Sheria : Tufanye Kazi kwa Haraka na Ubora - Mwanasheria Mkuu wa Serikali - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Wednesday, 26 March 2025

demo-image

Sheria : Tufanye Kazi kwa Haraka na Ubora - Mwanasheria Mkuu wa Serikali

 

Na Pamela Mollel, Arusha


Arusha, Machi 25, 2025 — Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Said Johari, ametoa wito maalum kwa Mawakili na Wanasheria wote wa Serikali kuzingatia ubora na weledi katika utoaji wa huduma za kisheria, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa wakati ili kuchochea maendeleo ya Taifa.

Akizungumza jijini Arusha katika mafunzo ya pili ya mwaka kwa Mawakili wa Serikali, Mhe. Johari alieleza kuwa ucheleweshaji usio wa lazima katika utoaji wa huduma umekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi za Afrika, na Tanzania haiwezi kukwepa kuathirika endapo haitachukua hatua madhubuti.

“Kaulimbiu yetu ni weledi na ubora, lakini hayo hayawezi kufikiwa kama hatufanyi kazi kwa haraka na kwa wakati. Ugonjwa huu wa kuchelewa chelewa ni tatizo kubwa – unaturudisha nyuma kama Taifa,” alisema Mwanasheria Mkuu huyo kwa msisitizo.

Johari aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza umahiri wa wataalamu wa sheria katika utendaji kazi wao wa kila siku, huku lengo kuu likiwa ni kuleta matokeo yenye tija kwa wananchi kupitia huduma bora za sheria zinazotolewa kwa wakati.

“Tunataka kuacha tabia ya kuahirisha mambo bila sababu za msingi. Tabia hiyo huwanyima wananchi haki zao kwa kuchelewa kupata huduma wanazostahili. Lazima tubadilike,” alisema.

Akitazama mbele, Johari alisema Tanzania inalenga kufikia uchumi wa kati wa viwango vya juu ifikapo mwaka 2050, jambo ambalo haliwezi kufanikiwa kama sekta ya sheria haitaimarika katika kasi na ubora wa huduma zake.

Kwa upande wake, Mwandishi Mkuu wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mratibu wa Mafunzo hayo, Rehema Katuga, alifafanua kuwa ofisi hiyo ina jukumu pana la kuishauri Serikali kwenye masuala yote ya kisheria.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na ushauri kuhusu mikataba, manunuzi ya umma, uandishi wa sheria, pamoja na uangalizi wa utekelezaji wa sheria mpya zinazotungwa.

“Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka, hasa ikizingatiwa kuwa tunakutana na changamoto kama kuvunjika kwa mikataba, ambayo mara nyingi husababishwa na mapungufu katika maandalizi au utekelezaji wake. Tunahitaji ujuzi wa hali ya juu ili kukabiliana na changamoto hizi kwa ufanisi,” alisema Katuga.

Mafunzo haya yamewaleta pamoja Mawakili wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali nchini, yakilenga kuwaongezea maarifa na mbinu mpya katika kutekeleza majukumu yao kwa haraka, kwa ufanisi, na kwa
 maslahi ya umma.

PHOTO-2025-03-25-23-27-48

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Said Johari akizungumza jijini Arusha katika mafunzo ya pili ya  mwaka kwa Mawakili wa Serikali

PHOTO-2025-03-25-23-27-48%20(4)


PHOTO-2025-03-25-23-27-48%20(3)
Sehemu ya washiriki wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu
PHOTO-2025-03-25-23-27-48%20(2)
Sehemu ya washiriki
PHOTO-2025-03-25-23-27-48%20(1)
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Said Johari akiwa meza kuu na viongozi wengine jijini Arusha katika mafunzo ya pili ya  mwaka kwa Mawakili wa Serikali
PHOTO-2025-03-25-23-27-48%20(5)
Mwandishi Mkuu wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mratibu wa Mafunzo hayo, Rehema Katuga, akiongea na wanahabari

No comments:

Post a Comment

Contact Form

Name

Email *

Message *

Tuwasiliane

Name

Email *

Message *