Dk Asha -Rose Migiro
Hakika
kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa
jingine. Ingawa huenda ni mapema sana
kwangu kutoa tafakuri kamili ya muhula wangu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa, hapana shaka kabisa kuwa nafasi hiyo imenipa uzoefu
maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa kunipa fursa hii, kuniamini na kwa ushirikiano
mkubwa wakati wote wa utumishi wangu.
Kukitumikia chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu
mfululizo ni heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi kama kilele kimojawapo cha maisha yangu ya utumishi wa umma.
Kila siku niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma
mbele mipaka ya ujuzi na elimu. Nimepata
kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika lenyewe; kuhusu dunia na watu wake, lakini pia
kufahamu ukomo wa uwezo wa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia changamoto
mbali mbali zinazoikabili dunia yetu.
Utumishi
wangu katika Umoja wa mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa uzoefu wa pekee.
Kazi hii imeujaza moyo wangu na unyenyekevu wa dhati kwani niliingia Umoja wa
Mataifa wakati ambapo dunia
inachagizwa na madhila
makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa kupindukia, kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na
udhalilishaji kwa wanawake na watoto; na
changamoto nyingine nyingi. Kwa muktadha huu ilikuwa fursa ya pekee kuchangia
juhudi za pamoja za kuimarisha Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake
katika kipindi cha mazingira magumu ya
kimataifa yaliyojaa changamoto za kipekee kabisa.
Daima
nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Mhe. Rais Jakaya Mrisho
Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo na kunienzi katika
kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa. Familia yangu, ndugu na marafiki
walikuwa karibu nami kwa dua na kunitia nguvu wakati wote wa utumishi wangu. Nawashukuru sana.
Hapana
shaka kazi yangu katika Umoja wa Mataifa
imeniwezesha kufahamiana kwa karibu na
viongozi wengi wa kimataifa na pia watu
mbali mbali waliopata mafanikio makubwa duniani. Nimeweza kufahamu kwa undani thamani ya
michango yao katika kujenga amani na ustawi wa dunia.
Zaidi
ya yote, sitasahau hisia nilizopata kila nilipokutana na watu wanyonge
waliokuwa wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa. Nitakumbuka daima tabasamu ya mwanamke mmoja
niliyekutana naye katika moja ya ziara zangu barani Afrika nilipotembelea
zahanati mojawapo kati ya kadhaa zinazofadhiliwa na Umoja wa Mataifa. Mama huyo mwenye watoto sita, alikuwa
amekikumbatia kitoto chake kimoja kilichokuwa nyonde nyonde; lakini alikuwa na tabasamu
iliyojaa faraja na matumaini kwa kuwa alikuwa amefanikiwa kupata bure dawa za
kunusuru maisha ya mwanawe.
Maendeleo
Nafasi
ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliasisiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi wa
utendaji wa Sekretariati na kuimarisha
uongozi wa Umoja Mataifa katika medani za uchumi na maendeleo ya
jamii. Majukumu ya Naibu Katibu Mkuu
yaliongezeka kadri Shirika lilivyokuwa linapanua shughuli zake. Hatimaye Naibu
Katibu Mkuu akakabidhiwa jukumu la kuoanisha na kuratibu idara zote zilizo
chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa. Jukumu hili lilikuwa na manufaa makubwa,
hususan tulipoingia katika utekelezaji wa dhana ya “Huduma ya Pamoja ” (Delivering
as One - DaO) ili kuleta ufanisi zaidi
katika kazi zetu hususan za maendeleo.
Kwa
bahati nzuri, ninamaliza kipindi changu kukiwa na maendeleo mazuri yanayotokana
na jitihada za kimataifa za kupambana na umaskini. Takwimu za kuaminika za hivi
karibuni zinatuambia kuwa juhudi zetu za kupunguza idadi ya watu maskini
duniani kufikia angalau nusu ya viwango vya sasa zimeanza kuzaa matunda.
Taarifa hii ni ya kutia moyo licha ya ukweli kwamba dunia inapitia dhahama
kubwa ya kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni.
Pamoja na majukumu mengine,nguvu zetu tulizielekeza zaidi kwenye kufanikisha
malengo ya maendeleo ya milenia na malengo mengine ya maendeleo yaliyokubaliwa
kimataifa. Nilihamasika sana na dhamira waliyoionesha wadau na washirika wetu
wa maendeleo: serikali, mashirika ya kiraia na mashirika ya biashara. Kwani
wote kwa pamoja waliyatumia malengo hayo kama
kilingo cha msingi katika kutokomeza umaskini.
