<<<<<<<<<<<>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>
Na
Saidi Mkabakuli
Katika kukabiliana na kasi ya maendeleo ya ukuaji wa
uwekezaji katika maeneo ya viwanda vikubwa na biashara za huduma mkoani Mtwara,
Serikali imesema kuwa kuna haja ya kuuimarisha Uwanja wa Ndege wa Mtwara ili
kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa watumiaji wa uwanja huo, hasa kufuatia
kugundulika kwa gesi mkoani humo,
Hayo
yamebainishwa mmoja wa viongozi wa timu ya ukaguzi wa
miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence
Mwanri wakati ilipofanya ziara kwa ajili
ya kujionea maendeleo ya uwanja wa huo.
Bibi
Mwanri alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini na mikakati
mbalimbali itakayopelekea kuuimarisha uwanja wa ndege wa Mtwara ili kuweza
kuhudumia uwekezaji mkubwa unaofanywa na makampuni mbali mbali ya ndani na nje
ya nchi mkoani humo. Aliongeza:
“Tathmini ya awali inaonesha kuwa miradi
mingi ipo mkoani Mtwara kufuatia kugundulika kwa gesi hivyo kuna haja ya dhati
ya kuuimarisha uwanja wa ndege wa Mtwara kwa lengo la kutoa huduma za uhakika
wakati huu wa mfumuko wa kiuchumi mkoani Mtwara,” alisema Bibi Mwanri.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Naibu Katibu Mtendaji
(Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara ambaye alikuwa
kiongozi mwenza wa ukaguzi, alisema kuwa kuna haja ya dhati ya kuwekeza katika
uwanja huo ili kukabiliana na kasi ya maendeleo ya mkoa wa Mtwara kufuatia wawekezaji
wengi kuendelea kumiminika na kuwekeza mkoani humo.
“Uwanja wa ndege wa Mtwara una fursa za
nyingi za kuhudumia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, hakika ni lango la
biashara hasa kipindi hiki cha uchumi wa gesi mkoani Mtwara, hivyo uendelezaji
wa uwanja huu ni jambo lisilo epukika,” alisema Prof. Rutasitara.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16),
Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa uwekezaji mkubwa katika
miundombinu ya nishati, usafirishaji (bandari, reli, barabara na usafiri wa
anga), maji (safi, taka na ya uzalishaji) na TEHAMA.
Serikali imeandaa Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Lengo kuu la Mpango huu ni kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka
misingi ya ukuaji mpana wa uchumi na unaolenga watu walio masikini zaidi.
Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja wa
mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa utekelezaji na
kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya
maendeleo kitaifa.
Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa
kati ifikapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment