Mke wa
Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama
Salma Kikwete akiwapungia wananchi mara baada ya kuwasili kwenye uwanja
wa Chuo cha Ualimu Nachingwea kuhudhuria sherehe za kutimiza mwaka za
vikundi vya WAMA kwenye Mradi wa Mwanamke Mwezeshe tarehe 18.3.2015.
Mamia
ya wanavikundi na viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe za kutimiza
mwaka za vikundi vya WAMA kwenye mradi wa Mwanamke Mwezeshe katika Mkoa
wa Lindi zilizofanyika Nachingwea wakifuatilia kwa makini sherehe hiyo.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akiwaonyesha waalikwa zawadi mbalimbali
alizopewa na wanavikundi vya WAMA kwenye mradi wa Mwanamke Mwezeshe
mkoani Lindi. Sherehe hizo zilifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Elimu
Nachingwea tarehe 18.3.2015.
Mke wa
Rais na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akiwahutubia mamia ya
wananchi na wana vikundi vya WAMA katika Mradi wa Mwanamke Mwezeshe
katika sherehe za kutimiza mwaka kwa vikundi hivyo zilizofanyika
Nachingwea tarehe 18.3.2015.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akimkabidhi cheti kwa Ndugu Fatuma Mchia,
Mwenyekiti wa Umoja wa Vikundi vya WAMA Kwenye Mradi wa Mwanamke
Mwezeshe kwa kuvuka lengo kwa kuingiza wanavikundi wengi kwenye mradi
huo.
Mke wa
Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama
Salma Kikwete akianzisha mchango wa papo kwa papo kwa ajili ya Mradi wa
Mwanamke Mwezeshe na kufanikiwsa kukusanya zaidi ya shilingi milioni
moja.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akizungumza na wanachuo wanaosomea ualimu
kwenye Chuo cha Ualimu Nachingwea mara baada ya kuhudhuria sherehe za
kutimiza mwaka kwa vikundi vya WAMA kwenye mradi wa Mwanamke Mwezeshe
zilizofanyia chuoni hapo tarehe 18.3.2015.
Mke wa
Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi,CCM, Mama
Salma Kikwete akishiriki katika mkutano wa ndani wa Chama cha Mapinduzi
wilayani Ruangwa akitokes Nachingwea ambako alihudhuria sherehe za
kutimiza mwaka kwa vikundi vya WAMA kwenye mradi wa Mwanamke Mwezeshe
tarehe 18.3.2015.
Mke wa
Rais na Mjumbe wa NEC Taifa ya CCM,Mama Salma Kikwete akiwasalimia
wananchi wa Kijiji cha Mnacho katika Wilaya ya Ruangwa ambao
walijikusanya kwa wingi hadi kupelekea Mama Salma kusimama na kuzungumza
nao. Mama Salma Kikwete yupo mkoani Lindi kwa ziara ya kikazi ya siku
tano.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akimsalimia mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya
Mnacho iliyoko wilayani Ruangwa. Mama Salma alikwenda shuleni hapo
kukabidhi madawati 100 aliyowaahidi wakati alipozuru shule hiyo mwaka
jana.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akikabidhi madawati 100 kwa Katibu Tawala wa
Wilaya ya Ruangwa Ndugu Sahius Kilowoko (kushoto) ambaye naye
alimkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Ndugu
Nicholaus Kombe (kulia). Mama Salma alitoa madawati hayo kwa Shule ya
Msingi Mnacho iliyoko wilayani `humo tarehe 18.3.2015.
PICHA NA JOHN LUKUWI.
Na Anna Nkinda - Maelezo , Nachingwea
Jumla
ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.9 zimetolewa kwa wanachama
wa vikundi vya kukopa na kuweka akiba vilivyopo chini ya mradi wa
Mwanamke Mwezeshe unaosimamiwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA).
Hayo
yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa sherehe za
kuadhimisha mwaka mmoja wa kuanzishwa kwa vikundi vya mradi wa Mwanamke
Mwezeshe zilizofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Ualimu
Nachingwea mkoani Lindi.
Mama
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA alisema fedha
zilizotolewa katika mkopo huo zimevuka lengo la kutoa mikopo yenye
thamani ya shilingi milioni 534 kwa mwaka na katika wilaya ya Nachingwea
mikopo yenye thamani ya shilingi 326,442,464/= ilitolewa.