Katika
kufanikisha utekelezaji madhubuti wa malengo ya maendeleo ya milenia nilipewa
jukumu la kukamilisha ahadi ya Katibu Mkuu aliyoitoa kwa nchi wanachama ya
kuunda Mfumo Kamilifu wa Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs Integrated Implementation Framework ).
Ninaona fahari kwamba naondoka Umoja wa Mataifa mfumo huu ukiwa umekamilika
ambapo Katibu Mkuu aliuzindua mwezi Juni mwaka huu. Kwa mara ya kwanza mfumo
huu umeweka utaratibu ambao utauwezesha Umoja wa Mataifa na wadau wote
kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa ahadi za kisera na kifedha. Hapana shaka utaratibu huu utaongeza
uwajibikaji wa wadau na upimaji sahihi wa hatua za maendeleo.
Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) Barani Afrika
Kwa mwelekeo huo huo, Katibu Mkuu
alizindua Jopo la Viongozi la Kuhimiza Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya
Milenia Barani Afrika (MDG Africa
Steering Group) mwezi September 2007. Kikundi hiki kinajumuisha taasisi
zote kuu duniani zilizo mstari wa mbele katika kuchochea kasi ya maendeleo ya
Afrika. Nilipata bahati ya kukiongoza
kikosi-kazi (MDG Africa Working Group) kilichokuwa
mhimili wa Jopo hilo la viongozi. Baada ya
miaka mitano ya majadiliano ya kina, Jopo hilo likiongozwa na Katibu
Mkuu limetoa mapendekezo kamambe ya
utekelezaji. Endapo mapendekezo haya yatazingatiwa basi yatakuwa nyenzo muhimu ya kuweka sera na
mikakati madhubuti itakayosaidia maendeleo katika nchi husika na duniani kwa
ujumla. Napenda kutoa mwito kwa wadau wote kuyapa umuhimu mapendekezo haya.
Ninafahamu kwamba tathmini kamili ya mafanikio ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia imepangwa
kufanyika Septemba mwaka 2013. Hata hivyo tayari tunaweza kusema kuwa Malengo
haya yameleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu wa kawaida sehemu nyingi duniani, hususan barani Afrika.
Ni dhahiri kuwa jamii nyingi zimenufaika
na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia sio kwa kufanyiwa hisani bali
kwa wao wenyewe kuwa na mikakati maalum ya kupiga hatua madhubuti za kujiletea
maendeleo stahimilivu na yaliyolenga kuleta usawa baina ya watu.
Mkutano wa Rio + 20
Ni jambo la kutia moyo kwamba maendeleo shirikishi na yenye kuleta usawa ni
baadhi ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano wa Rio +20 uliomalizika
hivi karibuni. Suala hili litachukua nafasi kubwa pia katika kuandaa mfumo wa
maendeleo unaotarajiwa baada ya mwaka
2015, mwaka uliokusudiwa kufikia malengo
ya maendeleo ya milenia. Nilipokabidhiwa
jukumu la kuratibu maandilizi ya ushiriki wetu kwenye mkutano wa Rio+20
nilitiwa moyo na nia ya dhati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kubuni
mkakati wa pamoja wa kutekeleza maazimio ya Rio+20. Napenda kuzishukuru nchi
wanachama kwa kufikia makubaliano katika masuala mengi yaliyojadiliwa Rio licha
ya changamoto nyingi zinazotokana na mtikisiko wa uchumi duniani. Ninafurahi
kwamba maazimio ya mkutano huu yatachangia upatikanaji wa maendeleo
stahimilivu, shirikishi na yenye kuleta usawa na hususan kuhakikisha kunakuwa
na mustakabali mzuri kwa wanawake na wasichana.
Uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia
Tukirejea kwenye suala hili, hata baada ya Mkutano wa Rio + 20 tutawajibika
kuendelea na juhudi za uwezeshaji wa wanawake na kuleta usawa wa kijinsia. Wakati wa utumishi wangu Umoja wa Mataifa
tumefanya bidii kubwa na kutumia muda mwingi kushughulikia suala hii. Tumetumia
hadhi na ushawishi wa ofisi yetu kupaza sauti za wanawake na wasichana na
kukuza ushiriki wao katika jamii. Tumeendesha kampeni za kupiga vita ukatili
kwa wanawake na wasichana. Tumezihimiza
mamlaka katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria
zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia, na tumetaka wapewe fursa kushika
nafasi za uongozi katika jamii. Ndiyo
maana kwa upande wetu hatukuweka koleo chini hadi pale tulipokamilisha
uanzishwaji wa idara inayojulikana kwa kifupi kama “UN Women” mnamo Julai 2010.
Hii ni idara ya Umoja wa Mataifa iliyoundwa
kwa madhumuni ya kuongoza masuala ya wanawake na usawa wa kijinsia kwa umakini
na ufanisi zaidi kuliko hapo awali. Tumefanya jitihada hizi kwa kuamini kuwa
hakuna uamuzi wowote ule, uwe mdogo au mkubwa, unaofanywa na Umoja wa Mataifa
bila ya kuzingatia maendeleo na ustawi wa wanawake na wasichana.
Huduma ya Pamoja
Kwa upande mwingine ninapenda kuwapongeza kwa dhati
wenzangu wote waliomo katika utumishi wa Umoja wa Mataifa,wake kwa
waume,walioutumia ujuzi na weledi wao wote kuchangia maendeleo ya nchi na jamii
tunazozihudumia. Natoa shukrani za pekee kwa wale wote waliopo kwenye ofisi na
vituo vya Umoja wa Mataifa nje ya Makao Makuu na ambao wanafanya kazi katika
mazingira magumu na yenye changamo nyingi. Hao wote wanadhihirisha umuhimu wa
kuwapo kwa Shirika hili kama chombo cha kuhimiza maendeleo katika ngazi zote za
kitaifa, kikanda na kimataifa. Katika
kutekeleza dhana ya “Huduma ya Pamoja” (Delivering
as One) Waratibu Wakaazi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na mchango muhimu
sana.Uratibu wao umeongeza ubora na wepesi wa utoaji huduma kwa nchi
wanamowakilisha Shirika. Hatuna budi kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika
kufanikisha dhana ya “Huduma ya Pamoja”.
Ni dhahiri kwamba uwezo wa nchi
mwanachama kumiliki mchakato wa maendeleo yake unakuwa imara zaidi
pale ambapo kuna mtiririko mzuri wa huduma za Umoja wa Mataifa na fursa
za kukuza ushirikiano endelevu na wadau wengine wa maendeleo. Wakati uamuzi rasmi kuhusu maendeleo ya dhana
hii ukisubiri kukamilika kwa majadiliano ya nchi wanachama, ninaamini kwa dhati
kuwa utaratibu wa kutoa “Huduma ya
Pamoja” kupitia mpango mmoja uliokubaliwa na wote ni mwelekeo sahihi na wenye
tija.
Nchini mwetu Tanzania, mashirika ya Umoja wa Mataifa
yamekuwa yakifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu sana toka mwaka 2011 kupitia
mpango mmoja uitwao “Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia Maendeleo” (United Nations Development Plan – UNDAP).
Mpango huu unakwenda sambamba na mwaka wa fedha wa Serikali yaani Julai 1 hadi
Juni 30 na kwa mantiki hiyo kuuwezesha kuzingatia vipaumbele vya Serikali.
Kupitia mpango huu Umoja wa Mataifa umejiwekea utaratibu wa kujipima na
kujitathmini ambao unatoa fursa kwa hatua za haraka kuchukuliwa inapobidi. Utaratibu
huu unapatikana kwenye tovuti. Kwa upande wa uendeshaji, mfumo huu wa utendaji
kazi kwa pamoja umetuwezesha kutekeleza majukumu mengi kwa kutumia raslimali
chache ambapo“ziada” iliyopatikana imeelekezwa kwenye shughuli nyingine za
maendeleo.
