Jumla ya nchi kumi katika eneo
la Maziwa makuu zimekubaliana kuunda jeshi la pamoja litakalokuwa na
jumla ya askari 4,000 katika kukabiliana na ghasia na vita vya mara kwa
mara mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Waziri wa Ulinzi wa DR Congo, Dakta Crispus
Kiyonga amethibitisha uundwaji wa jeshi hilo, akisema litafanya kazi
chini ya usimamizi wa Tanzania.
Mapigano ya hivi sasa mashariki mwa
Congo yalizuka mwezi Aprili mwaka huu wakati waasi wa M23 walipoliasi
jeshi la nchi hiyo na kusababisha watu laki tano kuyakimbia makaazi yao
wakihofia usalama wao.
Wakati huohuo, viongozi wa nchi wanachama wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika, SADC, wameanza
mkutano wao wa dharura jijini Dar es salaam nchini Tanzania.
Wameanza kwa kufanya kikao cha Asasi ya Ulinzi,
Siasa na Usalama ya SADC inayojulikana kama TROIKA chini ya Mwenyekiti
wake Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, kikao hicho cha
TROIKA kimewakutanisha marais Jakaya Kikwete, Hifikepunye Phohamba wa
Namibia na Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
Amesema mara baada ya kikao hicho cha TROIKA
viongozi hao watajumuika na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye pia ni
mwenyekiti wa mkutano wa kimataifa wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu,
pamoja na Rais Armando Guebuza wa Msumbiji ambaye ni Mwenyekiti wa sasa
SADC.
Viongozi hao kwa pamoja watajadiliana kwa kina
matatizo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na Zimbabwe
ambapo watawasilisha mapendekezo yao katika mkutano mkuu wa viongozi
wote 14 wa SADC utakaofanyika kesho. Na BBC Swahili
No comments:
Post a Comment