Baraza
la usalama la umoja wa mataifa hatimaye limeidhinisha kuwekewa vikwazo
kundi la Boko Haram baada ya utekaji nyara wa takriban wasichana 300 wa
shule katika eneo la Chibok Nigeria.
Kundi hilo limeshutumiwa kuwaua maelfu ya watu nchini Nigeria katika miaka michache iliyopita.
Nigeria
ni mwanachama wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kwa kipindi cha
miaka miwili. Kwa nafasi hii imeweza kushinikiza baraza hilo kuimulikia
tochi.
Hatua
ya baraza hilo kuiorodhesha Boko Haram miongoni mwa magaidi wa
kimataifa, wakipishana au hata kuhusishwa moja kwa moja na AL Qaeda,
huenda isionekane kama hatua kubwa. Lakini hii ina maana kuwa sasa jamii
ya kimataifa italichukulia kwa uzito mkubwa zaidi kundi hilo.
Baraza
hilo limeidhinisha pia vikwazo kuwekewa kundi hilo, viongozi wake na
yeyote anayehusishwa nalo. Hii ina maana kuwa hata mali zao zitazuiliwa
na akaunti zao zote zinazojulikana kufungwa.
Mjumbe
wa Marekani katika Umoja wa mataifa Samantha Power amepongeza hatua
hiyo akisema kuwa itaimarisha vita vya serikali ya Nigeria dhidi ya
Kundi hilo, ambalo limetikisa jamii ya kimataifa mwezi uliopita kwa
kuwateka zaidi ya wasichana mia mbili wa shule.
Kwa
upande wake mjumbe wa Australia katika baraza hilo balozi Gary Quinlan
amesema kuwa wanao ushahidi wa kutosha kuwa Boko Haram wamepewa mafunzo
na kundi la Al Qaeda hasa namna ya kujitengenezea mabomu, mtindo ambao
umekuwa mbinu mpya zaidi ya ugaidi.
Kiongozi
wa Boko Haram Abubakar Shekau amenukuliwa katika mtandao akitoa
matamshi ya kuunga mkono AL Qaeda nchiuni Afghanistan, Yemen na Somalia.
Kabla
ya kujumuishwa Boko Haram katika orodha ya Al Qaeda, kulikuweko makundi
62 kote duniani waliowekewa vikwazo kuhusika na Ugaidi, na watu binafsi
162, ambao wamewekewa vikwazo vya usafiri na mali zao kutwaliwa.
Shughuli
za Boko Haram katika miaka 5 iliyopita zimesababisha vifo vya maelfu ya
waislamu na wakristu wakiwemo watu 1500 waliouawa mwaka huu pekee.
Jina
la Boko Haram lina maanisha masomo ya magharibi ni Haram na kundi hilo
limetumia nembo hiyo kuendeleza mashambulio yao na chuki dhidi ya
chochote kinachhusishwa na nchi za magharibi.CHANZO BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment