Na Saidi Mkabakuli, Mpanda
Kufuatia
kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda,
mkoani Katavi, Serikali imewaasa watumiaji wa uwanja huo kutunza
miundombino ya uwanja huo ili kuweza kuhudumia wakazi na wageni wapitao
uwanjani hapo kwa muda mrefu.
Wito
huo umetolewa na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo
kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati
walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu katika Uwanja wa
Ndege wa Mpanda, mkoani Katavi.
Bibi
Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
imekamilisha kazi ya kuufanya uwanja huo uwe wa kiwango kizuri tayari
kwa kutumika kwa ndege za binafsi na biashara, hivyo uongozi wa uwanja
huo hawana budi ya kuhakikisha miundombinu ya uwanja huo inatunzwa
ipasavyo.
“Kama
munavyofahamu Serikali imekuwa ikiwekeza sana katika uendelezaji wa
miundombinu ya usafiri nchini hasa kuendelea kuboresha miundombinu ya
usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi na kuendelea na kazi ya ujenzi na
ukarabati wa viwanja vya ndege katika maeneo ya kimkakati, hivyo kuna
haja ya kuunga mkono jitihada hizi za Serikali,” aliasa Bibi Mwanri.
Akitoa
taarifa ya uendelezaji uwanja huo kwa msafara wa timu ya ukaguzi,
Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Bw Seneti Lyatuu alisema uwanja huo
umeboreshwa na hivyo, unaweza kutumika kutua na kuruka ndege za kiwango
cha kati na hata zile ndege kubwa zinaweza kutua kwa dharura.
“Uwanja
huu umekarabatiwa na barabara ya kuruka na kutua ndege imerefushwa kwa
kiwango cha lami kutoka urefu wa mita 1,500 na upana wa mita 30 hadi
kufikia urefu wa mita 1,820 na upana wa mita 30,” alisema Bw. Lyatuu.
Kwa
mujibu wa Meneja huyo, kukamilika kwa uwanja huo kumevutia idadi ya
abiria wanaoutumia uwanja huo kutoka abiria 285 mwaka 2009 hadi 2,390
mwaka 2013/14.
Kwa
mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 -
2015/16), Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa uwekezaji mkubwa
katika miundombinu ya nishati, usafirishaji (bandari, reli, barabara na
usafiri wa anga), maji (safi, taka na ya uzalishaji) na TEHAMA.
Serikali
imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa
kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo kuu la Mpango huu ni
kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi ya ukuaji
mpana wa uchumi na unaolenga watu walio masikini zaidi.
Mpango
wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja
wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa
utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na
tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa.
Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Timu
ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
ikiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda kujionea shughuli mbalimbali
za maendeleo uwanjani hapo.
Kiongozi
wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kushoto) akizungumza na Meneja wa Uwanja
wa ndege wa Mpanda, Mkoani Katavi Bw. Seneti Lyatuu (Kulia).
Anayefuatilia mazungumzo ni Bw. Omary Abdallah ambaye Kaimu Mkurugenzi
wa Mipango na Ufuatiliaji (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango).
Meneja
wa Uwanja wa ndege wa Mpanda, Mkoani Katavi Bw. Seneti Lyatuu (Kulia)
akifafanua jambo kwa Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo
kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kushoto).
Anayewasikiliza ni Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji (Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango), Bw. Omary Abdallah (Katikati).
Timu
ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
wakipata maelekezo ya uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda kutoka
kwa Meneja wa uwanja huo, Bw. Seneti Lyatuu (Kushoto).
Meneja
wa Uwanja wa ndege wa Mpanda, Mkoani Katavi Bw. Seneti Lyatuu (Kushoto)
akimuonesha kitu Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo
kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Wapili
kulia). Wanaoshuhudia ni wajumbe wa timu hiyo.
Sehemu ya Uwanja wa ndege wa Mpanda ikiwa imekamilika kwa kiwango cha lami.
Sehemu ya barabara ya kutua na kurukia ndege katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda.
PICHA ZOTE NA SAIDI MKABAKULI
No comments:
Post a Comment