Baadhi
ya wazee wa CUF kisiwani Pemba wakieleza dukuduku lao mbele ya Katibu
Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad, huko Mkanjuni Chake Chake Pemba.
Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wazee wa CUF wa
Wilaya nne za Pemba katika mkutano na wazee hao uliofanyika Ofisi za CUF
Mkanjuni Chake
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui akizungumza kwenye mkutano huo. (picha na Salmin Said, OMKR).
Na: Hassan Hamad, OMKR.
Wazee
wa Chama Cha Wananchi CUF kisiwani Pemba wameuomba uongozi wa Chama
hicho kuandaa utaratibu bora wa kutoa elimu ya wapiga kura, ili
kuhakikisha kuwa wanachama wote walioandikishwa wanashiriki katika zoezi
la upigaji kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Wakichangia
mjadala kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu mbele ya Katibu Mkuu wa
Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, kwenye kikao maalum cha wazee wa
CUF kilichofanyika Ofisi za CUF Mkanjuni Chake Chake Pemba, wazee hao
kutoka Wilaya nne za Pemba wamesema ni aibu kwa baadhi ya wanachama
kutoshiriki upigaji kura, jambo ambalo linachangia kukikosesha ushindi
chama hicho.
Kauli
hiyo imekuja baada ya kuwepo taarifa kuwa wananchi kadhaa kisiwani
Pemba hawakushiriki upigaji kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Akichangia
mjadala huo, mzee Mohammed Ali Salim kutoka Wilaya ya Mkoani amesema
elimu zaidi ya wapiga kura inahitajika, ili kuhakikisha kuwa kila
aliyeandikishwa kuwa mpiga kura anaitumia fursa hiyo.
Wazee
hao pia wameelezea haja ya kupatikana kwa vitambulisho vya Mzanzibari
Mkaazi (ZAN ID) kwa wakati muafaka, ili walionavyo waweze kuandikishwa
katika daftari la kudumu la wapiga kura mwezi ujao.
Wamesema
baadhi ya wananchi Kisiwani Pemba tayari wameshajiandikisha na kupewa
risiti, lakini bado hawajapatiwa vitambulisho vyao kwa takriban mwaka
mmoja sasa. Hivyo wameiomba taasisi inayohusika kurahisisha zoezi hilo.
Akijibu
hoja hizo, Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi wa CUF Mhe. Omar Ali Shehe
amesema Chama hicho kimejiandaa kutoa elimu kwa wapiga kura ili
kuhakikisha kuwa kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2010
hazitokei tena.
Kuhusu
vitambulisho, Mkurugenzi huyo amesema licha ya kuchelewa kwa
vitambulisho hivyo, lakini baadhi ya watu wameshindwa kuchukuliwa
vitambulisho vyao vya kupigia kura katika ofisi za tume ya uchaguzi, na
kuwahimiza kwenda kuvichukua.
Mapema
akiwahutubia wazee hao, Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif
Hamad, amesema tayari Chama hicho kimeshapata uzoefu wa kutosha wa
masuala ya kisiasa, na kuwataka wazee hao kujiandaa kwa ajili ya ushindi
katika uchaguzi ujao.
Aidha
amewataka kushirikiana na vijana ili kulinda na kudhibiti mianya
inayopelekea kupotea kwa kura za Urais, tofauti na kura za Ubunge na
Uwakilishi.
No comments:
Post a Comment