Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikagua mahema yaliyowahifadhi wahanga wa
Mafuriko katika kijiji cha Magole,mkoani Morogoro wakati alipotembelea
maeneo yaliathiriwa na mafuriko na kuwapa pole wananchi.
Eneo la Dumila, Morogoro lilikumbwa na mafuriko
makubwa na kusababisha wakazi wake kupoteza makazi na mali huku mamia ya
magari yakiwamo mabasi yanayosafirisha abiria kukwama baada ya kubomoka
kwa Daraja la Magole linalounganisha Barabara ya Dar es Salaam na
Dodoma.
Mvua hizo zilizonyesha kwenye Wilaya ya Kilosa, ndizo zilisababisha kufurika kwa Mto Mkundi unaopita kwenye eneo hilo.
Taarifa ya Bendera
Bendera alitoa taarifa ya mafuriko kwa Rais
Kikwete kwa niaba ya viongozi wa mkoa, wakiwamo wakuu wa wilaya,
wakurugenzi na wakuu wa taasisi mbalimbali akisema wananchi 12,472
wamepoteza makazi. Alisema pia kuwa nyumba 1,141 zilibomoka na 2,551
ziliingiliwa na maji huku kaya 2,759 zikiathiriwa na mafuriko. Bendera
alisema misaada ya mahema na vyakula imeanza kutolewa pamoja na dawa za
kukabiliana milipuko ya magonjwa endapo itatokea.
Alisema pia kuwa tayari baadhi ya miundombinu
imeanza kurejea kama kawaida huku huduma za majisafi zikitolewa na
magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha
Zimamoto Morogoro na Kampuni ya China ya High Quality Consulting and
Development Solutions. Bendera alisema pia kuwa jumla ya Sh53.7milioni
zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya muda ya waathirika hao.
JK aikataa taarifa
Rais Kikwete aliyekuwa akikatizakatiza taarifa
hiyo ya Bendera kwa maswali na ufafanuzi, alizikataa takwimu hizo
akisema hazionyeshi uhalisia. Akizungumza na wananchi wa eneo hilo
wakiwamo waliokuwa kwenye kambi iliyoko Sekondari ya Magole, Rais
Kikwete aliwahakikishia upatikanaji wa vyakula, dawa na majisafi na
salama.
Pia aliviagiza viwanda vya magodoro kuzisaidia
haraka iwezekanavyo, familia zilizoathirika na kuahidi kuwa Serikali
italipa baadaye ili kuwaepusha wakazi hao na hasa watoto na athari za
kiafya.
Alisema kazi ya ujenzi wa makazi ya muda itafanywa
JWTZ na si makandarasi kuepusha baadhi ya viongozi kujinufaisha kwa
mafuriko hayo. Rais Kikwete aliwataka Wakala wa Barabara Tanzania
(Tanroads), kuangalia uwezekano wa kutoa magogo yaliyoziba katika
makaravati na kuzibua mifereji ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi.
Akizungumzia ripoti hiyo Rais Kikwete alisema:
“Mmeshindwa kufafanua watu walioathiriwa na mafuriko hayo ni wangapi na
wanasaidiwa vipi hasa katika mahitaji mbalimbali na muhimu ya kimsingi
kama chakula.
“Taarifa yenu inanitia shaka. Sasa ninawataka
viongozi wa mkoa pamoja na Mkuu wa Mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi
wote wa halmashauri kurudia upya kumbukumbu zenu na kupata idadi kamili
ya waathirika ili kujua namna ya kuwasaidia. “Ninyi kama viongozi na
mnashughulikia maisha ya watu, mnatakiwa kuwa na kumbukumbu zenye
usahihi wa majina na kama hamna uhakika wa majina mnaomba vyakula kwa
ajili ya nani? Misaada mingine kwa wahisani ya nini?
“Tunataka tujue wanasaidiwaje, kina mama ni wangapi na kina
baba, watoto, tutoe misaada kadri inavyostahiki. Sasa kwa takwimu hizi
mnafahamu hawa watu wako wapi? Tutawasaidiaje? Wameathirika kwa kiasi
gani?.” Rais Kikwete alisema kiongozi mzuri hupimwa wakati wa kipindi
cha matukio na matatizo au majanga yanapotokea. Aliwataka viongozi hao
kujipanga kwa kuwatambua watu walioathiriwa na mafuriko kwa kuwa na
majina sahihi na idadi yao.
Miundombinu
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Injinia
Doroth Mtenga alisema ofisi yake itatumia kiasi cha Sh400 milioni
kukamilisha matengenezo ya eneo la tuta la Daraja la Magole katika Mto
Mkundi lililozolewa na maji na kusababisha mafuriko makubwa.
Fedha hizo zitatumika kurekebishia makaravati na
madaraja mengine madogo katika eneo hilo kutoka Wami Dakawa hadi Daraja
la Mkundi, Magole ambayo huathiriwa mara kwa mara pindi mto huo
unapojaa. Mtenga alisema kuwa ujenzi huo unakusudiwa kukamilika ndani ya
wiki ya kwanza ya Februari na kama hali ya hewa itaendelea kuwa nzuri,
ukarabati huo unatarajiwa kuendelea na kukamilika taratibu na magari
yataweza kupishana kama ilivyokuwa awali.
Wakati hayo yakifanyika, mafundi wa Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco), wameanza kazi ya kurudishia nguzo na nyaya za
umeme zilizoharibiwa na mafuriko hayo huku wataalamu wa Kampuni ya
Matrac Telecom, wakirekebisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenda Mkoa
wa Dodoma ambao pia uliharibiwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD),
Cosmas Mwaifwani amekabidhi kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro vifaa tiba,
magodoro 100 na dawa mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh80 milioni. Chanzo: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment