Na Anna Nkinda- Maelezo, Lindi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewataka wazazi na walimu kushirikiana kwa pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanakwenda shule na kusoma jambo ambalo litasaidia kupanda kwa kiwango cha elimu mkoani humo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo hivi karibuni wakati akiongea na wananchi pamoja na wanafunzi wa kijiji cha Ruaha waliofika kumsalimia mara baada ya kumaliza mkutano wake na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi la Ruaha lililopo katika kata ya Mingoyo wilaya ya Lindi mjini.
Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu Taifa alisema kiwango cha elimu katika mkoa huo kiko chini lakini kama wazazi watahakikisha watoto wao wanaenda shule kwa wakati na walimu wakihakikisha watoto wamefika shule na kuwafundisha kiwango cha elimu kitapanda kwa kiasi kikubwa.
“Na ninyi watoto muache tabia ya kupoteza muda kwa kuokota mabibo au maembe tumieni muda huo kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yenu kwa kufanya hivyo mtakuwa na maisha mazuri hapo baadaye”, alisema Mama Kikwete.
Akiwa katika matawi la Mkwaya, Ruaha na Majengo Mama Kikwete aliwataka vijana wa CCM kuungana kwa pamoja na kutafuta eneo kubwa la kikundi ambalo watalitumia kulima kilimo cha mazao ya biashara kama vile ufuta ambao utawapatia fedha nyingi na hivyo kujikwamua kiuchumi.
Aidha Mama Kikwete pia aliwataka kinamama kwenda kupima saratani ya mlango wa kizazi ambayo inauwa wanake wengi lakini vifo vya ugonjwa huo vinazuilika kama mgonjwa atakwenda kupima mapema na akigundulika kuwa na dalili za ugonjwa huo katika hatua za awali ataweza kupata matibabu na kupona.
No comments:
Post a Comment