Mshukiwa wa mashambulio ya mabomu katika kanisa moja nchini Nigeria siku ya Krismasi amekamatwa tena, mamlaka za Nigeria zimesema.
Maafisa wanasema, mshukiwa huyo, Kabiru Sokoto alikamatwa katika jimbo la mashariki la Taraba.
Anatuhumiwa kuwa mfuasi wa kundi la Boko Haram, ambalo lilisema liliendesha shambulio hilo.
Kutoroka kwake mwezi uliopita kulitia aibu polisi, ambapo mkuu wa polisi alifukuzwa kazi muda mfupi baadaye.
Boko Haram imefanya mfululizo wa mashambulio katika miaka ya hivi karibuni. Mwezi uliopita watu 185 waliuawa wakati wa mfululizo wa mashambulio mjini Kano.
Makumi ya watu walikufa katika kanisa moja kwenye viunga vya mji mkuu, Abuja, siku ya Krismasi.
Bw Sokoto kwanza alikamatwa mwezi uliopita, lakini alitoroka siku ya pili wakati akisafirishwa na polisi.
"Alikamatwa tena asubuhi ya leo mjini Mutum Biu katika jimbo la Taraba na makachero wa polisi," taarifa ya kiusalama imekaririwa na shirika la habari la AFP. "Anapelekwa Abuja sasa hivi na jeshi la anga la Nigeria." Mamlaka zimesema Bw Sokoto alipanga mashambulio ya mabomu Disemba 25 katika kanisa la Mtakatifu Theresa, la Katoliki katika eneo la Madalla, nje kidogo ya Abuja.
Alitoroka mwezi uliopita wakati polisi wakimpeleka nyumbani kwake ili kufanya upekuzi. Polisi walisema msafara wao ulishambuliwa na watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Boko Haram.
Waandishi wa habari walisema wakati huo kuwa ni uzembe wa polisi. Baadhi ya watu wanahisi huenda kuliwa na mzozano kati ya maafisa wa usalama na Boko Haram.
Boko Haram, - jina ambalo maana yake ni "elimu ya Magharibi ni haramu", wanataka kuanzisha sheria za Kiislam nchini Nigeria.
Nigeria, ambayo ni nchi yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika ikiwa na watu milioni 160, imegawanyika kati ya Waislam waishio kaskazini, na upande wa kusini wenye Wakristo wengi na watu wasio na dini.
No comments:
Post a Comment