Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia nyumba
iliyoporomoka dari na kujeruhi wakazi wake watatu hapo Mtaa wa Ukutani
Mjini Zanzibar.
Kulia ya Balozi Seif ni Mmiliki wa Nyumba Hiyo Bwana Mzee Abdulla Juma.
Balozi
Seif akiwaagiza watu wanaoishi ndani ya nyumba iliyoporomoka dari Mtaa
wa Ukutani kuhama ili kunusuru maisha yao kutokana na uchakavu wa nyumba
hiyo.
Aliyepo mwanzo kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mjini Kanali Mstaafu Abdi
Mahmoud Mzee.
Balozi
Seif akiwa pamoja na Mmiliki wa nyumba iliyoporomoka Dari eneo la
Ukutani Bwana Mzee Abdulla Juma na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Kanali
Mstaafu Abdi Mahmoud Mzee wakiangalia hali halisi ya mazingira ya nyumba
hiyo.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza wananchi
wanaoishi kwenye nyumba mbovu na zile zilizochakaa ndani ya Mji Mkongwe
wa Zanzibar wafanye utaratibu wa kuhama kwenye nyumba hizo mapema
iwezekanavyo ili kunusuru maisha yao.
Alisema
Serikali kamwe haitakuywa tayari kuachia wananchi wake wanaendelea
kuishi katika mazingira ya hatari wakati njia za kuepuka hatari hizo
zipo na wala hazina gharama yoyote.
Balozi
Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi ya kukagua Nyumba
ya Bwana Mzee Abdulla Juma ambayo iliporomoka dari sehemu ya sebule na
kujeruhi wakaazi watatu wa nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Ukutani Mjini
Zanzibar.
Watu
waliojeruhiwa ni wadogo wa Mmiliki wa Nyumba Hiyo Bwana Haroun Abdulla
Juma na Fahim Abdulla Juma waliolazwa Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja kwa
matibabu pamoja na Peter Monga aliyetibiwa na kuruhusiwa kurejea
nyumbani.
Balozi
Seif aliutaka uongozi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kuendelea
kuzifanyia uhakiki nyumba zote zilizomo ndani ya mji mkongwe na hatua
zichukuliwe mara moja na taasisi zinazohusika katika kuwahamisha wakaazi
wanaoishi kwenye nyumba zisizostahiki kuishi watu.
Mapema
Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana Mzee Abdulla Juma alimueleza Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mkasa huo umetokea majira ya saa 11.00
za asubuhi wkati dari ya nyumba hiyo sehemu ya sebule ilipoporomoka.
Bwana
Mzee alisema wakaazi wa nyumba hiyo kwa kushirikiana na majirani
walilazimika kuuvunja mlango mkuu wa nyumba hiyo ili kumnusuru Mtoto wa
mdogo wake aliyelazwa Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja baada ya kuvunjika
mguu.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Mussa
Awesu Bakari alisema watendaji wa Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na
wataalamu wa Taasisi za majengo na ujenzi tayari wameshafanya uhakiki wa
Nyumba 75 zilizomo ndani ya Mji Mkongwe .
Nd.
Mussa alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba zoezi hilo
linaendelea kwa lengo la kubaini nyumba zisizofaa kutumiwa kwa makazi ya
kawaida ya binaadamu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment