Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.PICHA|MAKTABA |
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ameuliza maswali saba ya
msingi kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaopinga Rasimu ya Katiba
iliyotolewa na Tume yake akitaka wawajibu wananchi ili kutuliza kiu yao.
Jaji Warioba ambaye tangu awasilishe Rasimu ya
Katiba Desemba 30, mwaka jana amegeuka kuwa adui kwa watu wanaotaka
muundo wa serikali mbili, aliuliza maswali hayo jana katika uzinduzi wa
ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza kuhusu mchakato wa Katiba.
Akizungumza kwa ukali, Jaji Warioba alisema:
“Kwanza, jibuni kwa nini mnapinga muundo wa Muungano wakati
walioupendekeza ni wananchi?
“Sheria inasema uwepo wa Muungano na mapendekezo
katika rasimu hayasemi Muungano usiwepo. Kumbukeni kuwa wananchi
walitakiwa kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha Muungano.”
Katika swali lake la pili, Warioba alisema kwa
nini Tanganyika imevaa koti la Muungano? Kwa kuwa katika ukusanyaji wa
maoni wananchi walieleza kuwa Serikali ya Muungano ya sasa siyo ya
Muungano, ni ya Tanganyika.
Katika swali la tatu alisema wajumbe hao
wanatakiwa kujibu maelezo ya wananchi ambao waliieleza tume hiyo kuwa
Katiba imevunjwa na madaraka ya rais yamechukuliwa na sasa kuna marais
wawili katika nchi moja.
“Tume inapewa lawama kubwa, wajibuni wananchi hii
tume ilitumwa na nani kukusanya maoni ya wananchi? Waambieni ilikusanya
maoni hayo kwa kutumia sheria ipi zaidi ya ile ya Mabadiliko ya Katiba?”
alisema Jaji Warioba katika swali lake la nne.
Katika swali lake la tano, Warioba aliwataka
wajumbe hao kutoa sababu za kumtuhumu kuwa amependekeza muundo wa
serikali tatu kwa sababu yeye pamoja na (Joseph Butiku) walikuwa wajumbe
wa Tume ya Jaji Kisanga na Jaji Nyalali ambazo nazo zilipendekeza
muundo wa serikali tatu, kitu ambacho alisema si kweli na hawakuwahi
kuwa mjumbe wa tume hizo.
Pia, aliwataka wajumbe hao kujibu swali la sita,
kwa nini hawataki kuzungumzia yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na badala
yake wanageuza rasimu hiyo kuwa imeandikwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Katika swali lake la saba, aliwataka wajumbe
kujibu kwa nini wanaishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa imeingiza
maoni yake, wakati ilikusanya maoni hayo kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba?
Alisema badala ya kujadili hoja za msingi, wajumbe
wa Bunge hilo wamekuwa wakitoa lugha za kejeli na matusi kwa baadhi ya
watu (akiwamo na yeye), kitendo ambacho alisema si sahihi na kinaweza
kuligawa taifa kwa sababu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba yametokana na
maoni ya wananchi.
Katika uzinduzi huo walikuwepo baadhi ya wajumbe
wa Bunge hilo ambao ni Dk Hamisi Kigwangalla aliyemwakilisha Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana, Julius Mtatiro, Maria Sarungi na aliyekuwa
mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole.
Amshukia Lukuvi
Katika maelezo yake, Jaji Warioba alieleza
kushangazwa kwake na wajumbe kulitumia Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), kama mfano wa kuwashawishi Watanzania kukubaliana na matakwa yao
ya kutaka kupinga mfumo wa serikali tatu.
“Nchi hii imekuwa na matatizo ya rushwa na
ufisadi, lakini hakuna hata siku moja mtu amesema jeshi linaweza kushika
madaraka. Leo kwa sababu ya madaraka mnaingiza jeshi na mchakato wa
Katiba katika makundi.”
Licha ya kutomtaja mlengwa, kauli hiyo ilionekana
kumlenga Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge),
William Lukuvi ambaye Aprili 13, mwaka huu aliwataka wananchi kupinga
muundo wa serikali tatu, akisema la sivyo jeshi linaweza kuchukua
madaraka.
Akiwa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma
alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Lukuvi
alisema muundo huo ukipita, nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali
ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.
Kauli kama hiyo pia iliwahi kutolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.
“Msiliingize jeshi katika siasa za makundi na
inakuwa mbaya zaidi kama mkienda katika makanisa na kutoa kauli za namna
hii,” alisema Warioba na kuongeza:
“Umoja wetu, amani na utulivu kwa kiwango kikubwa
mhimili wake ni viongozi wa dini. Wamekuwa wakihubiri umoja, amani na
mshikamano, hivyo tusiingize siasa za makundi kwenye makanisa na
misikiti.”
Jaji Warioba aliwataka wajumbe wa Bunge hilo
kukumbuka wajibu wao wa kuwaunganisha wananchi na kuwataka waachane na
kauli za kejeli, kuudhi na matusi kwani zinaweza kuleta mgawanyiko na
mpasuko nchini.
“Nimekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu lakini
sijawahi kuona taasisi yenye uzalendo wa hali ya juu kama JWTZ,” alisema
Warioba.
Warioba ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, kuanzia mwaka 1985 hadi 1990, alisema:
“Katika ziara zangu mikoani nilikuwa nikikutana na wanajeshi na
kunieleza matatizo yao. Licha ya wakati huo serikali za mataifa mengine
zilikuwa zikipinduliwa na jeshi, hapa kwetu ilikuwa tofauti, walikuwa na
uzalendo wa hali ya juu licha ya kuwa hali yetu kiuchumi ilikuwa
mbaya,” alisema.
Alisema wakati huo wanajeshi walikuwa wakivaa sare zilizochakaa na viatu vilivyopasuka, lakini hawakufikiria kuipindua Serikali.
Alisema hata katika vita dhidi ya Uganda, wanajeshi wa Tanzania
walishinda kwa sababu ya uzalendo na siyo vifaa vya kisasa vya kivita...
“Inashangaza kuona watu wanatolea mfano mmoja tu wa kama wanajeshi
wasipolipwa; kwa nini wasiseme mawaziri au watumishi wa serikali
wasipolipwa?”
Alisema kauli hiyo ni sawa na kuwaeleza wananchi
kuwa jeshi ni baya na kama ikipita Katiba isiyoendana na matakwa ya
walio wengi jeshi litachukua nchi.
Alisema wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ikikusanya maoni ya wananchi, wanajeshi na viongozi wa vyombo vya ulinzi
na usalama nchini walijikita zaidi kutoa maoni ya kuimarishwa kwa
ulinzi na usalama na siyo mambo mengine.
“Tatizo ambalo walitueleza ni kuchoshwa na kitendo
cha kupiga mizinga 21 kwa Amri Jeshi Mkuu wakiwa Dar es Salaam na
wakiwa Zanzibar. Walisema kwa nidhamu ya jeshi, Amri Jeshi Mkuu ni mmoja
tu. Nadhani mngewaondolea kero hiyo na si mambo mengine,” alisisitiza.
Kigwangalla
Kwa upande wake, Dk Kigwangalla alisema kama
tatizo ni Muungano ni vyema suala hilo likarejeshwa upya kwa wananchi
ili watoe maoni yao kwa sababu mchakato huo sasa umehamia katika muundo
wa Muungano pekee.
“Mchakato huu si wa kuifufua Tanganyika na kuvunja
mkataba wa Muungano na siyo wa kubadili muundo wa utawala. Mambo haya
yalihitaji mchakato unaojitegemea,” alisema.
Alisema tume zote zilizotoa mapendekezo ya
Serikali tatu zilikuwa na asilimia ndogo ya watu waliounga mkono kama
ilivyo kwa Tume ya Jaji Warioba.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
No comments:
Post a Comment