“Kutokana
na kilio cha wanawake wengi na wafanyabiashara wadogo wadogo cha
ukosefu wa mikopo yenye masharti naafuu mradi huu ulianzishwa na
kuwawezesha wanavikundi vya hisa kukopeshana kwa masharti naafuu
ikiwemo kiasi kidogo cha ziada ya mkopo ambayo kwa lugha ya kibenki
huitwa riba”, alisema.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alifafanua kuwa mradi wa Mwanamke Mwezeshe ambao ulianza
kufanya shughuli za kijamii mwanzoni mwa mwaka jana katika wilaya za
Rufiji, Kilwa, Liwale, Lindi vijijini, Nachingwea kwa ufadhili wa
Financial Sector Deeping Trust (FSDT) unalenga kuanzisha vikundi 3000
vyenye jumla ya wanavikundi 60,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Alisema
mradi huo pia umetoa ajira kwa wakazi wa maeneo ya mradi wapatao 120
ambao kati ya hao 48 wapo wilaya ya Nachingwea ambao wamepata mafunzo ya
ukufunzi wa wanavikundi na sasa wanafanya kazi ya kutoa elimu kwa
vikundi katika maeneo yao.
Mama
Kikwete alisema, “Vikundi hivi ni msingi mzuri wa kufanikisha jitihada
za kupunguza umaskini wa kipato kwa wanawake, ni mfumo unaowezesha
kuwafikia watu wengi zaidi kwa muda mfupi na huwavutia watoa huduma za
jamii kwani mtandao wa vikundi hivi unarahisisha kuwafikia wananchi”.
Akisoma
ripoti ya vikundi hivyo Godfrey Makwinya ambaye ni katibu umoja wa
walimu alisema madhumuni ya umoja huo ni kuviunganisha vikundi vya
hisa vya wilaya hiyo ili umoja uweze kusimama na kuleta ufanisi katika
vikundi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa
kumbukumbu za fedha kwa wanachama wake na kutatua changamoto
zinazowakabili katika biashara zao.
Makwinya
alisema umoja huo una vikundi 48 ambavyo vimemaliza mzunguko wa mwaka
wa kwanza vyenye wanachama 1294 kati ya hao wanaume ni 204 na wanawake
1090. Vikundi vimeweza kujiwekea akiba ya shilingi 187,842, 650/=,
kugawana shilingi 235,653,730/= na kupata faida ya shilingi
47,811,080/=.
Alizitaja
changamoto zinazowakabili kuwa ni kutokuwa na vifa vya kutosha vya
kuendesha ofisi vifaa hivyo ni samani za ofisi na Computer, wanahitaji
msaada wa kitaalam ili waweze kufungua benki yao na uhaba wa fedha za
kuendeshea shughuli za umoja wa walimu wa vikundi.
“Tunahakika
kama malengo yetu yatakuwa kama tulivyopanga na baadhi ya changamoto
zikatatuliwa, utakuwa umepunguza suala la umaskini kwa kiasi kikubwa
kama si kuondoa kabisa katika wilaya yetu ya Nachingwea”, alisema
Makwinya.
Kwa
upande wa wanavikundi vya hisa ambao wamenufaika na mradi huo
walimshukuru Mama Kikwete kwa kuanzisha mradi wa Mwanamke Mwezeshe na
kuwapanua akili wanawake walioko vijijini ambao wamekopa fedha na
kuzifanyia biashara na hivyo kujikwamua kiuchumi.
Zuhura
Matola alisema, “Nilishindwa kusomesha watoto kwa kukosa ada, nikaamua
kujiunga na vikundi vya hisa baada ya miezi minne ya kuweka akiba
nikachukua mkopo na kuanzisha biashara ya kupika maandazi. Katika hela
ya gawio nimefyatua matofali nataka kujenga nyumba ya kuishi.
“Hela
ya gawio iliyobaki nimenunua vitenge ambavyo naviuza kwa kuwakopesha
watu. Hivi sasa mimi na familia yangu tunakula, tunavaa na wanangu
wanasoma bila ya matatizo hakika mradi huu umetusaidia sisi wanawake
ambao uchumi wetu ulikuwa mdogo tumeweza kufanya mambo yetu wenyewe bila
ya kuomba msaada wa kifedha kutoka sehemu ningine”.
Hadi
kufikia mwishoni mwa mwaka jana mradi wa Mwanamke Mwezeshe ulishaunda
vikundi 1,047 na kuwafikia wanavikundi 26,710 kati ya hivyo vikundi 438
viko wilaya ya Nachingwea na vina wanavikundi 11605.
Miongoni
mwa shughuli za mradi ni kutoa mafunzo ya kuweka akiba ambayo
yatawawezesha wanavikundi kuweka akiba za jumla ya shilingi bilioni moja
na nusu kwa kipindi cha miaka mitatu ya mradi, kufikia mwishoni mwa
mwaka jana mradi ulikusanya shilingi 1,518,643,430/= na hivyo kuvuka
lengo la mwaka la kukusanya akiba ya shilingi milioni 500/=.
No comments:
Post a Comment