Deogratius Chami, mlemavu wa viungo aliyejikubali na kutafuta elimu licha ya unyanyapaa aliokutana nao hatimaye amehitimu shahada.Picha na Rehema Matowo. |
Suala la elimu kwa walemavu limekuwa likipuuzwa na wazazi, jamii na Serikali kwa ujumla
Zipo baadhi ya familia ambazo zinaamini ulemavu ni
laana ama mkosi, jambo linalosababisha mtoto anayezaliwa na ulemavu
kuishi maisha ya kificho na wakati mwingine huuawa, wakiamini kuwa kuzaa
mlemavu ni laana kwenye familia.
Hata hivyo, kuna familia zinazojenga uthubutu na
kuionyesha jamii kuwa ulemavu sio laana wala mkosi; kwamba watoto wao
walio na ulemavu huwasaidia kupata elimu na mahitaji mengine muhimu.
Nimekutana na mlemavu wa viungo ambaye anatembea na kiti cha magurudumu, miguu yake yote miwili haina uwezo wa kutembea.
Mlemavu huyu ni mhitimu wa Chuo Kikuu Kishiriki
cha Ushirika na Biashara Moshi; amepata Shahada ya Maendeleo ya Jamii na
anaamini ulemavu alionao siyo kasoro bali ni uwezo wa Mungu kuonyesha
karama zake.
Deogratius Chami (29), ni mlemavu ambaye katika
ulemavu huo ameyaona mengi ikiwa ni pamoja na kunyanyapaliwa kila
anapofika katika baadhi ya ofisi za Serikali au kuzungumza na mtu kwa
lengo la kutaka kusaidiwa kielimu .
Chami anasema hakuzaliwa akiwa mlemavu, bali
alipata ulemavu akiwa darasa la tano mwaka 1997;ulemavu wake
ulisababishwa na kuporomoka kwenye udongo maeneo ya Kibosho wilaya ya
Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Anasema ajali hiyo ilimfanya alazwe hospitali ya
rufaa ya KCMC kwa miaka miwili na baadaye alipata msamaria aliyempeleka
kwenye Kituo cha Moshi Chaple, akaishi hapo ili aweze kupata elimu kwa
kuwa ndio kitu pekee alichokuwa akitamani kwa wakati huo.
Anasema akiwa mtoto wa sita kati ya watoto 11 wa
familia yao ,asingeweza kuendelea na masomo kutokana na hali ya ulemavu
aliyokuwa nayo huku familia yao ikiwa ni ya kipato cha chini ikitegemea
kilimo cha kawaida kilichokuwa kikiwasaidia kupata mlo tu.
Anasema ufadhili alioupata wa kuishi Moshi Chaple
ulimsaidia kurudi darasani ambako mwaka 1999 ilimlazimu kurudia darasa
la tano katika Shule ya Msingi Kilimanjaro na kwa uweza wa Mungu
alifaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari Old Moshi hadi mwaka 2005.
Anasema kutokana na ulemavu aliokuwa nao alikuwa akikaa kwenye kiti cha
magurudumu muda wote hali iliyomsababishia vidonda vilivyosababishwa na
kukaa kwa muda mrefu hivyo kumfanya ashindwe kuingia darasani.
Hali hiyo ilimfanya afanye vibaya darasani, walimu
wake walijaribu kumshauri kurudia darasa lakini yeye alipinga na kuamua
kufanya mtihani wa kidato cha nne na kwa bahati mbaya matokeo hayakuwa
mazuri hivyo akashindwa kuendelea na kidato cha tano.
Siku zote wahenga wanasema penye nia pana njia na
ndio msemo aliousema Chami. Anasema baada ya kutafakari sana aliamua
kurudi darasani na kurudia mtihani mwaka 2006 akiwa kama mwanafunzi wa
kujitegemea na kufanikiwa kufaulu na kujiunga na kidato cha tano mwaka
2007 katika Shule ya Sekondari Majengo.
Matokeo ya kidato cha sita yalikuwa mazuri ambayo yangemuwezesha
kuendelea na elimu ya juu lakini kutokana na umaskini wa kipato na
familia kutokuwa na uwezo alishindwa kuingia darasani kama wanafunzi
wengine jambo ambalo lilimuumiza sana.
Anasema alihangaika kuingia kwenye mashirika
binafsi na kwenye ofisi za Serikali lakini hakufanikiwa hata kujieleza
kwa kuwa kila anapofika kabla hata ya salamu hujibiwa ‘leo hatuna njoo
kesho ‘wakimuona yeye ni ombaomba.
Anasema jambo hilo lilikua likimuumiza sana kutokana na ukweli kwamba hakuwa ombaomba kama walivyofikiri.
Anasema nenda rudi kwenye ofisi hizo ndio ulikuwa
mlango wake wa mafanikio kwani kutokana na yeye kutokata tamaa ya kwenda
na kurudi kesho yake ndio ilimgusa mfanyakazi mmoja wa ofisi ya mkuu wa
wilaya aliyemtaja kwa jina moja la Koshuma aliyetaka kujua tatizo la
yeye kufika katika ofisi hizo kila siku.
Anasema Koshuma alimsikiliza kama mtoto
anavyozungumza na baba yake na kuahidi kumsaidia na ndipo mlango wa
mafanikio ya kusonga mbele ulipofunguka.
Anasema Koshuma alimkutanisha na Peter Kisumo mzee
ambaye kwake amekuwa kama daraja la kusonga mbele kwa kuwa alimkubali
kama mtoto na kumwahidi kumsaidia kwa kadri ya uwezo wake.
Ndipo alipomtafutia mfadhili aliyemtaja kwa jina
la Atul ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mount Meru ambaye alikubali
kumsomesha kwa kipindi cha miaka mitatu akiwa Chuo Kikuu Ushirika.
“Kwa kweli nawashukuru sana wote walionisaidia, hasa Atul na Kisumo, Mungu awabariki sana,” anasema.
Anaushukuru pia uongozi wa chuo kwa kumsaidia kusoma vizuri kwani walihakikisha hakuna mwanafunzi anayemnyanyapaa. Chanzo MWANANCHI
No comments:
Post a Comment