Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza wanahabari
,wadau wa habari na Tasnia nzima ya habari nchini kwa kuadhimisha Miaka
20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani (World Press Freedom Day) leo,
Ijumaa, Mei 3, akiwahakikishia kuwa Serikali yake itaendelea kukuza,
kulea, kulinda na kutetea Uhuru wa Habari ulioshamiri kwa kiwango cha
juu kabisa nchini kwa sasa.
Aidha, Rais Kikwete
amesisitiza kuwa Serikali yake na yeye binafsi, kama mdau wa habari,
wataendeleza kuelekeza nguvu kubwa katika kupanua Uhuru wa Habari kwa
sababu uhuru huo ni kigezo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii
ya Tanzania na katika kujenga na kupanua demokrasia nchini.
Katika salamu zake kwa
wanahabari, wadau wa habari na Tasnia nzima ya habari nchini ambayo
inasherehekea Miaka 20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Dunia kitaifa mjini
Arusha leo katika shughuli zilizoandaliwa na Taasisi ya Habari Kusini
mwa Afrika (MISA), Tawi la Tanzania, Rais Kikwete amesema:
“Kama muumini na mdau wa
Uhuru wa Habari ambao ni sehemu ya Uhuru Mpana Zaidi wa Kutoa Maoni
(Freedom of Expression), napenda kuwapongezeni wanahabari wote nchini na
wadau wenzenu duniani katika kusherehekea siku hii ya kuadhimisha Miaka
20 ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani ambayo kitaifa hapa kwetu
inaadhimishwa na shughuli zilizoandaliwa na MISA-Tan mjini Arusha.”
Ameongeza Mheshimiwa Rais:
“Sisi katika Tanzania tunayo kila sababu ya kusheherekea Siku hii ya leo
ya Uhuru wa Habari nchini kwa sababu sote ni wadau wa habari ni
mashahidi wa mafanikio makubwa na mengi katika nyanja ya habari katika
miaka 20 iliyopita katika nchi yetu. Kwa sababu hiyo, naungana nanyi
katika kusheherekea na kuadhimisha mafanikio haya makubwa.”
Siku ya Uhuru wa Habari
Duniani ambayo chimbuko lake ni Mkutano wa Waandishi wa Habari wa Afrika
waliokutana na kutoa Tamko la Windhoek (Namibia) – the Windhoek
Declaration on Promoting an Independent and Pluralistic African Press
pamoja na kuanzisha Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika – Media
institute of Southern Africa (MISA), Mei 3, mwaka 1991, ilichaguliwa na
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa Siku ya Uhuru Duniani mwaka 1993.
Amesisitiza Rais Kikwete: “Napenda kutumia Siku hii ya leo
kuwapongezeni tena kwa kazi yenu nzuri ambayo imeendelea kuchangia
maendeleo ya nchi yetu kupitia njia ya kuhabarisha, kuelimisha na
kuburudisha wananchi. Vile vile, napenda kutumia nafasi ya Siku ya leo
kuwaelezeeni utayari wa Serikali yetu kuendelea kuithamini kazi hii
nzuri. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuifanya kazi yenu kwa
kuongozwa na misingi mikuu ya weledi wa taaluma ya uandishi wa habari.”
Ameongeza Rais Kikwete:
“Aidha, kama ambavyo tumekuwa tukifanya, napenda kuwahakikishieni kuwa
mimi binafsi na Serikali ninayoingoza nitaendelea kushirikiana nanyi
katika kupanua, kulea, kulinda na kutetea Uhuru wa Habari nchini ikiwa
ni haki ya waandishi kufanya kazi yao kwa mazingira mwafaka ya kisiasa,
kiuchumi, kisheria na kijamii. Vile vile, napenda kuwahakikisheni
tutaendelea kushirikiana nanyi katika kulinda uhuru wa wapata habari
nchini ambao ni muhimu kama ulivyo uhuru wa vyombo vya habari.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
03 Mei, 2013
No comments:
Post a Comment