwao.
Mratibu
wa Kituo cha Mabinti Center kilichopo chini ya Hospitali ya CCBRT Bi.
Katia Geurts akiwaelezea maafisa wa Vodacom Foundation shughuli
zinazofanywa na kituo hicho wakati walipotembelea kituo hicho kuangalia
maendeleo ya wanawake hao baada ya matibabu. Mabinti hao wanapata elimu
ya kazi za mikono mara baada ya kupona Fistula baada ya matibabu katika
Hospitali ya CCBRT ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi
makwao.
Wanawake
waliougua na kutibiwa na hatimaye kupona maradhi ya fistula katika
Hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam wameamua kujikita katika sanaa
ya kazi za mikono kwa lengo la kujiajiri sambamba na kujikwamua na wimbi
la umasikini.
Takribani
wanawake wapatao 62, chini ya mpango madhubuti ulioratibiwa na
hospitali ya CCBRT, wamekuwa wakihitimu mafunzo mbalimbali ya kazi za
mikono zikiwemo sanaa za ushonaji wa batiki, nguo za aina tofauti,
utengenezaji wa mabegi, kofia, na ususi katika Kituo kinachoendeshwa na
hospitali hiyo kijulikanacho kama ‘Mabinti Centre’ tangu mwaka 2007.
Mratibu
wa Kituo hicho, Katia Geurts aliueleza ujumbe wa wafadhili kutoka
Taasisi ya Vodacom Foundation waliotembelea kituo hapo kuwa kituo
kinatoa mafunzo mahususi kwa wakinamama waliopona baada ya kusumbuliwa
na fistula.
“Wengi
wao wanatoka katika familia duni, hivyo mafunzo haya wanayoyapata baada
ya kumaliza matibabu ya Fistula yanakwenda kuwasaidia kujiajiri wao
wenyewe warudipo makwao jambo linalowasaidia kupunguza ukali wa maisha,”
alisema Geurts.
Aliongeza
kuwa baada ya kuhitimu mafunzo hayo kituo hicho huwapatia vyeti vya
uhitimu vinavyotambulika, sanjari na vitendea kazi vinavyoendana na
stadi stahiki aliyohitimu mwanafunzi kwa minajiri ya kuwarahisishia
upatikanaji wa mahitaji muhimu ya maisha yao.
Mkufunzi
wa Kituo hicho ambaye awali alikuwa mmoja wa waathirika wa fistula
hospitalini hapo, Tatu Hussen Jane Rugalabamu, alisema katika kipindi
cha mwaka mmoja tangu aanze kufundisha wenzake kituoni hapo amebaini
kuna idadi kubwa ya wanawake wenye matatizo ya fistula ndani ya jamii
lakini waume zao wamekuwa wakiwaficha kwa dhana ya kuficha aibu.
“Kuna
haja kubwa ya kuelimisha akinababa wawaruhusu wake zao wenye matatizo
waje kutibiwa. Fistula kwani inatibika na wala sio tatizo la kulogwa
kama wengi wanavyodhani, sisi sote hapa kwenye kituo cha mabinti
tulikuwa na maradhi hayo na sasa tumepona kabisa wanawake jitokezeni,”
alisema Rugalabamu.
Kwa
upande wake Mkuu wa Vodacom Foundation,Renatus Rwehikiza, baada ya
kukagua shughuli mbalimbali za mafunzo zinazoendelea kituoni hapo,
alisema kwa niaba ya wafanyakazi wa Vodacom na Vodafone duniani kote,
wataendelea kuwasaidia akinamama wote wanaopatwa na maradhi ya Fistula
hatua kwa hatua, sambamba na kuhakikisha wanazidisha kasi katika kampeni
inayoendelea dhidi ya maradhi hayo.
“Tutaendelea
kuwa karibu zaidi na waathirika wa Fistula kuanzia hatua ya
kuwasafirisha kutoka vijijini na mikoani kwa kuwatumia fedha kupitia
huduma yetu ya M-Pesa, pia tutakuwa pamoja wakati wote wa matibabu na
baada ya kupona tutawaunga mkono kwenye mafunzo kama haya ili kuwaletea
ustawi ulio bora kwa maisha bora kwa ajili yao na familia zao,” alisema
Rwehikiza.
No comments:
Post a Comment