Picha Zote na Othman Michuzi, Mtaa Kwa Mtaa Blog
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Akson ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuandaa bonanza la pamoja la michezo lililopewa jina la “CRDB Bank Pamoja Bonanza” kwa mafanikiao makubwa pamoja na kuhamasisha utamaduni wa kushiriki katika michezo na kujenga afya na kuhamasisha mshikamano kwa Watanzania katika shughuli za maendeleo.
Akizungumza katika bonanza hilo, Spika alisema kuwa bonanza hilo limeleta msisimko na mwamko mkubwa kulinganisha na miaka ya nyuma, ambapo mwaka huu idadi ya washiriki imeongezeka na kufanya maana na lengo halisi la mashindano hayo kupata umaarufu jijini Dodoma na Tanzania kwa ujumla.
“Kwa mwaka huu tumeona hata ndugu zetu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na pia vijana wetu wa Bongo Flava ambao kwa pamoja wameleta msisimko mkubwa na kuleta ushindani, hongereni sana ndugu zetu Benki ya CRDB kwa kuwa na maono makubwa hivi”. Alisema Tulia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema Benki ya CRDB inaipa kipaumbele michezo, kwani michezo ni afya, inaleta umoja na upendo, inawaleta pamoja Wafanyakazi wa Benki na wadau mbalimbali wa Michezo nchini. Hivyo Benki inatumia bonanza hilo kama sehemu tu ya kuisogeza karibu na Serikali, Bunge na wadau mbalimbali nchini ili kupata nafasi ya kusikiliza mahitaji yaliyopo na kujua namna gani benki inaweza kushiriki katika mipango ya maendeleo ya nchi na kuthibitisha kauli mbiu yake ya “Ulipo Tupo” na kuwa ni benki inayomsikiliza Mteja.
Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Benki ya CRDB, Ally Laay aliwashukuru Wabunge na wadau mbalimbali wa serikali na wananchi waliohudhuria mashindano hayo na kujitokeza kwa wingi kushiriki bonanza hilo lililotanguliwa na matembezi yaliyo anzia katika viwanja vya bunge vikiwemo vikundi mbalimbali vya Jogging, wanafunzi wa vyuo na Sekondari pamoja na wananchi kwa kutambua umuhimu wa michezo.
Mashindano hayo yalimalizika kwa Timu za Bunge la Jamhuri wa Muungano kutwaa ushindi wa jumla kwa Mpira wa Miguu, Mpira wa Kikapu, Mpira wa Pete pamoja na Ule wa kuvuta kama (Tag of War) katika bonanza hilo.
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Mhe. Tabia Maulid Mwita akizungumza wakati akitoa salamu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, katika Bonanza la Pamoja la Benki ya CRDB (CRDB Bank Pamoja Bonanza), lililofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma Juni 25,2022. |
No comments:
Post a Comment