Maisha : Bilionea David Mulokozi Afanyiwa Birthday ya Kifalme, Banana Zoro Aitikisa Babati - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Thursday, 19 March 2026

Maisha : Bilionea David Mulokozi Afanyiwa Birthday ya Kifalme, Banana Zoro Aitikisa Babati



Na Mwandishi Wetu.

Babati, Manyara: Sherehe ya kumbukizi ya kuzaliwa ya Mkurugenzi wa Mati Super Brands Ltd, Bilionea David Mulokozi, imegeuka kuwa somo la upendo na kuthaminiana baada ya mkewe, Doreen Mulokozi, kumuandalia tukio la kushtukiza lililogusa wengi.

Katika sherehe hiyo iliyofanyika Babati Mjini na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa, Doreen alimzawadia mumewe zawadi mbili kubwa—ikiwa ni pamoja na kumualika mwanamuziki anayempenda, Banana Zoro, ambaye aling’ara jukwaani kwa burudani ya hali ya juu na kukonga nyoyo za mwenyeji wa hafla pamoja na wageni wote.


Mbali na burudani hiyo iliyoongeza shamrashamra katika tukio hilo, Doreen alimkabidhi mumewe gari kama zawadi maalum ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa, hatua iliyodhihirisha mapenzi ya dhati na kuthamini mchango wake ndani ya familia.

Kwa upande wake, Banana Zoro alitoa shukrani zake za pekee kwa mwaliko huo, akieleza kuwa kushiriki katika hafla hiyo kumekuwa na maana kubwa kwake binafsi na kitaaluma.

Akizungumza kwa hisia na furaha, David Mulokozi alimshukuru mkewe kwa maandalizi hayo pamoja na zawadi ya kushtukiza, akieleza kuwa tukio hilo limekuwa moja ya kumbukumbu muhimu zaidi katika maisha yake.
“Kumbukizi yangu ya kuzaliwa alinifanyia mke wangu Doreen… kwangu vilikuwa vitu vya kipekee sana katika maisha yangu,” alisema Mulokozi.

Kwa utani, Mulokozi aliwataka pia wanawake wengine kuiga mfano huo kwa kuwapatia waume zao zawadi zenye thamani, badala ya zawadi ndogo ndogo za kawaida, jambo lililozua vicheko na furaha miongoni mwa wageni waliohudhuria.
Naye Doreen alimtakia mumewe baraka na mafanikio zaidi katika shughuli zake, huku akimuomba aitunze zawadi hiyo kama kumbukumbu muhimu ya upendo wao ili waendelee kuikumbuka hata watakapokuwa wazee.
Sherehe hiyo ilifanyika kwa mafanikio makubwa, ikijumuisha burudani, furaha na mshikamano wa kifamilia pamoja na marafiki, huku ikiakisi ujumbe mzito wa kuthaminiana, upendo wa kweli na umuhimu wa kusherehekea maisha pamoja.

No comments:

Post a Comment