Na Anna Nkinda – Maelezo, New York
Ukosefu wa uelewa na imani potofu miongoni mwa wanajamii ni moja ya chanzo cha unyanyapaa kwa watoto wenye tatizo la usonji (Autism) .
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Mama Salma Kikwete wakati akiongea na Prof. Andy Shih ambaye ni Makamu wa Rais mwandamizi wa Mambo ya kisayansi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Autism Speaks yenye makao yake mjini New York.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema jamii
bado haina uelewa kuhusu tatizo la usonji kwani kuna baadhi ya watu
wanahusisha tatizo hilo na mambo ya ushirikina lakini kama jamii itakuwa
na uelewa tatizo la unyanyapaa litapungua au kwisha kabisa.
Alisema
usonji bado ni tatizo nchini Tanzania na nchi zingine lakini wazazi
wengi wanaona aibu kusema hadharani wana watoto wenye matatizo hayo na
hivyo kuwa vigumu kwa watoto hao kupata huduma muhimu ikiwemo elimu.
“Tunatakiwa
kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu waliobobea katika taaluma hii ili
kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa kuhusu tatizo hilo kwa kufanya
hivyo watoto hawa watapata huduma za muhimu kama elimu na afya”, alisema
Mama Kikwete.
Kwa upande wake Prof. Shih alisema
Taasisi yake iko tayari kufanya kazi na WAMA ili kuwasaidia watoto
wenye tatizo la usonji ili waweze kupata elimu na huduma ya afya kama
watoto wengine.
Prof.
Shih alisema tatizo la unyanyapaa bado ni kubwa kwa watoto lakini kama
jamii itapata elimu na kulifahamu tatizo hilo itaweza kuwasaidia watu
wenye matatizo hayo na hivyo kupunguza tatizo la unyanyapaa.
Usonji
ni hali ya udhaifu katika ukuaji wa ubongo ambayo huleta athari kubwa
katika mawasiliano, mahusiano ya kijamii na utambuzi.Tatizo hili ni la
dunia nzima na bado hakuna maelekezo kamili ya chanzo chake wala tiba.
Wanaoathirika
zaidi ni watoto wa kiume kuliko wa kike kwa uwiano wa nne kwa moja hii
ikiwa na maana kuwa kila watoto watano wenye usonji wanne ni wa kiume na
mmoja wa kike.
Mwaka
1997 wizara ya Elimu na Utamaduni ikishirikiana na wanachama wa
National Association for People with Autism in Tanzania (NAP-T)
walianzisha kitengo cha watoto wenye usonji katika shule ya msingi
Msimbazi Mseto ambacho ni kitengo mama cha kutoa huduma.
Hivi
sasa Serikali inavitengo vitano, viwili vipo Dar es Salaam, viwili
Arusha na kimoja Morogoro. Pia kuna vitengo kadhaa vilivyoendeshwa na
watu binafsi.
No comments:
Post a Comment