KANJANJA WA MJENGONI : KAULI YA TIDO MHANDO DHIDI YA JUMA NKAMIA - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Monday, 18 November 2013

KANJANJA WA MJENGONI : KAULI YA TIDO MHANDO DHIDI YA JUMA NKAMIA


BARAZA la Habari Tanzania (MCT) limemshukia Mbunge wa Kondoa Kusini Juma Nkamia, kwa kile ilichodai kuwa ametoa kauli ya kulikashifu baraza hilo bungeni, ilhali ni miongoni mwa wa watu waliofaidi matunda ya baraza hilo. Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuhusu kauli hiyo ya Nkamia aliyoiita kuwa ni ya dharau kwa baraza hilo, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema kauli ya mbunge huyo pamoja na kusikitisha inashangaza kwa kuwa Nkamia anajua fika kazi za baraza hilo na kunufaika na matunda yake. Alisema wakati mbunge huyo akichangia bungeni hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, alisema MCT na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ni sawa na asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) lakini zimekuwa zikijipa kazi ya kusimamia waandishi wa habari nchini. Alisema matamshi hayo pamoja na kusikitisha yameonesha dharau kwa chombo hicho, ambacho kimekuwa kikifanya kazi kubwa nchini na kuheshimiwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa nchi ambao wamekuwa wakifikisha malalamiko yao kwenye baraza hilo na kufanyiwa kazi. “Si busara kwa mbunge huyu ambaye pamoja na nafasi aliyonayo ya ubunge lakini pia taaluma yake ni ya uandishi wa habari, kutumia Bunge na kanuni za chombo hicho, kushambulia Baraza hili lenye wanachama wa kitaasisi takribani 131. Hii ni dharau isiyokubalika kwa wanahabari na wapenda demokrasia,” alisema Mukajanga. Alisema pamoja na matamshi hayo kuonesha dharau kwa MCT, lakini pia yameshangaza wanahabari kutokana na ukweli kuwa Nkamia, wakati alipokuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Maendeleo ya Jamii alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na baraza hilo hasa katika masuala ya Sheria ya Haki ya Kupata Habari. Alisema mbunge huyo akiwa kiongozi wa msafara pamoja na wabunge wenzake kadhaa waliwahi kupelekwa nchini India na MCT, kwa ajili ya kwenda kujifunza namna Sheria hiyo ya Haki ya Kupata Habari na Uhuru wa Vyombo vya Habari inavyofanya kazi. “Mimi nashangaa wakati wa maandalizi ya safari ile, Nkamia alikuja hapa MCT na kuzungumza na waandishi wa habari na alisifia sana kazi za Baraza hili na aliporejea aliitisha mkutano pale uwanja wa ndege na alisifia sana safari hiyo na walichojifunza huko India, sasa iweje leo aongee kinyume?” Alihoji. Mukajanga aliendelea kusema, “Baraza linatafsiri matamshi haya kuwa ni ya nia mbaya kwa ustawi wa Baraza hili huru Afrika Mashariki na Kusini Mwa Afrika, na ni kama makusudi ya kuwatishia na kupunguza nguvu za viongozi wake na kuleta hali ya kutoelewana kati ya wanachama wake kwa nia ya kulisambaratisha.” Alisema tangu kuanzishwa kwa MCT Juni 30, 1995 limefanya mambo mengi ikiwemo kusimamia maadili ya waandishi wa habari, limekuwa likiandaa mitaala ya kufundishia waandishi wa habari ambayo imepitishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na kusuluhisha migogoro mbalimbali inayohusu tasnia ya habari. “Baraza halitakubali kamwe kazi nzuri iliyofanywa miongo miwili ikanyagwe na kupuuzwa, viongozi wakuu wa Serikali na wanasiasa kama vile marehemu Dk Omar Ali Juma, Edward Lowassa na Frederick Sumaye wamefaidika na usuluhishi na kuheshimu Baraza hili,” alisema. Hivi karibuni Mbunge huyo wakati akichangia makadirio ya matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2013/2014, alisema MCT pamoja na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ni sawa na asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) lakini cha kushangaza zinafanyakazi kwa maslahi binafsi huku zikijipa mamlaka ya kusimamia waandishi wa habari nchini. Source: HABARI LEO

No comments:

Post a Comment