Kilimo : Waziri azindua Mfumo wa Ukaguzi wa Mifugo. - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Saturday, 28 August 2021

Kilimo : Waziri azindua Mfumo wa Ukaguzi wa Mifugo.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), (wa pili kutoka kulia) akizindua rasmi mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma na kuwataka watekelezaji wa mfumo huo kutogeuka kuwa Jeshi la Polisi au mahakama. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake iliyofanyika jijini Dodoma na kubainisha kuwa mfumo utaboresha na kuongeza thamani mazao ya mifugo nchini. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo Bw. Amosy Zephania akifafanua juu ya mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake ambao umewezesha kufanyika mapitio ya sheria tatu za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama ya mwaka 2010, Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 na Sheria ya Veterinari ya mwaka 2003 na kanuni 12. Hafla fupi ya uzinduzi wa mfumo huo imefanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma akibainisha umuhimu wa kuzinduliwa kwa mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake ambao umeshirikisha wananchi, katika hafla fupi ya uzinduzi wa mfumo huo iliyofanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na baadhi ya washiriki wa hafla fupi ya uzinduzi wa mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake, iliyofanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

 

 

Na. Edward Kondela

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amezindua mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake na kuwataka watakaotekeleza mfumo huo kutogeuka kuwa Jeshi la Polisi na watoa hukumu kwa wananchi.

 

Mhe. Ndaki ametoa kauli hiyo (27.08.2021) jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa mfumo huo ili kuongeza tija na kuinua pato la taifa kupitia sekta ya mifugo.

 

Amesema mfumo huo ni rahisi na ushirikishwaji hivyo ni vyema wakaguzi kutogeuka kuwa Jeshi la Polisi na kuwasumbua wadau wa sekta ya mifungo.

 

“Utaratibu huu ni wa ushirikishwaji, sasa tunapokuwa huko kufanya ukaguzi kuhusiana na ubora na viwango tusijigeuze sisi kuwa polisi. Kwa nchi yetu mfumo huu ni rahisi na ambao umelenga kuzipatia taarifa wizara, taasisi na wadau wengine kuhusiana na ukaguzi, ubora na usalama wa mifugo pamoja na mazao yake.” Amesema Mhe. Ndaki

 

Ameongeza kuwa umuhimu wa mfumo huo ni kuhakikisha utekelezaji wa wajibu wa kulinda afya za walaji, mifugo na mazao yake kwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu jambo ambalo litasaidia wafugaji kuzalisha mifugo kwa tija kwa kutumia pembejeo na huduma zilizosajiliwa na kutambuliwa kisheria.

 

Aidha ametoa rai kwa wakaguzi kutumia mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake kuhakikisha sheria, kanuni, taratibu za kusimamia na udhibiti wa ubora, usalama na viwango stahiki vinasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.

 

Pia, ametumia fursa hiyo, kutoa wito kwa wataalam wa wizara, mamlaka za serikali za mitaa, taasisi na wadau waliopo kwenye vyama vya tasnia kuhakikisha wakaguzi, wazalishaji, watoa huduma kwenye mifugo wanazingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kuhakikisha mlaji wa mifugo na mazao yake anaendelea kunufaika kiafya na kimaslahi kupitia maziwa, nyama na mayai na bidhaa nyingine.

 

Waziri Ndaki amewaomba wafugaji wote nchini kujenga utamaduni wa kutumia pembejeo na malighafi zenye ubora, usalama, viwango stahiki kutoka kwenye vyanzo vilivyosajiliwa kwenye uzalishaji wa mifugo.

 

“Hatua hii muhimu itasaidia upatikanaji wa bidhaa bora zinazozalishwa, kuchakatwa na kukaguliwa na wataalam wa mifugo hapa nchini.” Amefafanua Mhe. Ndaki

 

Awali, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Miugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Bw. Amosy Zephania amesema wizara imeanzisha na kuboresha mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake ambao umejikita kwenye tasnia za kuku, maziwa, nyama, mayai, ngozi, malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo.

 

Amebainisha kuwa mfumo huo umeanishwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa maboresho ya ufugaji kibiashara (L-MIRA) ambao umewezesha kufanyika mapitio ya sheria tatu za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama ya mwaka 2010, Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 na Sheria ya Veterinari ya mwaka 2003 na kanuni 12.

 

Bw. Zephania amesema mfumo huo umelenga kuongeza ari na hamasa ya uwekezaji kwenye sekta ya mifugo kwa kutatua changamoto za ubora, usalama na viwango stahiki kwenye mifugo, mazao ya mifugo na pembejeo za mifugo.

No comments:

Post a Comment