Afya ya Jamii
Katika eneo la afya, ambamo wanawake na watoto ndiyo
wanaathirika zaidi, hatua muhimu zinachukuliwa kupunguza vifo na
kuhakikisha kwamba kila mwanamke na kila mtoto anakingwa na maradhi, hususan
kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Tukiwa Nairobi Aprili mwaka 2011, Katibu Mkuu
Ban Ki-moon, Michel Sidibe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) pamoja nami tulishuhudia mfano hai wa jitihada
za Umoja wa Mataifa. Tulipata fursa ya kukutana na mwanamke aliyeathirika na
virusi ambaye alijaaliwa kupata mapacha watatu waliozaliwa bila ya maambukizi. Nikiwa
mjumbe wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa
iliyoshughulikia taarifa na uwajibikaji katika masuala ya afya ya mama na mtoto
(Commission on Information and
Accountability on Women's and Children's Health) ambayo iliendeshwa kwa
umahiri na Rais Kikwete wa Tanzania na Waziri Mkuu Harper wa Canada, nina imani
kwamba jumuiya ya kimataifa hivi sasa
imepata mfumo madhubuti utakaohakikisha kwamba kunakuwa na ufuatiliaji, usimamizi
na uwajibikaji kuhusu afya ya mama na mtoto. Hakuna shaka kwamba mfumo huu
utafikia hatua ya utekelezwaji siku za hivi karibuni.
Hali kadhalika, kazi nzuri imekuwa
ikifanywa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la
Mpango wa Uzazi Duniani (UNFPA), Babatunde Osotimehin, na Margaret Chan,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kuboresha afya ya mama na
mtoto. Matokeo ya jitihada za wenzangu
hawa yalikuwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya
Naibu Katibu Mkuu katika nyanja zote za maendeleo. Ama kwa hakika matunda ya
kazi zao yanaimarisha imani yangu kuwa Umoja wa Mataifa ni Shirika lenye
umuhimu mkubwa; na kwamba mchango wetu, japo mdogo, unasaidia sana katika
kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Nilijawa na imani kama hiyo nikiwa katika
ziara nyingine za kikazi. Kwa mfano nikiwa Montevideo, Uruguay, Novemba 2011, pamoja na wenzangu
Michelle Bachelet, Helen Clark na Alicia
Barcena, tulisimama kidete kuunga mkono
kampeni ya kitaifa ya kupiga vita vitendo vya ukatili kwa wanawake.
Nilipozuru Haiti mwezi Aprili2010, miezi michache baada ya tetemeko ambalo
lilikuwa kubwa kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini humo kwa kipindi cha
takriban karne moja, nilikutana na watu ambao walikuwa wameathirika vibaya
sana: waliopoteza familia nzima, waliopata ulemavu wa maisha, waliopoteza mali
zao zote! Lakini bado watu hawa walikuwa na nyuso za matumaini wakitarajia
mchango wa Umoja wa Mataifa na wa wadau wengine wa jumuiya ya kimataifa. Mnamo
Novemba 2010 tulizuru Laos, ambako Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na
Serikali na wadau wengine wengi katika utoaji wa misaada muhimu ya maendeleo
ikiwa ni pamoja na kuisaidia Laos kupambana na janga la mabaki ya mabomu ya
“cluster munitions”.
Hii ni mifano michache tu inayojibu hoja za wakosoaji wa
Umoja wa Mataifa.Ujumbe wangu kwao ni huu: wanyonge na wenye kutaabika sehemu
zote duniani ni mashuhuda na watetezi wakubwa wa Umoja wa Mataifa. Kwa wanyonge na wahitaji walio wengi Shirika
hili ni nguzo ya kutumainiwa katika jitihada zao za kila siku za kujiletea
maisha yenye utu na heshima.
Mageuzi katika menejimenti na usimamizi wa mabadiliko
Ukweli huu haumaanishi kuwa Umoja wa Mataifa hauna kasoro au upungufu. La
hasha! Ndiyo maana wakati wa utumishi wangu tulijielekeza kikamilifu kwenye
kuboresha masuala ya utawala, uendeshaji na namna tunavyofanya kazi. Ni wazi
kwamba hivi sasa Umoja wa Mataifa umebadilika kutoka chombo cha huduma za
mikutano na kuwa mtendaji mwenye majukumu muhimu nje ya kumbi za mikutano. Kwa
ushirikiano na msaada maridhawa wa wafanyakazi wenzangu, tulijikita katika
kuhamasisha mabadiliko ya kiutendaji katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja
na kujenga desturi ya uwajibikaji, uadilifu na kufanya kazi kwa tija zaidi huku
tukitumia rasilmali chache.
