WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 utakaogharimu shilingi trilioni 114.8, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 40.6 na sekta ya umma shilingi trilioni 74.2.
“...fedha hizo zinajumuisha mikopo na misaada ya wabia wetu wa maendeleo. Kwa niaba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kuwahakikishia kwamba fedha hizi zitapatikana na malengo tuliyojiwekea yatatekelezwa.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Juni 29, 2021) wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema mpango huo una dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu na umejikita katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.
Amesema Serikali itahakikisha malengo ya Mpango huo yanafikiwa. “Kamwe hatutafumbia macho tabia ya ukwepaji kodi, kazini, ufujaji wa fedha na rushwa na tutaendelea kuenzi bunifu na kupokea mawazo mbadala yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa Mpango huu.”
“Katika Mpango huu wa Tatu tutaendelea kutekeleza miradi ya kielelezo kama ilivyokuwa katika Mpango wa Pili hususan ujenzi wa reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115; ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta (EACOP) na ununuzi wa meli na ujenzi wa bandari ya uvuvi (Mbegani).”
Kadhalika, Waziri Mkuu ameongeza kuwa mpango huo ni mkakati mahsusi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020. “Niwaahidi Watanzania kwamba mambo yote tuliyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020, yanaenda kutekelezwa kupitia Mpango huu.”
Waziri Mkuu amesema mpango huo umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025; Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020; Mpango Elekezi wa Muda Mrefu 2011/2012–2025/2026 na Matokeo ya Tathmini Huru ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/2017–2020/2021.
Pia, Waziri Mkuu amesema mpango huo umezingia sera na mikakati mbalimbali ya kisekta; matokeo ya tafiti zilizofanywa na vyuo na taasisi mbalimbali nchini; Dira ya Afrika Mashariki 2050; Dira ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika 2050; Ajenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; na Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
“Wizara ya Fedha na Mipango endeleeni na utaratibu wa kutoa elimu ya kutosha ili kumwezesha kila mmoja kushiriki kikamilifu katika utekelezaji. Aidha, ninaagiza Wizara, Taasisi za Umma, Idara Zinazojitegemea Wakala za Serikali, Sekta Binafsi na Wadau wote wa maendeleo kuhakikisha ofisi zao zina nakala ya Mpango huu na kuanza kuutekeleza.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuimarisha upangaji mipango na kusimamia rasilimali za ndani ya nchi ikijumuisha rasilimali za madini, maliasili, gesi asilia, ardhi, fedha na rasilimali watu kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wote.
Amesema ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi na unafikia malengo yaliyopangwa, Wizara imeandaa mwongozo wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi na programu za maendeleo na mfumo wa kitaifa wa kusimamia miradi ya maendeleo.
Naye, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Nchini Tanzania, Christine Musisi amesema wananchi, Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi watautumia mpango huo kama nyenzo muhimu ya utekelezaji wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. Pia ameihakikishia Serikali kwamba mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yataunga mkono utekelezaji wa mpango huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment