Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eng. Ngosi Mwihava akizungumza
kabla ya kuanza kwa mnada wa kwanza wa madini yaliyokamatwa
yakisafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria.Wengine katika picha ni
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini
Tanzania (TMAA), Bruno Mteta (wa kwanza kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya
Ushauri wa Madini Tanzania, Richard Kasesera (wa pili kulia), Kamishna
Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Salim Salim (wa
tatu kushoto), Meneja Usafirishaji Madini wa TMAA, George Kaseza (wa
pili kushoto), na maafisa wengine kutoka TMAA, Eng. Charles Shamika (wa
nne kushoto) na Flora Kisena (wa kwanza kushoto).
Mkurugenzi
wa Fedha na Utawala kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA),
Bruno Mteta (wa nne kulia), akisoma moja ya zabuni (bid) ya ununuzi wa
madini yaliyokuwa yakipigwa mnada jijini Arusha. Wengine katika picha ni
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eng. Ngosi Mwihava (wa
tano kulia), Zabibu Napacho, Afisa Mfawidhi Ofisi ya TMAA-Arusha (wa
kwanza kulia), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari TMAA, Eng.Yisambi Shiwa
(wa pili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Madini Tanzania,
Richard Kasesera (wa tatu kulia), Kamishna Msaidizi wa Madini
anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Salim Salim (wa tatu kushoto),
Meneja Usafirishaji Madini wa TMAA, George Kaseza (wa pili kushoto), na
Eng. Charles Shamika (wa nne kushoto), Flora Kisena (wa kwanza kushoto)
kutoka TMAA.
wadau
mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi waliohudhuria Maonesho ya Tatu ya
Kimataifa ya Vito ya Arusha, wakishuhudia mnada wa kwanza wa madini
yaliyokamatwa yakisafirishwa nje ya nchi bila kuwa na vibali
husika.Aliyenyanyua karatasi ya maombi ya zabuni (bid) ya madini hayo ni
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala katika Wakala wa Ukaguzi wa Madini
Tanzania (TMAA), Bruno Mteta.
Meneja
Usafirishaji Madini kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA),
George Kaseza (katikati),akizungumza na waandishi wa habari mkoani
Arusha, mara baada ya kumalizika kwa mnada wa kwanza wa madini
yaliyokamatwa yakisafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria.
NaTeresia Mhagama
Madini
yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 yaliyokamatwa wakati
yakisafirishwa nje ya nchi bila kufuata taratibu za nchi za usafirishaji
madini yamepigwa mnada na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).
Madini
hayo yamepigwa mnada jijini Arusha katika Maonesho ya Tatu ya Kimataifa
ya Vito yaliyofanyika katika hoteli ya Mount Meru ambapo mnada huo wa
kwanza kufanyika nchini ulishuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati na Madini, Eng.Ngosi Mwihava, Mwenyekii wa Bodi ya Ushauri wa
Madini, Richard Kasesera, Makamishna Wasaidizi wa Madini nchini na
wananchi waliohudhuria maonesho hayo.
Meneja
Usafirishaji Madini wa TMAA, George Kaseza amesema kukamatwa kwa madini
husika ni matokeo ya juhudi za Serikali za kufanya kaguzi katika
viwanja vikubwa vya ndege vya Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro na
kueleza kuwa huo ni utekelezaji wa sheria ya madini ya mwaka 2010
inayoeleza kuwa usafirishaji madini kinyume na taratibu na kanuni
zilizowekwa ni kosa la jinai hivyo watoroshaji wa madini hayo
walikamatwa na kufikishwa katika Jeshi la Polisi.
"Udhibiti
hufanyika ili kuhakikisha kwamba madini yote yanasafirishwa kwa kufuata
taratibu, sheria na kanuni zinazosimamia biashara na uchimbaji
unaofanyika kwenye Sekta ya Madini.Moja ya taratibu hizo ni ulipaji wa
mrabaha kabla ya kusafirishwa nje ya nchi na kuwa na vibali maalum
ambavyo madini husika yanatakiwa kuambatana navyo kabla ya kusafirishwa
nje nchi", alisema Kaseza.
Alieleza
kuwa madini hayo yaliyopigwa mnada jijini Arusha yalikamatwa yakiwa
yanasafirishwa kinyume na taratibu ikiwemo kutokuwa na vibali vya
usafirishaji ama kutokuwa na vithibitisho vya ulipaji wa malipo ya
mrabaha.
"Adhabu
za waliokamatwa na madini haya zilishatolewa na Mahakama ambapo wengi
walishatumikia adhabu zao ikiwamo kifungo ama kulipa faini na madini
yao kutaifishwa na kuwa mali ya serikali, hivyo serikali imeamua kufanya
mnada wa kwanza kupitia maonesho haya ili kuhakikisha kwamba fedha
zinazopatikana katika mnada huo zinaingia katika mfuko wa Serikali na
kulinufaisha Taifa", alisema Kaseza.
Alieleza
kuwa upigaji mnada wa madini husika pia utapelekea watu kufuata sheria
zinazosimamia Sekta ya Madini na kusisitiza kuwa serikali haitasita
kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watoroshaji, wanaofanya biashara
haramu ya madini na kumiliki madini kinyume cha sheria.
Akifungua
mnada huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eng. Ngosi
Mwihava alieleza kuwa serikali inaendelea kuisimamia Sekta ya Madini
ipasavyo ili kuhakikisha kwamba madini yaliyopo Tanzania yanawanufaisha
watanzania na kusisitiza kuwa kupitia utaifishaji madini yanayotoroshwa,
serikali itakuwa ikipata fedha zitakazosaidia katika shughuli za
maendeleo.
Alieleza
kuwa minada husika itakuwa ikifanyika kwa uwazi na haki na kwamba
mshindi wa zabuni husika atakuwa ni yule aliyetimiza vigezo vilivyowekwa
ikiwemo kutokuwa chini ya bei iliyowekwa na serikali ambayo
imezingatia thamani ya madini husika.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Madini nchini, Richard Kasesera alisema
kuwa kufanyika kwa mnada huo kunaonesha jinsi serikali inavyotekeleza
kwa vitendo mpango wake wa kuwakamata wale wote wanaotaka kuvusha madini
nje ya nchi bila kufuata taratibu, kukwepa ushuru na kufanya biashara
ya madini bila vibali.
Alitoa
onyo kuwa hakutakuwa na msamaha kwa wale wote wanaokamatwa
wakisafirisha madini kinyume na taratibu na kwamba Serikali itaendelea
kukamata, kutaifisha na kupiga mnada madini hayo hivyo aliwataka wadau
wote katika Sekta ya Madini ndani na nje ya nchi kuhakikisha wanafuata
taratibu na sheria zinazosimamia sekta husika ili kujiepusha na kadhia
hiyo.
No comments:
Post a Comment