BAADA YA VIFO KENYA : WANANCHI WA MPEKETONI WALALA MSITUNI KUOKOA MAISHA YAO - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Wednesday, 18 June 2014

BAADA YA VIFO KENYA : WANANCHI WA MPEKETONI WALALA MSITUNI KUOKOA MAISHA YAO


Maporomoko
Wakazi wa kijiji cha Maporomoko wakiwa safarini Juni 17, 2014 Kaisari baada ya watu tisa kuuawa usiku katika kijiji hicho. Picha/LABAN WALLOGA 
Na KALUME KAZUNGU

MAUAJI ya zaidi ya watu 50 yaliyotekelezwa mnamo Jumapili usiku katika maeneo ya Mpeketoni, Kibaoni na Poromoko, sasa yamegeuza maboma mengi kuwa mahame.
Kufikia Jumanne jioni, familia nyingi hazikuwa majumbani huku wengi wa wakazi wakigeuza misitu kuwa ngome salama.
Mengi ya maboma yaliyotembelewa na Taifa Leo Jumanne jioni  yalikuwa pweke baada ya familia nyingi kugeuza mkondo wa maisha na kutafuta usalama misituni.
“Leo ni siku ya tatu. Mimi na familia yangu tumehama nyumbani na kutafuta makao msituni kila usiku. Tunarudi majumbani baada ya alfajiri. Tunaogopa kupatwa hapo na kushambuliwa kama wenzetu,” akasema mmoja wa wakazi wa Majembeni, Bw Johnson Kitsao Ndokolani.
Mjini Mpeketoni, hali ya taharuki ilizidi kughubika eneo hilo kwa siku ya tatu mfululizo huku makazi mengi yakiachwa bila wenyewe.
Biashara pia ziliendelea kufungwa kwa siku ya tatu mfululizo.
Watu pia walilazimika kuhama kutoka mjini humo kwa kuhofia mashambulizi.
Shule pia ziliendelea kufungwa kwa siku ya tatu mfululizo huku wazazi wakiendelea kuwazuia watoto wao wasihudhurie madarasa kwa hofu za kiusalama.
Katika shule ya Msingi ya Lake Kenyatta iliyoko mjini Mpeketoni, hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyefika shuleni kuendelea na masomo.
Wengi wa wanafunzi waliozungumza na wanahabari walionekana kutishika huku wakilalamika kwamba ikiwa hali itaendelea hivyo basi huenda wakafeli mitihani.
Njaa
“Nimempoteza mjomba wangu. Siwezi kufika shuleni. Naomboleza. Serikali ifanye hima na kutuhakikishia usalama wa kutosha. Tutakalo zaidi ni usalama na masomo yaweze kurudi kama kawaida. Twahofia tutaanguka mitihani ikiwa hali itaendelea hivi,” akasema Julius Njoroge ambaye ni mwanafunzi wa Lake Kenyatta.
Wakazi pia wanalalamikia njaa. Walisema vyakula havipatikani tena madukani tangu shambulizi la Jumapili uvamizi wa Jumapili usiku.
“Wenye maduka bado wanataharuki. Mashambani hakuendeki tena. Chakula ni tabu na tunahofia kwamba huenda tukafa kwa njaa,” akasema Catherine Mwasambu.
Hata hivyo usalama bado umeimarishwa katika maeneo husika kwani vikosi vya polisi bado vimekita kambi kushika doria misituni na katika maeneo ya miji iliyotekelezwa mauaji. Chanzo: Taifa Leo

No comments:

Post a Comment