Tuzo : NCAA Yajivunia Tuzo ya Kimataifa - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Thursday, 3 July 2025

demo-image

Tuzo : NCAA Yajivunia Tuzo ya Kimataifa

Badru%201
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Bw. Abdul-Razaq Badru kupitia mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika jijini Arusha tarehe 30 Juni, 2025 amewashukuru Watanzania, Wadau wa Sekta ya Utalii na wageni mbalimbali waliotembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwa kuipigia Kura hifadhi hiyo na kuiwezesha kutangazwa kuwa Kivutio bora cha Utalii Barani Afrika mwaka 2025.
badru%203

badru%202


Na Said Njuki, Manyara Media Pro

WAKATI dunia ikishuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira kote duniani, Mamlaka ya Eneo la Hifadhi la Ngorongoro (NCAA) kwa upande wake inajivunia tuzo bora ya kimataifa ya mwaka 2025.

Tuzo hiyo iliyotangazwa na mtandao wa World Travel Awards (WTA) Juni 28, mwaka huu jijini Dar es Salaam, imeifanya NCAA kuwa kivutio bora cha utalii zaidi barani Afrika kwa mwaka 2025 (Africans leading tourist attractions 2025).

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo, Abdul-Razaq Badru akiongea na waandishi wa habari juzi jijini Arusha alisema NCAA imepata tuzo hiyo kutokana na vigezo halisia vilivyomo katika hifadhi hiyo.

"NCAA si tu kivutio bali ni hazina hai ya maumbile ya kipekee iliyohifadhiwa vizuri karne na karne na kuwa urithi wa kihistoria na utamaduni wa asili kuanzia Kreta ya Ngorongoro lakini pia Nyayo za Laetoli zenye umri wa zaidi ya miaka milioni 3.6 iliyopita".alisema Badru na kuongeza.

"Uhamaji wa nyumbu unaovuka savana zisizo za mwisho, makumbusho ya Olduvai, mchanga unaohama pamoja na mlima Lolmalasin ambao ni wa tatu kwa urefu nchini...vivutio hivi kwa ujumla vinipa thamani kubwa NCAA na kuwa kivutio bora na utalii Afrika kwa mwaka 2025".

Alisema ni jambo kubwa la kujivunia kwani  NCAA pia imekuwa kivutio bora cha utalii Afrika kwa mwaka 2023 si kwa kubahatisha ni ubora wake wa asili ukihanikizwa na utunzaji shirikishi na makini wa mazingira katika eneo hilo.

Mamlaka ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro inazo hadhi tatu zinazotambulika kimataifa tofauti na hifadhi zingine ambazo ni urithi mchanganyiko wa dunia (Mixed World Heritage Site), hifadhi hai ya kimataifa (Biosphere Reserve) na hifadhi ya kijiolojia ya Ngorongoro-Lengai (Ngorongoro-Lengai UNESCO Global Geopark).

Kamishna Badru alisema mafanikio haya si ya NCAA pekee kwani yamepatikana kwa juhudi shirikishi na wadau wa utalii akiwemo Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu yake maarufu ya "The Royal Tour" na Amazing Tanzania.

"Kupitia ushindi huu tunatoa pongezi za dhati kwa wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika sekta ya utalii ambapo kupitia filamu zake, anetangaza vivutio vyetu duniani na kuendelea kuiletea heshima Tanzania kupitia tuzo mbalimbali". Alisisitiza Kamishna Badru.

Alitoa shukrani kwa wadau wa utalii walioshiriki kuipigia kura NCAA wakiwemo wageni wa mataifa mbalimbali waliotembelea hifadhi hiyo, viongozi na wanafunzi wa vyuo vikuu na waandishi wa habari kwa kutimiza jukumu lao la kuhabarisha jamii.


Katika hatua nyingine Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) aliwavisha vyeo Manaibu Kamishna wawili na kushuhudia uvishwaji vyeo kwa Makamishna Wasaidizi waandamizi watano.

Makamishna Wasaidizi Waandamizi hao watano, waliovishwa vyeo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Eneo la Hifadhi la Ngorongoro (NCAA) Jenerali (Mustaafu), Venance Mabeyo.

Waliovishwa vyeo na Waziri ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Joas Makwati aliyepandishwa cheo kuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Uhifadhi, utalii na Maendeleo ya Jamii na Naibu Kamishna wa Uhifadhi Aidan Makalla anayesimamia Huduma za Shirika NCAA.

Makamishna waliovishwa vyeo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NCAA ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia idara ya Mipango na Uwekezaji, Gasper Lyimo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Paul Shaidi anayesimamia Kitengo cha huduma za Sheria, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Charles Wangwe anayesimamia Idara ya Uhasibu na fedha.

Wengine ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwin Kashaga anayesimamia Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani, na Afisa Uhifadhi Mkuu Daraja la kwanza Mariam Kobelo anayesimamia Idara ya Huduma za Utalii na masoko aliyepandishwa cheo kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi.

Katika hafla hiyo, Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) aliwataka Makamishna hao kufanya kazi kwa bidiii na weledi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa cheo ni dhamana na kinakuja na majukumu.

“Nimatumaini yangu kuwa viongozi wote mliovaa vyeo leo mtakuwa chachu ya kufanya kazi kwa kujituma na kuonesha mfano wa kuigwa kwa Maafisa na Askari mnaowaongoza, juhudi zenu ndiyo zitakazochangia kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro na kuendelea kuwa kivutio kwa wageni wanaotembelea”. Alisema Balozi Chana.

Kwa upande wakale Kamishna wa Uhifadhi NCAA Abdul-Razak Badru alisema watumishi wote wameshapatiwa mafunzo ya kijeshi kutoka mfumo wa awali wa kiraia na kuwa mamlaka hivyo itahakikisha inatumia rasilimali ya watumishi waliopo kuongeza nguvu ya kuhifadhi, kulinda, kuendeleza jamii na kuboresha miundombinu ya utalii.

Mwenyekiti wa bodi ya NCAA Jenerali, Venance Mabeyo (mstaafu) alisema kuwa mafanikio ya Ngorongoro yanategemea uadilifu na uwezo wa viongozi wake  huku akiwaasa viongozi hao kubeba matumaini mapya katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii. 

No comments:

Post a Comment

Tuwasiliane

Name

Email *

Message *

Contact Form

Name

Email *

Message *