Elimu na Maisha : Mama Salma Kikwete Azuru Mafia na Kutembelea Shule ya Sekondari Bweni - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Saturday, 14 March 2015

Elimu na Maisha : Mama Salma Kikwete Azuru Mafia na Kutembelea Shule ya Sekondari Bweni

 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) Dkt. Ramadhan Dau akitoa maelezo mafupi kuhusu Shule ya Sekondari Bweni iliyoko katika Kata ya Kanga wilayani Mafia ambayo imejengwa na “Mafia Island Development Foundation, MIDEF”. Dkt. Dau ni mmoja wa viongozi wa Taasisi hiyo. Mama Salma alitembelea  Shule hiyo tarehe 13.3.2015. Waliokaa kutoka kushoto ni Mbunge wa Mafia Mheshimiwa Abdulkarim Shah, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo,  Ndugu Mohamed Msosa, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo na mwisho ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mafia.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bweni iliyoko katika Kata ya Kanga wilayani Mafia  tarehe 13.3.2015.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea na wananchi wa Kijiji cha Bweni katika Kata ya Kanga waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kusalimiana naye.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea na wananchi wa Kijiji cha Bweni katika Kata ya Kanga waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kusalimiana naye.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea na wananchi wa Kijiji cha Bweni katika Kata ya Kanga waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kusalimiana naye.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifurahia zawadi alizopewa na akina mama wajasiriamali wa Kata ya Kanga huko Mafia mara baada ya kumaliza kuzungumza na wanafunzi na wananchi wa eneo hilo.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifurahia zawadi alizopewa na akina mama wajasiriamali wa Kata ya Kanga huko Mafia mara baada ya kumaliza kuzungumza na wanafunzi na wananchi wa eneo hilo.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifurahia zawadi alizopewa na akina mama wajasiriamali wa Kata ya Kanga huko Mafia mara baada ya kumaliza kuzungumza na wanafunzi na wananchi wa eneo hilo.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizungumza na walimu wa Shule ya Sekondari Bweni iliyoko huko Mafia mara baada kuongea na wanafunzi.
  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) Dkt. Ramadhan Dau alikuwa ni miongoni mwa viongozi mbalimbali waliofika kwenye uwanja wa ndege wa Mafia kwa ajili ya kumpokea Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipowasili wilayani humo tarehe 13.3.2013 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimsalimia mtoto mwenye ulemavu wa ngozi/albino aliyekuwa amebebwa na mama yake. Mama Salma alikutana na mtoto huyo wakati alipowasili kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mafia.PICHA NA JOHN LUKUWI
 
Na Anna Nkinda – Maelezo, Mafia 
Wazazi na walezi wilayani Mafia wametakiwa kutokubali kupokea mahari za watoto wao wakiwa wanafunzi bali wawasimamie na kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kufika elimu ya chuo kikuu. 
 Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanafunzi pamoja na wazazi wa shule ya Sekondari Bweni iliyopo kata ya Kanga wilaya ya Mafia mkoani Pwani. 
 Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema baadhi ya wazazi wanapokea mahari za watoto wao na kuwaozesha wakiwa na umri mdogo jambo ambalo huwafanya kukatisha masomo yao na wanawanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu. 
 “Mtoto akisoma atakuwa na maisha mazuri hapo baadaye ataweza kufanya kazi za kitaalamu za kuajiriwa au kujiajiri yeye mwenyewe, kujikomboa na umaskini, kuwasaidia wazazi wake, ataepukana na mimba za utotoni na kujiepusha na maradhi yanayotokana na ngono zembe kwani elimu ni msingi wa kila kitu”. 
Wanawake wenzangu mtoto wako wa kike akiwa mwali usikubali kumuweka ndani ili asubiri mwanaume wa kumuoa na ukisikia mmeo kapokea mahari ili binti huyo aolewe katoe taarifa sehemu inayohusika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake”, alisisitiza Mama Kikwete. 
 Kwa upande wa wanafunzi aliwaasa kujiepusha na kitendo cha kujiingiza katika mapenzi wakiwa na umri mdogo bali wasome kwa bidhii , wawe na nidhamu kwa walimu wao na kuwa na malengo katika maisha yao kwa kufanya hivyo watatimiza ndoto zao. 
 Alisema, “Wanangu someni kwa bidii msitake utajiri wa haraka, watoto wa kiume mnaacha kwenda shule, mnakatisha masomo na kukimbilia kuvua samaki kwa kudhani kuwa mtapata maendeleo kumbukeni elimu ni urithi usioweza kutoweka katika maisha yenu”,. 
 Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwahimiza wazazi kwenda Hospitali kupima ugonjwa wa saratani za shingo ya kizazi, matiti na tezi dume ambazo zikigundulika katika hatua ya awali mgonjwa anaweza kutibiwa na kupona kabisa. 
 Kuhusu utunzaji wa ardhi Mama Kikwete alisema wilaya hiyo imejaliwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba inayowavutia watu wengi na kuwasihi wananchi kutoiuza kiholela bali waitunze, kama kuna wawekezaji utaratibu maalum ufuatwe. 
 Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng. Evarist Ndekilo aliwahimiza wananchi hao kuona umuhimu wa kuwarithisha watoto wao elimu ambayo ni ufunguo wa maisha na siyo mali kama uvuvi, ng’ombe na mashamba. 
 Eng. Ndekilo alisema atakuwa mkali kwa mtu yoyote atakayekatisha elimu ya mtoto wake na katika suala la mtoto kuacha shule baada ya kupewa ujauzito mahakama ndiyo itakayotoa maamuzi na siyo wazazi kumalizana wenyewe kwa wenyewe. 
 Akisoma taarifa ya shule Mwalimu mkuu Mohamed Msossow alisema shule hiyo ilifunguliwa mwaka 2007 ikiwa na walimu wanne na wanafunzi 199 kati ya hao wavulana walikuwa 147 na wasichana 52 . Hivi sasa kuna walimu 20 na wanafunzi 131 kati ya hao wavulana 61 wasichana 70 na walimu 20. Aliyataja mafanikio waliyo nayo ni walimu wa kutosha wa masomo ya sanaa, vitabu vya kutosha vya masomo ya sayansi na sanaa kwa uwiano wa mwanafunzi mmoja kwa kitabu kimoja, madarasa ya kutosha, ushirikiano mzuri na jamii inayowazunguka na matokeo mazuri ya kitaaluma katika mitihani ya kidato cha pili na cha nne. 
 “Changamoto zinazotukabili ni upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati, nyumba za walimu na vifaa vya maabara, kutokana na mazingira ya mahali shule ilipo shule inahitajika kuwa na usafiri ili kurahisisha walimu kufika wilayani”. 
 Idadi ndogo ya wanafunzi inayosababisha kupata mgao mdogo wa fedha ya ruzuku kutoka Serikalini na kusababisha ugumu katika kuendesha shughuli mbalimbali za shule, ukosefu wa umeme na uhaba wa vyanzo vya maji”,alisema Mwalimu Msossow. Mama Kikwete yuko wilayani humo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na akiwa shuleni hapo aliwapatia wanafunzi zawadi ya shilingi milioni moja. 
 Shule ya Sekondari Bweni imejengwa na Taasisi ya Maendeleo ya Kisiwa cha Mafia (MIDEF) chini ya usimamizi wa Dkt. Ramadhan Dau ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuikabidhi kwa Serikali ambapo hivi sasa ni Shule ya Sekondari ya kata ya Kanga.

No comments:

Post a Comment