Mlipuko unaodhaniwa kutokana na bomu la kurushwa kwa mkono umetokea katikati ya ibada katika kanisa katoliki la Mt Joseph lililopo Olasiti Jijini Arusha ambako kwa siku ya leo kulikuwa na ibada ya Kuzindua Parokia ya Mt Joseph Olasiti.
Mlipuko huo unaelezwa kutokea majira ya katikati ya saa nne na saa tano asubuhi wakati Askofu wa Kanisa hilo akiendelea na ibada. Ibada hiyo sambamba na uzinduzi husika imeahirishwa hadi wakati mwingine.
Balozi wa Papa na ujumbe wake walikuwa miongoni mwa wageni muhimu katika tukio hilo la uzinduzi. Balozi huyo Mhashamu Askofu Franscisco Padilla alikuwa Arusha toka alhamisi ya Mei 2, 2013 na alipatiwa ulinzi wa kutosha na Jeshi la Polisi.
Haijaweza kuthibitika hasa sababu za wahusika kurusha “bomu” lakini mmoja wa washukiwa tayari ametiwa nguvuni na Polisi.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa takribani watu watatu wamefariki na zaidi 66 kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali ya Mt Meru kwa matibabu.
Viongozi mbalimbali wa kijamii na kiserikali wameweza kufika eneo la tukio, miongoni mwao akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, Meya wa Manispaa ya Arusha, Gaudence Lyimo, na Mbunge wa Arusha Mjini Mh Gobless Lema.
Wengine ni Mbunge wa Arumeru Mashariki, mh. Joshua Nassari, Diwani Msofe wa Kata ya daraja Mbili (CHADEMA), diwani wa Kata ya Olasiti na viongozi wengine wa Jeshi la Polisi na usalama Mkoa na Wilaya.
Jengo la kanisa halijadhurika lakini taharuki miongoni mwa watumiaji wa jengo hilo wakiwemo waumini wa kaisa hilo ni kubwa.
Chanzo cha mlipuko huo inasemekana kuwa kuna gari ndogo ilifika kanisani hapo na kusimama. Baadae alishuka mtu aliyekuwa amevalia vazi mithili ya kanzu na kurusha kitu kuelekea kanisani ambacho ndicho kilichosababisha mlipuko huo..
Lema hospitaliniMbunge wa Arusha mjini Godbless Lema akiwa na mbunge wa Arumeru Joshua Nassari wametoa damu kwa ajili ya majeruhi walioumia katika mlipuko huo.
Lema amewahimiza wakazi wa Arusha na vijana kujitolea kwa wingi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya majeruhi. Watu wengi wameitikia wito na wanaendelea kujitolea kuchangia damu kama ishara ya kumuunga mkono mbunge wao.
Picha kwa hisani ya Arusha 255 Blog |
No comments:
Post a Comment