Matukio : Burudani kibao kupagawisha uzinduzi wa Handeni Kwetu Cup - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Saturday, 17 March 2018

Matukio : Burudani kibao kupagawisha uzinduzi wa Handeni Kwetu Cup




BENDI kongwe ya muziki wa dansi hapa nchini, The African Stars Twanga Pepeta, inatarajiwa kuonyeshana ubabe na msanii wa muziki wa singeli anayetamba nchini, Suleiman Jabir 'Msaga Sumu' katika shoo ya uzinduzi wa ligi ya Handeni Kwetu Cup, utakaofanyika Machi 24, katika Uwanja wa Mkata, wilayani Handeni, mkoani Tanga kuanzia asubuhi hadi jioni itakapomalizika mechi ya ufunguzi ya mpira wa miguu.

Ligi hiyo inayoratibiwa na Kambi Mbwana kwa kushirikiana na Chama Cha Soka wilayani Handeni (HDFA), inasubiriwa kwa hamu na wadau wa michezo na burudani katika viwanja mbalimbali vya Kata wilayani Handeni, ambapo mbali na Twanga Pepeta na Msaga Sumu, wasanii wengine watakaotumbuiza ni Nyota wa Bongo Fleva, Top C, Bendi ya Handeni Super Makoba, wasanii wa muziki wa kizazi kipya wa Handeni na vikundi vya burudani vya asili.


Akizungumzia tukio hilo, Mbwana ambaye pia ni mdau wa maendeleo wilayani Handeni, alisema uzinduzi huo utaweka historia kutokana na mikakati kabambe ya kuhakikisha kwamba mashabiki wanapata kitu kizuri kutoka kwa wasanii na wacheza soka kwa ujumla.

"Bendi ya Twanga Pepeta itakuwa na ziara Tanga Mjini kuanzia Machi 23 katika Ukumbi wa Tanga Hotel na Machi 24 usiku katika ukumbi wa Rombo Hotel, hivyo tumewaomba wakitoka Tanga, wapitie uwanjani Mkata ili wawape burudani ya dansi kwenye uzinduzi huo ambapo wameridhia.


" Ukiacha Twanga ambao pia watafanya burudani wilayani Korogwe katika ukumbi wa Mamba Club Machi 25 siku ya Jumapili, pia Msaga Sumu atakuwepo uwanjani Mkata ili kuonyesha namna gani mwanaume atakuwa machine kama mashairi yake yanavyosema, tukiamini kuwa wasanii wote waliothibitishwa kuwapo Mkata kwenye uzinduzi huo watafanya vitu vya hali ya juu, hivyo tunawaomba mashabiki waje kwa wingi uwanjani kujipatia burudani," Alisema Mbwana.

Kwa mujibu wa Mbwana, viingilio vya uzinduzi wa ligi hiyo Machi 24 Mkata vitakuwa Sh 3,000 kwa watu wazima na Sh 1,000 kwa watoto, huku onyesho la Handeni Mjini la Twanga Pepeta na Msaga Sumu Ukumbi wa Rombo likiwa ni sh 7,000, wakati lile la Tanga Hotel Machi 23 nalo ni Sh 7,000 kama litakavyokuwa onyesho la Korogwe Mjini Jumapili ya Machi 25 ambapo mashabiki wa bendi ya Twanga Pepeta watalazimika kulipa sh 7,000.

Twanga Pepeta wameamua kuja mkoani Tanga kujibu kiu za mashabiki wao baada ya kutokuja muda mrefu, hivyo mashabiki wao wa wilayani Handeni, Korogwe na Tanga Mjini watapata sehemu nzuri za kuangalia makali ya bendi hiyo ambapo katika Ukumbi wa Mamba Club (Korogwe) na Tanga Hotel (Tanga), watakuwa peke yao jukwaani, tofauti na Msaga Sumu na wengineo watakaopanda jukwaani Mkata na Handeni mjini Machi 24.

No comments:

Post a Comment