Ilitubidi pia kuweka mifumo thabiti ya kusimamia mabadiliko yaliyokuwa
yakijitokeza. Katika kufanya hivyo tulitambua wazi kwamba hakukuwa na njia ya
mkato wala njia mbadala ya kuliimarisha Shirika letu na kulifanya liwe la
kisasa zaidi katika kutekeleza majukumu yake.Tulihakikisha kwamba utendaji kazi
wetu unakwenda sambamba na changamoto zilizopo, lakini pia tulizingatia ufinyu
wa bajeti, misimamo tofauti na wakati
mwingine inayaokinzana ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Katika hali hii
ilitulazimu kuwa wabunifu zaidi ili kuleta muafaka baina ya nchi wanachama na
kuhakikisha kwamba raslimali chache zilizopo zinatoa tija kubwa zaidi.
Wafanyakazi ndiyo rasilmali kubwa kupita zote. Hivyo kila tulipoendelea na
jitihada za kuboresha Shirika ilitubidi kuwekeza vilivyo kwa wafanyakazi wa
Umoja wa Mataifa kwa kuwapatia fursa za mafunzo na msingi imara wa maendeleo
yao kazini. Ni jambo lililo dhahiri kuwa
wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanatekeleza majukumu yao katika
mazingira hatarishi na yenye kubadilika mara kwa mara. Tunafahamu, tena kwa
uchungu mkubwa, kuwa Bendera ya Umoja wa Mataifa -
“bendera ya bluu” - hivi sasa si
kinga tena. Haituhakikishii usalama
kwani wengi wa watumishi wetu mahiri wamekuwa wahanga wa matukio ya kikatili ya
ugaidi. Nilishuhudia tukio la aina hii huko Abuja, Nigeria, ambako watumishi
wenzetu walipoteza maisha kutokana na shambulio la kigaidi la tarehe 26 Agosti
2011. Na mara nyingi wenzetu wanapotangulia mbele ya haki, wapendwa wao
wanaachwa katika hali ngumu ya maisha. Ni faraja kubwa kwangu kuwa miongoni mwa
masuala ambayo tuliyasimamia kabla ya kumaliza utumishi wangu ni kuanzisha
mchakato wa kubaini namna bora ya kuwasaidia wahanga wa majanga hayo pamoja na
familia zao.
Utawala wa sheria
Mojawapo ya majukumu ya Umoja wa Mataifa ni kukuza sera zinazolenga kulinda
haki za binadamu na kuendeleza utawala wa sheria katika ngazi za kitaifa na
kimataifa. Leo hii, nchi nyingi zimelipa kipaumbele suala la kuimarisha utawala wa sheria, hususan
kufuatia umuhimu wake katika ajenda za ujenzi wa amani (peace-building) na
maendeleo stahimilivu. Kwa mantiki hiyo, nilifurahi nilipopata fursa ya
kusimamia ujenzi wa mfumo madhubuti wa sera na mwongozo wa utekelezaji wa
shughuli za utawala wa sheria nikishirikiana na nchi wanachama. Kwa upande wao
nchi wanachama zimepanga kufanya mkutano wa ngazi ya juu wakati wa kikao cha
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2012. Nia kubwa ni kuendeleza
jitihada katika suala hili ili kukuza heshima ya watu wote duniani na kujenga
amani kati ya mataifa.
Hitimisho
Japokuwa muda wangu wa utumishi katika Umoja wa Mataifa umefikia tamati,
naamini hakuna tamati katika utekelezaji wa malengo, misingi na maadili ya
Umoja wa Mataifa. Ili mradi bado kuna
umaskini duniani na mahitaji ya chakula; bado kuna changamoto ya kutunza utu na
heshima ya binadamu na haja ya kuimarisha amani duniani basi hakika nitaendelea
kuunga mkono jitihada, misingi na malengo ya Umoja wa Mataifa popote pale
nitakapokuwa. Kwani ni dhahiri kwamba njia bora ya kukabiliana na changamoto
kubwa zilizo mbele yetu ni kujenga ubia na ushirikiano wa karibu baina ya
serikali, asasi za kiraia, wafanyabiashara, mashirika ya hisani, taasisi za
kitaaluma na watu binafsi.
Aidha, ninaaamini kuwa vijana, kizazi ambacho kina kila sababu ya kuwa na kiu
ya kuishi kwenye dunia yenye utu, usawa, haki na amani, watauchukulia Umoja wa
Mataifa kuwa mbia wa kuaminika katika kujenga mustakabali wao.
Asha-Rose Migiro
No comments:
Post a Comment