Eng.
Japhet Kivuyo kutoka kitengo cha mzani wa Vigwaza mkoani Pwani
akifafanua jambo kwa waandishi wa habari waliotembelea mzani huo jana
jijini Dar es salaam.
Taa ya
mzani wa Vigwaza ikielekeza gari lililobeba mzigo mzito kupinda kushoto
kwa ajili ya ukaguzi wa kina. Changamoto kubwa iliyopo madereva
hawafati taratibu za taa na wengine hawazielewi.
Kamera
zilizounganishwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) eneo la mzani
wa Vigwaza zikirekodi matukio mbalimbali yanayotokea katika eneo hilo
ili kutambua magari yanayotii na kuvunja sheria.
Meneja
wa Wakala wa Barabara mkoani Pwani Eng. Tumaini Sarakikya akielezea
ufanisi wa mzani wa vigwaza kwa waandishi wa habari (pichani) ambao
unapunguza foleni pamoja na rushwa kwa watumiaji wa mzani huo.
Msimamizi wa Mzani wa Vigwaza, Godo Biwi akionesha jinsi mzani huo unavyofanya kazi kwa njia ya teknolojia kwa uwazi na uharaka.
Baadhi
ya magari yaliyozidisha uzito yakiwa yameegeshwa ndani ya mzani wa
Vigwaza mkoani Pwani, ambapo gari litakaloegeshwa kwa kushindwa kulipa
fidia baada ya siku tatu litalipa faini ya dola 20 kwa siku ambazo
zitabadilishwa kwa fedha za kitanzania.
Gari
lenye mtambo wa kukagua madaraja makubwa linalomilikiwa na Wakala wa
Barabara mkoani Pwani kwa ajili ya kupima umadhubuti wa madaraja na
kuona ubora na mapungufu yake.
Imeelezwa
kuwa ufanisi wa kutumia mzani wa kisasa wa Vigwaza utafikiwa endapo
madereva na watumiaji wa barabara watajielimisha taratibu za kutumia
mizani hiyo ili kwenda na kasi ya upimaji, kuokoa muda na kuondoa
msongamano katika barabara kuu ya Chalinze-Kibaha.
Hayo
yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa wa Pwani Eng. Tumaini
Sarakikya, wakati akikagua namna mzani huo unavyofanyakazi na kusisitiza
umuhimu wa madereva kufuata maelekezo ya alama za barabarani katika
eneo hilo ili kujiepusha na uvunjaji wa sheria.
“Mzani
huu una urefu wa mita 22 hivyo utasaidia kuondoa msongamano eneo hili
kwani unauwezo wa kupima gari lote mara moja na kwa dakika moja tofauti
na mizani nyingine zinazopima gari kwa awamu ambazo hutumia dakika 3”,
amesisitiza Eng. Sarrakikya.
Eng.
Sarakikya amesema teknolojia inayotumika katika mzani huo itasaidia
kuepuka majadiliano yanayoweza kuleta hisia za rushwa na upendeleo
ambavyo ni changamoto katika utendaji kazi wa mizani hapa nchini.
Akizungumzia
utendaji kazi wa mzani huo Eng. Japhet Kivuyo, amesema takriban magari
1800 hupimwa katika mizani ya awali (weigh in motion sensor) ambapo
asilimia 60 ya magari hayo hupimwa katika mizani kuu na asilimia 40
huruhusiwa kupita bila kupimwa baada ya kuonekana yamekidhi vigezo.
Naye
Mkuu wa mzani wa Vigwaza Eng. Simfukwe Sylvester, amezungumzia umuhimu
wa wasafirishaji kupanga vizuri na kubeba mizigo inayowiana na magari
yao ili kuepusha usumbufu na uharibifu wa barabara.
Amesema
gari litakalokaidi kupima katika mzani huo litaadhibiwa kwa kulipa
faini ya dola za kimarekani elfu 2, na pia gari litakaloegeshwa kwa
kushindwa kulipa fidia baada ya siku tatu litalipa faini ya dola 20 kwa
siku ambazo zitabadilishwa kwa fedha za kitanzania.
Katika
hatua nyingine Eng. Sarakikya amesema ujenzi wa barabara kati ya
Mlandizi -Vigwaza na Vigwaza –Chalinze utaanza hivi karibuni baada ya
wakandarasi wa kujenga eneo hilo kupatikana.
IMETAYARISHWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI, WIZARA YA UJENZI.
No comments:
Post a Comment