Msemaji
wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene
(kushoto) akizungumza na wahariri wa Gazeti la Jamhuri Bw. Deodatus
Balile, Muhariri Mtendaji (katikati) na Bw. Manyerere Jackton , Naibu
Muhariri Mtendaji (kulia) alipotembelea Ofisi za gazeti hilo mtaa wa
Samora jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa
watendaji wa Idara ya Habari kuvitembelea vyombo vya habari kwa lengo la
kuimarisha ushirikiano na kutatua changamoto zinazoikabili tasnia ya
Habari nchini.
Muhariri
Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri Bw. Deodatus Balile (kulia) akizungumza
jambo na viongozi wa Idara ya Habari waliotembelea ofisi za gazeti hilo jijini Dar es salaam. Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara
ya Habari-Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo,Afisa habari wa
Idara ya Habari Bi. Jovina Bujulu na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na
Msemaji wa Serikali Bw. Assah Mwambene.
Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya Habari-Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo
akifafanua utaratibu wa utoaji wa vitambulisho kwa waandishi wa habari
(Press Card) na namna Idara ya Habari inavyozingatia kigezo cha elimu
cha taaluma ya Habari katika kutoa vitambulisho kwa waandishi wa Habari
(Press Card) hapa nchini.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Vyombo
vya habari nchini vimeaswa kutoa kipaumbele kwa habari zinazojenga
jamii kwa kuihamasisha kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo,
kudumisha uzalendo na kuepuka habari zinazoweza kusababisha mgawanyiko
na chuki katika jamii.
Wito
huo umetolewa jijini Dar es salaam na Msemaji wa Serikali na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene alipotembelea ofisi za
gazeti la Jamhuri zilizoko mtaa wa Samora jijini Dar es salaam ikiwa
ni sehemu ya utaratibu wa Idara hiyo kuvitembelea vyombo mbalimbali vya
habari nchini kwa lengo la kukuza ushirikiano na kujadili changamoto
mbalimbali za tasnia ya habari hapa nchini.
Amesema
kuwa serikali inaheshimu mchango mkubwa unaotolewa na tasnia ya habari
hapa nchini na kuongeza kuwa habari ni moja ya sekta inayokuwa kwa
kasi, yenye uwekezaji mkubwa na inayoajiri watu wengi hapa nchini.
“Sisi
kama serikali ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tasnia ya habari hapa
nchini inapiga hatua kutokana na umuhimu wa pekee ilio nao katika
jamii,hivyo utaratibu huu wa kuvitembelea vyombo vya habari ni wa
kawaida ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya
kutatua changamoto mbalimbali zilizopo” .
Akizungumza
na wahariri wa gazeti hilo Bw. Mwambene amesema kuwa vyombo vya habari
hapa nchini vinao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa vinatoa kipaumbele
kwa habari zinazogusa masuala mbalimbali ya wananchi na kuibua
changamoto mbalimbali zilizo katika jamii kwa lengo la kuongeza ufanisi,
uwajibikaji na ustawi wa taifa.
Amelipongeza
gazeti hilo kwa kuendelea kuzingatia weledi katika utoaji wa habari
zake kwa kuweka msisitizo wa utoaji wa habari zinazohamasisha uzalendo.
“Kwanza
nawapongeza kwa kazi mnayoendelea kuifanya hasa moyo wa uzalendo
mliouonyesha mlipokuwa mkiandika habari na kuchapisha makala kuhusu
uhusiano wa Tanzania na nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo pia katika masuala mbalimbali yenye kuhamasisha uzalendo nchini”
Ameeleza
kuwa hivi sasa taifa la Tanzania liko katika mchakato wa masuala
makubwa yanayogusa maisha ya watu na maendeleo yao yakiwemo ya Uchaguzi
mkuu utakaofanyika mwaka ujao na zoezi linaloendelea la kupata katiba
mpya na kufafanua kuwa katika hilo vyombo vya habari vina wajibu wa
kuhamasisha umoja wa kitaifa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari – Usajili wa Magazeti
Bw. Raphael Hokororo amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa taaluma ya
habari inaendelea kulindwa hapa nchini na waandishi wa habari wanafanya
kazi zao bila vikwazo idara ya Habari imekuwa ikitoa vitambulisho vya
waandishi wa habari (Press Card) kwa waandishi wenye sifa na taaluma ya
habari.
Amesema
utoaji wa vitambulisho kwa waandishi wa habari umesaidia kudhibiti
uwepo wa waandishi wasio na sifa katika shughuli mbalimbali za serikali
ikiwemo mkutano wa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
“Katika
hili tumeweka msisitizo wa matumizi ya vitambulisho hivi na tumeanza na
Bunge maalum la Katiba waandishi wote wanaoandika habari za bunge la
katiba tumewapatia vitambulisho” Amesema Bw. Hokororo.
Kwa
upande wake Muhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri Bw. Deodatus Balile
amewapongeza viongozi hao wa Idara ya Habari wakiongozwa na Mkurugenzi
wa Idara hiyo Bw. Assah Mwambene kufuatia utaratibu huo wa kuvitembelea
vyombo vya habari na kuongeza kuwa unaongeza ushirikiano baina ya
vyombo vya habari na
serikali.
Kuhusu
mchakato wa kupata katiba mpya na uchaguzi mkuu ujao Bw. Balile
ameeleza kuwa gazeti la Jamhuri linaendelea kutoa kipaumbele kwa
habari zenye maslahi kwa taifa na pia habari za vyama vya siasa vyenye
kujenga hoja kwa wananchi.
Aidha
amesema kuwa wao kama chombo cha habari makini wataendelea kuihabarisha
jamii kwa kuzingatia maadili, uzalendo na kukemea vitendo viovu
vinavyorudisha nyuma maendeleo ya taifa.
No comments:
Post a Comment