NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
INAELEZWA kuwa umeme wa maji, (Hydro power) ndio umeme wenye bei nafuu zaidi ukilinganisha na umeme unaotokana na vyanzo vingine.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa TANESCO anayeshughulikia uzalishaji (Power Generation), Mhandisi Abdallah Ikwasa, matumizi ya juu ya umeme nchini kwa sasa ni Megawati 1,060, kati ya hizo, TANESCO kwa kutumia mitambo yake, huzalisha Megawati zaidi ya 1,000, na kati ya hizo, Megawati 381 zinatokana na umeme unaozalishwa kutokana na maji, (Hydro powere) kutoka vituo vinne vya umeme wa maji vya Kidatu, Mtera, New Pangani Falls, Hale na Nyumba ya Mungu.
Hata hivyo katika siku za karibuni shughuli za kibinadamu zimekuwa zikiongezeka kwenye vyanzo vya maji yanayoelekea kwenye vituo vya kufua umeme, na hivyo kutishia shuhghuli za uzalishaji umeme kwenye vituo hivyo. Mhandisi Ikwasa alitoa mfano Mto Pangani ambapo yapo maeno ambayo shughuli za kilimo zinaendelea karibu na mto, na madhara yatokanayo na shughuli hizo hupelekea kingo za mto kuwa dhaifu na wakati wa mvua maji yanachukua udongo na kuingiza kwenye mto na hivyo kina cha mto kinakuwa kifupi.
Wasimamizi wa kituo cha kudhibiti mfumo wa umeme cha Mtera.
“Sasa kipindi ambacho mvua zinanyesha unatarajia maji mengi yatiririke kwenye mto lakini kwa sababu kina kimepungua mto hauwezi kubeba yale maji na badala yake maji yanasambaa na kusababisha mafuriko na mbaya zaidi hayafiki kwenye mabwawa kwa kiwango kinachohitajika.” Alisema Mhandisi Ikwasa. Alisema TANESCO kama wadau wakubwa wa maji wamekuwa wakishirikiana na mamlaka zinazosimamia mabonde, ili kuelimisha watumiaji wengine wa maji.
“Tunataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na matumizi endelevu ya maji, tunatambua wananchi wanahitaji maji kwa kilimo na sisi tunayahitaji kwa uzalishaji umeme kwa hivyo yakitumika vizuri yanaweza kufanya kazi zote.” Alisema.
Mhandisi Ikwasa aliipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inazochukua kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa.
“Makamu wa Rais aliunda kikosi kazi cha kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa na juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda.” Alisema.
Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bi. Leila Muhaji, akizungumza jambo.
Ili kuhakikisha wananchi wanajenga dhana ya umiliki wa miundombinu ya TANESCO, Shirika limekuwa likishirikiana na wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kusaidia kutoa huduma za afya, elimu ya awali na usafiri katika maeneo yanayozunguka vituo vya kuzalisha umeme.
“Tunataka wananchi wafahamu kuwa pamoja na kwamba kazi yetu ni kuzalisha umeme, lakini tunataka tuwe sehemu ya maisha yao, kwa kusaidia mambo ya kijamii kama vile kutoa elimu bure ya awali, zahanati, na usafiri wa basi unaosaidia wananchi kusafiri kuelekea kwenye shughuli zao, tunadhani kwa ushirikiano huu, wananchi watakuwa wakwanza kulinda miundombinu yetu na pia kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwenye vyanzo vya maji.” Alisema Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bi. Leila Muhaji.
Ili kuhakikisha ujumbe huo pia unawafikia wananchi wote kupitia vyombo vya habari, wahariri wa vyombo vya habari walipata fursa ya kutembelea vituo vya kufua umeme wa maji vya Hale, New Pangani na Nyumba ya Mungu, vilivyoko mikoa ya Tanga na Kilimanjaro, kituo cha Mtera kilichoko mkoani Iringa na Kidatu mkoani Morogoro ili hatimaye watoe elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ya vyanzo vya mito ambayo maji yake ndio huelekea kwenye vituo vya kufua umeme.
Meneja wa kituo cha kufua umeme wa maji cha Kidatu, Mhandisi Anthony Mbushi, (kushoto), akizungumza kuhusu jinsi mageti ya kuruhusu maji kwenye mabwawa kwenda kwenye mitambo ya kufua umeme yanavyofanya kazi. Kulia ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, anayeshughulikia uzalishaji umeme. Mhandsisi Abdallah Ikwasa.
Wananchi wa Kidatu, wakisub iri usafiri wa basi la Shirika la Umeme TANESCO, kuwapeleka kwenye mnada ili kuuza mazao yao. Usafiri huo hutolewa bure na Shirika katika mpango wake wa Corporate Social Responsibility (CSR) ili kujenga uhusiano mwema.
Moja ya mashine za kufua umeme wa maji, (turbine), kituo cha Hale.
Bwawa la New Pangani Water Falls.
Mhandisi Mahenda S.Mahenda, Meneja vituo vya kufua umeme vya Pangani Hydro Systems, akifafanua jambo.
No comments:
Post a Comment