NA WAMJW-DAR ES SALAAM
TAASISI ya Mifupa nchini MOI sasa itafanya upasuaji wa mifupa kwa wagonjwa wapatao 1000 kwa mwezi kutoka wagonjwa 500 mpaka 700 baada ya kupokea msaada wa chumba cha upasuaji na vifaa vyake kutoka kwa Serikali ya Kuwait .
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa kuzindua na kupokea msaada wa chumba cha upasuaji na vifaa vyake vyenye thamani ya shilinigi milioni 186 leo katika Taasisi ya mifupa MOI leo jijini Dar es salaam.
“Hii ni faraja kubwa sana kwa Serikali kwani uboreshwaji wa huduma katika hospitali zetu za kibingwa kubwa kama MOI itaweza kuhudumia wagonjwa wengi Zaidi kutoka wagonjwa 700 kwa mwezi mpaka kufikia 1000 kwa mwezi” alisema Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Aidha Makamu wa Rais Samia Suluhu amesema kuwa anaishukuru Serikali ya Kuwait kupitia Balozi wake Jasem Al Najem kwa msaada huo kwani utaisaidia kwa kiasi kikubwa MOI katika kuboresha utoaji huduma hasa katika fani ya upasuaji kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi hapa nchini.
Kwa uapnde wake Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa kukamilika kwa vyumba hivi viwili vya upasuaji, kutaiwezesha Taasisi ya MOI kuwa na jumla ya vyumba vya upasuaji 8 kutoka 6 vilivyopo sasa na miongoni mwa vyumba hivi vya upasuaji kimoja kitakuwa maalumu kwa ajili ya watoto tu.
“MOI imeshatoa matibabu ya upasuaji kwa wagonjwa 1,670 ikiwemo upasuaji mifupa (wagonjwa 1,228), kubadilisha nyonga (wagonjwa 84), kubadilisha goti (wagonjwa 72), upasuaji wa uti wa mgongo (wagonjwa 109), ubongo (wagonjwa 64), na watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi (wagonjwa 113” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika kuimarisha na kuboresha afya za Watanzania jengo hilo pia litakuwa na vitanda 16 vya ICU (Intensive Care Unit) na 16 vya HDU (High Dependency Unit), hivyo kuimarisha huduma za tiba kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
Naye Balozi wa Kuwait Nchini Balozi Jasem Al Najem amesema kuwa Nchi ya Kuwait ipo mstari wa mbele katika kuhakikisha Hospitali na Vituo vya afya nchini Tanzania vinatoa huduma bora za Afya kwa kutumia Taaluma na ujuzi wa kisasa ikiwemo vifaa na vifaa tiba .
“Serikali ya Kuwait itakuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha afya za wananchi kwa kuendelea kutoa misaada mbalimbali ikiwemo vifaa,vifaa tiba na wataalamu wa afya na kutochoka katika hilo” alisema Balozi Najem.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya MOI Bi. Zakia Mejhi amesema kuwa Taasisi yake imeokoa Bilioni 3 za kufanyia upasuaji kwani kwa sasa huduma hizo za kibingwa zinafanyika nchini kwa Shilingi Bilioni 12 kutoka Bilioni 15 za rufaa ya kwenda kutibiwa nje.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema uboreshaji wa huduma katika hospitali zetu za kibingwa kama MOI, zitaipunguzia Serikali mzigo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi na hivyo kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kupokea vifaa vya Chumba Cha Upasuaji wa Watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI) leo tarehe 15 Mei, 2018.“ Aidha kwa namna ya kipekee nakushukuru Mheshimiwa Balozi wewe binafsi na Serikali ya Kuwait kwa ushirikiano ambao mnaendelea kuipatia Serikali yetu ya awamu ya Tano katika Sekta mbalimbali za maendeleo lakini hasa hasa katika sekta ya afya” alishukuru Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais amesema kuwa Balozi wa Kuwait Mhe. Jasem Al Najem amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza sekta ya Afya hapa nchini ambapo leo wamesaidia vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 258 ambavyo vitaiwezesha Taasisi kuimarisha utoaji wa huduma ya upasuaji hasa kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Makamu wa Rais amesema msaada huo utaiwezesha Taasisi kuwa na chumba cha upasuaji ambacho kitakuwa maalum kwa watoto tu, hivyo idadi ya wagonjwa watakaopata huduma ya upasuaji itaongezeka kutoka 500-700 kwa mwezi, kufikia zaidi ya wagonjwa 1000 kwa mwezi na watahudumiwa kwa haraka zaidi.
Wakati huo huo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile amesema Tanzania iatendelea kuimarisha uhusiano na nchi ya Kuwait kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada haswa msaada inayohusu sekta ya afya.Balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Al Najem amesema kuwa Wananchi wa Kuwait wana mapenzi makubwa na Watanzania na kuahidi wataendelea kutoa msaada.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa hafla ya kupokea vifaa vya chumba cha upasuaji wa watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsalimia mtoto Daniella Wilfred Pallangyo mwenye umri wa miaka 8 ambaye ana matatizo ya kichwa kikubwa wakati wa hafla ya kupokea vifaa vya chumba cha upasuaji wa watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI). (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa kuwait nchini Mhe. Jasem Al Najem wakati wa hafla ya kupokea vifaa vya chumba cha upasuaji wa watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI). (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa hafla ya kupokea vifaa vya chumba cha upasuaji wa watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI). (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo ya baadhi ya vifaa vya upasuaji kutoka kwa Dkt. Karima Khaled wakati wa hafla ya kupokea vifaa vya chumba cha upasuaji wa watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI). (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo ya baadhi ya vifaa vya kisasa vya upasuaji vinavyoweza kuona mishipa na kuisoma kutoka kwa Dkt. Karima Khaled wakati wa hafla ya kupokea vifaa vya chumba cha upasuaji wa watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI). (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
No comments:
Post a Comment