Kutoka Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge:Ukweli Kuhusu Mishahara Ya Waheshimiwa Wabunge - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 21 June 2012

Kutoka Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge:Ukweli Kuhusu Mishahara Ya Waheshimiwa Wabunge



Wakati Bunge liko kwenye mchakato wa Bajeti ya 2012/13, yameanza kujitokeza maneno na taarifa mbalimbali juu ya kupanda kwa mishahara ya watumishi wa Umma wakiwemo Wabunge. Mathalani, siku ya Jumatano tarehe 20 Juni 2012, gazeti moja linatokalo kila siku lilikuwa na habari yenye kichwa kisemacho “Mishahara ya Wabunge juu”.

Ofisi ya Bunge imeona ni vyema kutoa ufafanuzi juu ya suala zima la mishahara ya Wabunge ili umma uweze kuelimika ipasavyo juu ya taratibu zinazotawala jambo hili kama ifuatavyo:

·         Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo inajumuisha Fungu Na. 42 lenye Bajeti ya Bunge bado haijasomwa Bungeni, na hivyo haiwezekani leo hii kueleza kuwa kuna nyongeza ya bajeti inayohusu mishahara kwa Wabunge.

·         Si kweli kwamba mishahara ya Wabunge imeongezwa toka kiwango wanacholipwa sasa, kwa kuwa mishahara yao kama ilivyo ya watumishi wote wa umma, hurekebishwa kwa waraka maalum  toka Ofisi ya Rais,  na si Kamisheni au Kamati yoyote ya Bunge.

·         Waraka wa mwisho wa toka Ofisi ya Rais unaotoa Masharti ya Kazi ya Mbunge ulitolewa tarehe 25 Oktoba 2010, na kueleza kuwa Mbunge atalipwa mshahara katika ngazi ya LSS (P) 2, na ni waraka huo unaotumika mpaka sasa. 

·         Mapendekezo ya ongezeko la 32% ya Bajeti ya Ofisi ya Bunge yaliyooneshwa kwenye kitabu cha Bajeti namba 2, cha matumizi ya kawaida yaliyowasilishwa mezani ni ya matumizi mengine ambayo hayana uhusiano na ongezeko la mishahara.


Mwisho, Ofisi ya Bunge wakati wote inathamini sana mchango wa vyombo vya habari katika juhudi za kuelimisha umma juu ya kazi za chombo chao cha uwakilishi. Hata hivyo, Ofisi inasikitishwa sana na habari za upotoshaji zinazotolewa kwa lengo la kujenga chuki kati ya Wabunge na watu wanao wawakilisha.

Kwa mantiki hiyo, tunazidi kuwasihi Waandishi waandike habari au makala baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu jambo husika na pale inapobidi waweze kupata ufafanuzi toka Idara husika katika Ofisi ya Bunge, ili kuepuka kuupotosha umma.


Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge,
S.L.P 941, DODOMA.
21 Juni 2012

No comments:

Post a Comment